Dar es Salaam. Wakati Bara la Afrika likiwa kwenye mtanziko kuhusu kusitishiwa misaada ikiwemo dawa za ARV, malaria na kifua kikuu, utawala wa Rais wa Marekani Donald Trump umeondoa agizo la kusitisha mikopo ya shirikisho, ruzuku na misaada mingine ya kifedha.
Jaribio la Rais Trump kufungia mabilioni ya dola katika ufadhili wa Serikali lilizuiliwa kwa muda mahakamani.
Mpango huo wa Trump umesababisha mitazamo tofauti serikalini na kuzua hofu kwamba litavuruga programu zinazowahudumia mamilioni ya Wamarekani na kutatiza sekta za elimu, huduma za afya, makazi, misaada ya majanga na programu nyingine.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari ya Reuters, hayo yameelezwa jana Januari 29, 2025 na Ofisa wa Ikulu muda mfupi kabla ya kufika mahakamani kwa siku ya pili mfululizo kutetea sera hiyo.
Uamuzi wa kuondoa agizo la Ofisi ya Usimamizi na Bajeti (OMB) lililotolewa Jumatatu, ulifanyika muda mfupi kabla ya jaji wa shirikisho katika Rhode Island kuanza kusikiliza ombi la majimbo 22 yanayoongozwa na chama cha Democratic pamoja na Wilaya ya Columbia, la kutaka zuio la muda dhidi ya sera hiyo, wakisema inaweza kuwa na athari mbaya kwa bajeti zao.
Amri kama hiyo kutoka kwa Jaji Mkuu wa Mahakama ya Wilaya ya Marekani, John McConnell, ingeweza kuwa ya muda mrefu zaidi kuliko ile iliyotolewa na Jaji wa Wilaya ya Marekani Loren AliKhan siku ya Jumanne katika kesi tofauti iliyofunguliwa na mashirika yasiyo ya faida katika mahakama ya shirikisho ya Washington, D.C.
Amri ya Rais Donald Trump ilizua sintofahamu serikalini Jumanne Januari 28, 2025 na ilionekana kuvuruga malipo kwa watoa huduma za matibabu na walezi wa watoto.
Ilikuwa mojawapo ya juhudi kadhaa za kuunda upya Serikali ya shirikisho tangu alipoingia madarakani Januari 20, 2025.
Wanachama wa Chama cha Democratic walisema ilikuwa ni shambulio lisilo halali dhidi ya mamlaka ya Bunge juu ya matumizi ya fedha za shirikisho, huku Republican wakitetea kuwa ilikuwa ni utekelezaji wa ahadi ya kampeni ya Trump ya kupunguza bajeti ya shirikisho ya Dola trilioni 6.75.
Katika kesi ya kupinga hatua hiyo, mawakili wa majimbo 23 walidai kuwa sera hiyo haikuwa ya kikatiba kwa sababu Bunge lilikuwa tayari limeamua jinsi fedha hizo zingetumika. Pia walisema ingeweka hatarini fedha za misaada ya majanga kusaidia kusini mwa California kujenga upya baada ya moto wa nyika.
“Rais hana mamlaka ya kuamua ni sheria zipi zitatekelezwa na kwa nani,” alisema Mwanasheria Mkuu wa Jimbo la New York, Letitia James, alipokuwa akitangaza kesi hiyo Jumanne.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la BBC, limeripoti kuwa Jaji wa Marekani amesitisha kwa muda amri ya Rais Donald Trump ya kusimamisha mamia ya mabilioni ya dola katika ruzuku na mikopo ya shirikisho, dakika chache kabla ya utekelezaji wake.
Amri ya Jaji Loren AliKhan ya kusitisha mpango huo ilitolewa baada ya shauri lililofunguliwa mapema siku hiyo na mashirika yanayowakilisha wapokeaji wa ruzuku.
Kesi hiyo inadai kuwa hatua ya Ikulu ya Marekani ya kusimamisha kwa muda ufadhili ambao tayari ulikuwa umeidhinishwa ni kinyume cha sheria.
Katika saa chache kabla ya agizo hilo kuanza kutekelezwa, kulikuwa na mkanganyiko mkubwa kuhusu ni mashirika gani na programu zipi zingekumbwa na athari.
Kaimu mkuu wa ofisi ya bajeti ya Ikulu alikuwa ameelekeza mashirika, “kusitisha kwa muda shughuli zote zinazohusiana na matumizi au utoaji wa msaada wowote wa kifedha wa shirikisho.”
Ilielezwa kuwa hatua hiyo ilikusudia kuipa serikali mpya muda wa kutathmini ruzuku na mikopo ipi inaendana na ajenda yao.
Msemaji wa Ikulu, Karoline Leavitt, alisema mpango wa Trump wa kusitisha mabilioni ya dola za serikali ya Marekani ulikuwa ni hatua ya kuwa “wasimamizi wazuri wa kodi za wananchi.”
Akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano wake wa kwanza kabisa, alisema kusitishwa kwa ufadhili huo kungeruhusu serikali kupunguza matumizi kwa programu zinazohusiana na masuala ya jinsia na utofauti wa kijamii.
Lakini hatua hiyo ilisababisha mkanganyiko na hasira kutoka kwa wapinzani Januari 28, huku wapokeaji wa mikopo na ruzuku za shirikisho kama mashirika yasiyo ya faida na taasisi za utafiti wakijaribu kuelewa athari za kupoteza ufadhili ghafla.
Jaji AliKhan alisema Jumanne kuwa alitoa zuio la muda ili “kudumisha hali ilivyo” hadi atakapofanya kikao cha kusikiliza hoja Jumatatu (Februari 3, 2025) asubuhi.
Agizo la Ikulu lingeweza kuathiri mabilioni ya dola zilizotengwa kwa programu za shirikisho, kutoka kwa misaada ya maafa hadi utafiti wa saratani.
Katika chapisho kwenye mtandao wa X, Diane Yentel, rais wa Baraza la Kitaifa la Mashirika Yasiyo ya Faida, shirika lililofungua kesi hiyo, alisherehekea uamuzi huo.
“Kesi yetu imefaulu, mahakama ya wilaya ya Marekani imezuia OMB (Ofisi ya Usimamizi na Bajeti) kutekeleza mpango wake usio wa busara wa kusitisha ufadhili wa shirikisho,” aliandika.
Katika kesi hiyo, shirika lake liliandika kuwa agizo la Trump linajaribu, “kuondoa karibu programu zote za ruzuku za shirikisho.”
Imeandikwa na Herieth Makwetta na mashirika