Alhamisi Januari 30, 2025 itakumbukwa kuwa siku iliyoacha huzuni kwa wanazuoni, masheikh, wanafunzi wa taaluma za dini ya Kiislamu na Waislamu wa Tanzania kwa kuondokewa na Sheikh Mohamed Iddi Mohamed Husein Kisodya Mahede, maarufu kwa jina la Sheikh Abuu Iddi.
Huyu alikuwa mwanazuoni maarufu wa Kiislam na Mratibu wa Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania. Kifo kimetunyang’anya mwanazuoni huyu wa daraja ya juu, ambaye mpaka anarudi kwa Mola wake, jamii ya Kiislamu nchini imeshindwa kumtumia na kufaidika naye ipasavyo. Kifo ni nini?
Kifo ni maendeleo kwa maana ya mabadiliko yanayomtoa mwanadamu kutoka katika hali moja hadi nyingine. Moja ya maana ya kifo ni kutengana roho na mwili baada ya kuunganishwa kwa njia ya kupuliziwa roho katika mwili pale mimba inapofikisha arobaini ya tatu au siku 120 tangu ilipotungwa.
Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) ameuelezea mchakato huu wa makuzi ya mimba katika Hadith kutoka kwa Swahaba Abuu
Abdir-Rahmaan Abdillaah bin Mas-uud (Allaah Amridhie) ambaye amesema: “Ametusimulia Mjumbe wa Allaah (Allaah amrehemu na ampe amani) ambaye ni mkweli mwenye kuaminiwa: “Hakika kila mmoja wenu hukusanywa umbo lake katika tumbo la mama yake siku arobaini akiwa ni mkusanyiko wa mbegu (za uzazi za mama na baba), kisha arobaini zijazo huwa ni donge la damu, kisha arobaini zijazo huwa pande la nyama, kisha Allaah humtuma malaika kwake na kumpulizia roho (yake). Na (malaika huyo) anaamrishwa maneno manne; Kuandika riziki yake, ajali yake (umri atakaoishi duniani), amali zake, na (ni) mtu muovu au mwema. Wallaahi! naapa kwa Yule ambaye hakuna muabudiwa wa haki isipokuwa Yeye, hakika mmoja wenu huenda afanye amali za watu wa peponi hadi ikawa kati yake na Pepo ni dhiraa na kile kilichoandikwa kikathibiti akafanya amali ya watu wa motoni akaingia motoni. Na mmoja wenu hufanya amali za watu wa motoni hadi ikawa kati yake na moto ni dhiraa na hapo kile kilichoandikwa kikathibiti akafanya amali ya watu wa peponi akaingia peponi.” [Hadith hii inapatikana katika vitabu cha Hadith za Mtume Muhammad viitwavyo Sahih Al-Bukhary na Sahih Muslim]
Tunafundishwa hapa kuwa kifo si kuangamia kwa roho bali kutengana roho na kiwiliwili chake kama tukio hilo linavyotokea kwa kila mmoja wetu pale anapolala.
Tunasoma katika Qur’aan Tukufu Sura ya 39 (Surat Az-Zumar), aya ya 42 kuwa: “Mwenyeezi Mungu huzipokea roho zinapokufa. Na zile zisizokufa (huzipokea) wakati wa kulala kwake, huzishika zilizohukumiwa kufa, na huzirudisha nyingine mpaka ufike wakati uliowekwa. Hakika katika hayo bila ya shaka zipo ishara kwa watu wanaofikiri.”
Kufa kwa roho hapa ni kule kutengana na kiwiliwili chake ili kutimiza ule muda wa uhai na maisha ya mwanadamu duniani. Roho haifi bali huonja utengano baina yake na kiwiliwili.
Mwanadamu ana umauti wa aina mbili na uhai wa aina mbili. Kabla ya roho kupulizwa katika mwili pale mimba inapotimiza siku 120, mwanadamu anahesabiwa kuwa katika hali ya umauti (umauti wa kwanza). Roho ikipulizwa anauanza uhai wa kwanza hadi pale anapoufikia umauti wa pili, tunaoujua sana, ili afikie uhai wa pili, wa mwisho na wa milele.
