Bukombe. Vilio na simanzi vimetawala katika viwanja vya Shule ya Sekondari Businda wakati miili saba ya wanafunzi waliopoteza maisha kwa kupigwa na radi ikiagwa leo Alajsi Januari 30, 2025 kabla ya kwenda kuzikwa.
Tukio la wanafunzi kupigwa radi lilitokea Januari 27, 2025 wakati wakiwa darasani wakiendelea na masomo, katika ajali hiyo wanafunzi saba walipoteza maisha na 82 kujeruhiwa.
Katika viwanja vya shule ya Businda, maelfu ya wananchi waliohudhuria, baadhi walikuwa wamekaa kwenye viti huku wengine wakisimama na kila familia iliyopata msiba ikitengewa hema ambalo walikaa pamoja na ndugu zao.
Mwananchi limeshuhudia watu wakishindwa kujizuia kuangua vilio huku wengine wakianguka na kuzimia na kusaidiwa na watu wa huduma ya kwanza pamoja na vijana wa mgambo waliokuwa kila eneo la uwanja huo.
Ibada ya kuaga wanafunzi hao imefanyika katika viwanja vya shule hiyo iliyopo Mji Mdogo wa Ushirombo na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini, Serikali na maelfu ya wananchi wa Bukombe.
Kabla ya miili kuletwa uwanjani mapema asubuhi, viongozi wa dini walipata nafasi ya kufanya ibada kwenye familia kila moja kwa imani zao na badaye kwa pamoja wakaungana na viongozi na wananchi kwa ajili ya kuaga kwa pamoja.
Katika viwanja hivyo, viongozi wa dini za kiislam,Wasabato,Pentekoste na Katoliki walitoa salamu za pole na kuwasihi wananchi kuwa wavumilivu kwa kuwa kifo hakivumiliki na yote ni mapenzi ya Mungu.
Wakati wa kusoma historia ya wanafunzi hao waombolezaji walishindwa kujizuia na kuangua vilio na minong’ono pindi msoma historia alipowataja wanafunzi wawili ambao kila mmoja ni mtoto pekee kwenye familia yake.
Wanafunzi walionusurika kwenye tukio hilo walikaa pamoja na wanafunzi wengine na wakati wote walionekana wakifuta machozi na wakati wa kuaga wengi walishindwa kumaliza safari ya kuaga na kulazimika kubebwa na kuondolewa kwenye eneo hilo kwa msaada zaidi.
Manusura aeleza ilivyokuwa
Mmoja wa manusura wa ajali hiyo ya radi, Shedrack Elisha amesema siku ya tukio wakiwa darasani huku mvua ikinyesha, alisikia harufu ya moto wa makuti na hajui kilichoendelea hadi pale alipojikuta yuko hospitali.
“Wanafunzi walikuwa wakipiga kelele sana, waliokuwa dawati la mbele yangu wote wamefariki, inaumiza sana, hatuna cha kusema zaidi ya kumshukuru Mungu maana ni mapenzi yake.
Amesema waliopoteza maisha ni wale waliokuwa wamekaa upande wa dirishani na kwamba yeye ameumia mguu na licha ya kuruhusiwa kutoka hospitali, bado hawezi kutembea vizuri na yuko kwenye maumivu makali ya mguu.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Theodora Mushi amesema siku ya tukio, Januari 27, 2025, wanafunzi zaidi ya 100, wakiwa darasani, walipigwa na radi na saba kati yao walipoteza maisha huku wengine watatu wakipoteza maisha wakati wakipatiwa matibabu na wengine 82 wakijeruhiwa.
Amewataja waliopoteza maisha kuwa ni Erick Bugalama, Peter Manyanda ambaye ni mtoto pekee wa wazazi wake, Doto Masasi, Gabriel Makoye, Astera Mkina, Nicas Tonpoli na Erick Akonay ambaye ni mtoto pekee katika familia.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Doto Biteko, akiongoza shughuli ya kuaga miili saba ya wanafunzi hao wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Businda iliyoko Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, ametoa pole kwa waliopoteza wapendwa wao.
Biteko ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Bukombe, amesema tukio lililotokea ni la majonzi na amewapa pole familia zilizoondokewa na wapendwa wao kwa kuwa sio jambo la kawaida lakini hakuna neno zaidi ya pole.
“Niwape pole sana wana Businda, niliona mlivyohangaika kuokoa maisha ya wengine waliojeruhiwa kwa kuwakimbiza hospitali ili wapate huduma, mmefanya jambo jema kuokoa maisha ya wengine, upendo wenu hasa wakati wa matatizo umekuwa faraja,” amesema Biteko.
Naibu Waziri Mkuu amewashukuru watoa huduma wote waliojitoa kwa moyo kuwasaidia wanafunzi waliokuwa wamezimia, akisema kifo ni fumbo na unaweza kukwepa jambo lolote lakini sio kifo.
Amesema wameamua kuaga kwa pamoja kwa kuwa sio tukio la kawaida kutokea na amewataka wazazi kumshukuru Mungu kwa kila jambo na tukio hilo liwe ukumbusho kwa waliobaki kutenda mema.
Bitoko ametoa salamu za Rais Samia Suluhu Hassan amesema Rais Samia ametoa pole kwa jamii ya Biteko na kuamua kugharamia gharama za maziko na ubani kwa kila familia iliyokutwa na msiba.
Mkuu wa Mkoa wa Geita amewataka wananchi kumtanguliza Mungu katika kila jambo wanalolifanya kwa kuwa kifo hakizoeleki na kuwasihi wafiwa kuwa na moyo wa uvumilivu.
Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Paskas Muragili, akitoa salamu za pole, amesema tukio hilo lilitokea saa 8:20 mchana wakati wanafunzi wakiwa darasani na waliogundua ni wanafunzi wa kidato cha pili na nne ambao walipeleka taarifa kwa walimu.
Amesema madarasa hayo mawili yalikuwa na wanafunzi 138 na walioathirika moja kwa moja ni wanafunzi 89 na 82 walipelekwa hospitali kwa matibabu na tayari wameruhusiwa na kuungana na familia zao.
“Hawa saba tunaowaaga leo, wanne walipoteza maisha hapohapo kwenye tukio na watatu walifikishwa wakiwa mahututi na walipoteza maisha wakiendelea na huduma, niwashukuru sana madaktari wa binafsi na wale wa Serikali wamejitoa sana kuwahudumia,” amesema Biteko.
Askofu wa Jimbo Katoliki Geita, Flavian Kassala amesema kipindi hiki ni cha kutafakari na kumuomba Mungu awe faraja.
“Maisha yetu yanapita lakini tunalo tumaini kubwa zaidi katika Kristo Bwana wetu tumuendee yeye, atuvushe kama sisi binadamu bado tunayo nafasi ya kushirikiana na Mungu kufanye dunia iwe sehemu ya faraja,” amesema.
Ameshauri pale inawezekana kukinga nguvu za asili ambazo zinatuzunguka ni vema zikafanyika na kuweka juhudi za kupunguza majanga yanayoweza kuikuta jamii.