Wadau wa michezo nchini, ndugu, jamaa, marafiki, wanasiasa na wakazi wa Jiji la Mwanza wameuaga mwili wa Mkurugenzi wa Kituo cha Michezo na Shule za Alliance, James Bwire na kesho Jumamosi utasafirishwa kwenda kuzikwa kijijini kwao Nyamwaga, wilayani Tarime, mkoani Mara, Jumapili.
Bwire ambaye enzi za uhai wake alikuwa mdau wa michezo nchini kupitia kituo cha kukuza na kulea vipaji cha Alliance amezalisha wachezaji wanaotamba ndani na nje ya nchi.
Alifariki dunia Januari 25, 2025, Saa 4 usiku wakati akipatiwa matibabu Hospitali ya Rufaa ya Bugando, jijini Mwanza.
Waombolezaji hao wameongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wilfred Kidao na Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi (TPLB), Almasi Kasongo pamoja na wadau mbalimbali kutoka nyanja ya michezo, siasa na elimu.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wilfred Kidao amesema sekta ya michezo nchini imepoteza mtu muhimu ambaye amekuwa mhimili mkubwa katika maendeleo ya soka nchini.
Amesema kituo cha Alliance kimezalisha wachezaji wengi ambao ni tegemeo kwa timu za taifa na wengine wanacheza nje ya nchi ambao baadhi ya ada za uhamisho wao zinapaswa kuinufaisha Alliance, hivyo, watafanya mazungumzo na familia ya James Bwire ili kupata fedha hizo.
“Sisi TFF tumeguswa na huu msiba Alliance kilikuwa ni kituo chetu cha kimkakati vijana wengi wametoka hapa tumefanya vitu vikubwa chini ya Alliance. TFF tutahakikisha tunaendeleza na maono ya Bwire ili yadumu,” amesema Kidao na kuongeza;
“Hata ndoto za vijana wenye vipaji vinatimizwa bila changamoto zozote, kwa hiyo tutakaa na wanafamilia na tutaongea kwa sababu kuna fedha ambazo zinatokana na vijana wanaocheza Ulaya ambao wamelelewa hapa, tutakaa kuona familia inanufaika nazo vipi.”
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amesema James Bwire atakumbukwa kwa mambo muhimu matatu ambayo ni mwanamichezo aliyetoa heshima kwa mkoa huo kwa kuhakikisha unapata timu ya Ligi Kuu, alikuwa jemedari wa kuongoza mapambano ya kitaaluma ili kuinua maendeleo ya elimu na alikuwa kiongozi shupavu.
Mtanda ameiomba jamii kuiunga mkono familia ya mkurugenzi huyo kwa kuendeleza ndoto alizoziishi na kutamani kuzitimiza ili kuhakikisha shule za Alliance zinaendelea na hazipotezi mwelekeo.
“Nilimfahamu Bwire miezi michache iliyopita alikuja ofisini mara mbili lakini tulionana mara moja akaniomba nimsaidie timu ya wasichana (Alliance Girls) itashuka daraja, akasema nina imani ukiingiza nguvu yako kidogo timu hii haitashuka daraja,” amesema Mtanda
Ameongeza; “Walikuwa wamebakiza mechi tatu dhidi ya Yanga Princess, Baobab Queens na Ceassia Queens kwa hiyo nilifanya kazi ambayo yeye alinitaka nifanye na bila shaka Alliance Girls haikushuka daraja.”
Mwakilishi wa umoja wa vijana waliosoma Alliance, Jimmyson Masinga amesema; “Ametufundisha kufanya kazi kwa juhudi ili kuleta maendeleo kwa taifa na alitulea katika misingi ya usawa. Alikuwa anaweza kuamka saa 10 usiku kuja kutukagua mabwenini, kwa hiyo alifanya shule kuwa kama sehemu ya familia yake.”
Baadhi ya wanasiasa, Charles Chinchibela (Chadema) amesema alimshinda James Bwire kwenye uchaguzi wa nafasi ya Diwani kata ya Mahina mwaka 2010 lakini hakukata tamaa na mwaka 2015 aligombea tena na kushinda.
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi amesema wilaya hiyo imempoteza mdau mkubwa wa maendeleo na mwekezaji katika sekta ya elimu na maendeleo.
“Alikuwa mstari wa mbele kuungana na Serikali katika suala la maendeleo na kushirikiana na jamii na wana Mahina, ni mtu wa watu tumeondokewa na mtu ambaye tulikuwa tunamtumainia,” amesema Makilagi.
James Bwire (56) alizaliwa Disemba 7, 1969 katika kijiji cha Kisangola Kata ya Nyamwaga wilayani Tarime Mkoa wa Mara akiwa ni mtoto wa kwanza kati ya watoto tisa wa familia ya Bwire Manga.
Bwire ambaye alianza kusumbuliwa na maradhi ya Moyo tangu mwaka 2016 ameacha watoto saba wakiwemo wanne wa kiume na watatu wa kike na wajukuu wawili.