Tunasoma katika Qur’aan Tukufu Sura ya 2 (Surat Al-Baqarah), Aya ya 28: “Vipi mnamkanusha Mwenyezi Mungu na hali mlikuwa wafu, akakufufueni! Kisha atakufisheni, tena atakufufueni, kisha kwake mtarejeshwa?”
Kwa nini leo tunazungumzia kifo?
Januari 30, mwaka huu tumeshuhudia kutangulia kurudi kwa Mola wetu Mlezi mmoja wa wanazuoni wa daraja la juu ambaye elimu yake ya dini haitiliwi shaka Sheikh Mohamed Iddi Mohamed aliyefariki jijini Dar es Salaam na kuzikwa katika Makaburi ya kijiji cha Mkata, wilaya ya Handeni, mkoani Tanga baada ya Swala ya Ijumaa.
Hadi anafariki, marehemu alikuwa ni mshauri wa mambo ya dini na jamii wa Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Abubakar Zubeir bin Ally Mbwana, mwalimu wa taaluma za Kiislamu na lugha ya Kiarabu na elimu za Kiislamu ambaye elimu yake haitiliwi shaka. Pia alikuwa kiongozi wa taasisi za Kiislamu; Arrisaalah Islamic Foundation na mratibu wa Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania.
Marehemu Sheikh Abuu Iddi aliyefariki akiwa na umri wa miaka 56, ni miongoni mwa wanafunzi wa daraja ya juu wa mwanazuoni mtengeneza wanazuoni marehemu Sheikh Muhammad bin Ayyubu bin Khamis Alkamaadhy (Allaah amrehemu).
Sheikh Abuu Iddi Mohamed Iddi ni nani?
Marehemu Sheikh Abuu Iddi ni mwanazuoni aliyeruzukiwa akili razini na ufahamu wa hali ya juu kiasi cha kuweza kutumia taaluma za lugha ya Kiarabu alizojaaliwa kuwa nazo, kujiongezea elimu kwa kusoma taaluma mbalimbali na vitabu vitabu bila ya kuhitaji msaada isipokuwa mara chache sana.
Inasimuliwa kuwa marehemu Sheikh Muhammad bin Ayyubu, alimuamini marehemu Sheikh Abuu Iddi na kumbebesha baadhi ya majukumu akiwa chuoni Shamsiyyah (TAMTA) pamoja na udogo wake wa umri wakati huo.
Ushahidi mwingine wa kuaminika hata kitaaluma ni kupewa nafasi ya kuwasomesha wanafunzi wenziwe, kuaminiwa katika kutoka huduma ya tafsiri na ukalimani kwa wahadhiri wageni kutoka nchi za Kiarabu na kushiriki kikamilifu katika kikundi cha mijadala maarufu “Sumba Mrars”.
Sheikh Abuu Iddi alikuwa ni miongoni mwa wanazuoni wenye uhusiano mkubwa na watu mbali, akiamiliana kwa unyenyekevu na wakubwa kwa wadogo na alitumia muda wake mwingi kutoka ushauri wa kidini na kusuluhisha migogoro.
Sheikh Muhammad Iddi alizaliwa Tanga, maeneo ya Mkata, mwaka 1969 na alianza kusoma Qur’aan kabla ya kujiunga na Tamta mwaka 1984 na baada ya hapo hakusoma popote isipokuwa kwa Marehemu Sheikh Muhammad bin Ayyubu hadi kufikia daraja ya ualimu.
Marehemu Sheikh Muhammad Iddi Mohamed ameacha wajane watatu na watoto 11.
Mbali ya kusomesha Sheikh Abuu Iddi alikuwa mwandishi mzuri aliyeandika makala mbalimbali magazetini na vitabu kikiwemo kitabu “Misingi 15 ya Amani”.
Tunamuomba Allaah Mtukufu amrehemu mja wake Sheikh Abuu Iddi Mohamed Iddi Mohamed, mwanazuoni mahiri na mwanajamii.
Sheikh Abuu Iddi Mohamed Iddi Mohamed atabakia mfano wa mwanazuoni wa Kiislamu Mtanzania ambaye elimu yake haikumjengea kiburi wala majivuno wala kutaka ukubwa.
INNAA LILLAAHI WAINNAA ILAYHI RAAJIUUN.
Sheikh Khamis Mataka ni Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Bakwata na Katibu Mkuu wa Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania.
Simu: 0713603050/0754603050