Baada ya Goma, M23 yatangaza kuitafuta Kinshasa, Tshisekedi aapa kupambana nao

Goma. Kiongozi wa Kundi la M23, Corneille Nangaa amesema baada ya kuukamata mji wa Goma, wataendelea na mapigano hadi mji mkuu wa nchi hiyo, Kinshasa.

Kundi la M23 linadaiwa kufadhiliwa na Serikali ya Rwanda, huku nchi hiyo ikikanusha madai hayo.

Juzi kwenye mkutano wa dharura wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Rais Paul Kagame, alisema lengo la vikosi vya Jeshi la Ulinzi la Rwanda (RDF) nchini Congo ni kuwaondoa wapiganaji waliohusika kwenye mauaji ya kimbali ya mwaka 1994 waliokimbilia nchini humo.

Tovuti ya The Africa Report imeripoti kuwa Nangaa amesema uamuzi wa kuandamana hadi Kinshasa, unalenga kuikomboa nchi wakati huu ambao wapiganaji wa kundi hilo wanaendelea kuyakamata maeneo ya mashariki yenye utajiri wa madini.

“Tutaendelea kusogea na kuyakomboa maeneo mengine zaidi hadi tutakapofika Kinshasa,” amesema Nangaa ambaye ni kiongozi wa makundi ya waasi, ikiwemo M23, alipozungumza na vyombo vya habari mjini Goma jana Alhamisi.

“Sasa hivi tuko Goma na hatutaondoka hadi pale sababu zilizotufanya tukamate silaha na kuingia mtaani zitakapokuwa zimeshughulikiwa,” amesema.

Ameahidi kuwa kundi hilo litahakikisha huduma za msingi ikiwemo usalama na umeme unarejeshwa katika Mji wa Goma na misaada ya kibinadamu itarejeshwa siku za usoni katika mji huo.

Kiongozi huyo wa waasi ametoa kauli hiyo baada ya Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Felix Tshisekedi kuahidi vikosi vyake vita vitaendeleza mapigano kukabiliana na waasi hao Jumatano.

 “Tunajipanga na tutapambana na hawa magaidi na wanaowafadhili ipasavyo,” alisema Tshisekedi.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la AFP, waasi wa M23 baada ya kuiteka Goma, wameanza kujitanua kutokea Kivu Kaskazini kwenda Jimbo la Kivu Kusini.

Mapigano hayo eneo la Goma yamesababisha vifo vya watu zaidi ya 100 huku zaidi ya 1,000 wakijeruhiwa na makumi kwa maelfu wakiyakimbia makazi yao kutafuta hifadhi eneo la lenye amani.

Tayari Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean-Noel Barrot amewasili leo Alhamisi Januari 30, 2025, nchini DRC kwa lengo la kukutana na Rais Tshisekedi.

Wakati huo, Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ni Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), amewasili jijini Harare nchini Zimbabwe kwa ziara ya kikazi ya siku moja kuhusiana na suala hilo.

Rais Samia akiwa Zimbabwe atashiriki mkutano wa dharura wa wakuu wa nchi na Serikali wa SADC ulioitishwa kwa lengo la kujadili hali ya ulinzi na usalama Mashariki mwa DRC.

Mkutano huo utaongozwa na Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe ambaye ni Mwenyekiti wa SADC, Emmerson Mnangagwa.

Mkutano huo unafanyika kufuatia Mkutano wa dharura wa utatu wa wakuu wa nchi na Serikali wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama (SADC Organ Troika), nchi zinazochangia askari katika Misheni ya SADC nchini DRC (SAMIDRC), uliofanyika Januari 28, 2025.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika.

Related Posts