Siha. Watumishi wawili wa Bodi ya Maji Magadini Makiwaru, Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, wamesimamishwa kazi kwa tuhuma za kuwaunganishia huduma ya maji wananchi 63 kinyume cha utaratibu.
Watumishi hao ambao ni mafundi wa bodi hiyo, wanadaiwa kuwaunganisha wananchi hao kwenye huduma ya maji bila kuwajumuisha kwenye mfumo wa malipo, jambo lililosababisha upotevu wa mapato ya Sh9.5 milioni.
Meneja wa Bodi hiyo, Ezekiel Maningo akizungumza leo Alhamisi, Januari 30, 2025, amesema tatizo hilo lilibainika mwishoni mwa Julai, 2024 baada ya kuona upungufu wa maji licha ya uzalishaji kuwa mkubwa.
“Tulianza kuona upungufu wa maji na kujiuliza yanapotelea wapi ilhali tunazalisha kwa wingi. Kufuatia hilo, tulianza ufuatiliaji kwa kushirikiana na wananchi, ndipo tukagundua kuwa baadhi yao waliunganishiwa maji kinyume cha utaratibu,” amesema Maningo.
Ameongeza kuwa uchunguzi ulibaini kuwa mafundi wanane walihusika katika sakata hilo, na wawili wamesimamishwa kazi kwa kuhusika kwa kiwango kikubwa, huku wengine sita wakitakiwa kurejesha fedha na uchunguzi ukiendelea.
“Hata hivyo, uchunguzi unaendelea na endapo watabainika na makosa mengine, hatua zaidi zitachukuliwa dhidi yao,” amesema Maningo.
Mwenyekiti mstaafu wa Kijiji cha Magadini, Munguatosha Kessy amesema sakata hilo lilibainika mwaka 2024 baada ya wananchi kulalamikia ukosefu wa huduma ya maji katika mkutano wa kijiji.
“Wananchi walilalamika maji kutopatikana, ndipo bodi ilipoanza kufuatilia na kugundua kuwa baadhi ya watu walipewa huduma hiyo kinyume cha utaratibu. Hatua zilichukuliwa, ikiwa ni pamoja na kufikisha wahusika kwenye vyombo vya sheria,” amesema Kessy.
Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Kilimanjaro, Musa Chaulo amesema uchunguzi wao ulibaini baadhi ya wananchi waliunganishiwa maji bila mita, huku wengine wakiwa na mita lakini hawakuwa kwenye mfumo wa malipo ya bili za maji.
“Tulibaini kuwa jumla ya wateja 63 walipata huduma ya maji bila kuingizwa kwenye mfumo wa malipo, na hivyo kusababisha upotevu wa mapato ya Sh9.5 milioni,” amesema Chaulo.
Hata hivyo, amesema baada ya uchunguzi huo, Takukuru ilihakikisha wateja hao wanaingizwa kwenye mfumo wa malipo, ambapo kufikia Desemba 23, 2024, kiasi cha Sh3.6 milioni kilikuwa tayari kimeingizwa kwenye akaunti ya maji ya Magadini Makiwaru, huku wadaiwa wengine wakiendelea kulipa.