Dar es Salaam. Uvumbuzi wa hivi karibuni wa programu ya Kichina iitwayo DeepSeek katika uwanja wa akili bandia (AI) umetikisa sekta ya ubunifu duniani na kuathiri thamani ya kampuni nyingine zinazotoa huduma kama zake katika masoko ya hisa.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ukurasa wa Instagram wa Wealth, kampuni hiyo imefanikiwa kuunda aina ya AI inayofanana na ChatGPT ya OpenAI kwa gharama nafuu zaidi, jambo ambalo limeibua mjadala kuhusu matumizi makubwa ya fedha za Marekani katika teknolojia.
Baada ya kutambulishwa kwa DeepSeek, athari zake zilionekana moja kwa moja kwenye soko la hisa la Marekani, ambapo thamani ya hisa za kampuni ya teknolojia ya Nasdaq ilishuka kwa zaidi ya asilimia 3.
Vilevile hisa za kampuni ya NVIDIA, moja ya makampuni makubwa ya teknolojia nchini Marekani, ziliporomoka kwa karibu asilimia 17.
Rais wa Marekani, Donald Trump, ameelezea ujio wa ubunifu huo kama kengele ya kuwaamsha Wamarekani, akisema “China imetufanya tuamke. Tunapaswa kujifunza kutoka kwenye mbinu zao za gharama nafuu ya kutumia fedha kidogo lakini upate matokeo makubwa”.
Trump aliongeza kuwa uvumbuzi wa DeepSeek unatoa fursa kwa Marekani kujipanga upya na kuboresha mipango yake ya kiteknolojia. “Hatuwezi kuacha nchi nyingine kutuacha nyuma. Huu ni wakati wa kufanya mabadiliko makubwa”
Moja ya mambo yaliyowashangaza wataalamu ni jinsi DeepSeek ilivyofanikiwa kuunda AI yao kwa gharama ya Dola za Marekani 5.6 milioni (Sh14.3 bilioni) wakati kampuni kama OpenAI zinatumia zaidi ya Tsh254.5 bilioni kwa miradi kama hiyo.
Ufanisi huu umeibua wasiwasi kwamba gharama kubwa za vifaa vya NVIDIA zinaweza kutokuwa muhimu tena kwa kiwango kilichokuwa kikitegemewa hapo awali.
Hali hii ilisababisha NVIDIA kupoteza thamani ya soko yenye jumla ya Sh1.52 trilioni katika siku ya kwanza ya kutambulishwa kwa DeepSeek, ikiwa ni hasara kubwa zaidi kuwahi kutokea katika historia ya kampuni za Marekani.
Hata hivyo kuna wasiwasi kwa DeepSeek kukataliwa kwenye soko la Marekani.
Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni kutoka Polymarket, kuna uwezekano wa asilimia 13 kwamba DeepSeek itakataliwa Marekani kufikia Aprili.
Hata hivyo, asilimia hii ni ndogo ikilinganishwa na makadirio ya awali, jambo linaloonyesha kwamba wataalamu na wawekezaji wanapata mtazamo wenye matumaini zaidi.