DPP amkatia rufaa Dk Slaa Mahakama ya Rufani

Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania (DPP) amewasilisha kusudio la kukata rufaa kupinga uamuzi uliyotolewa jana na Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam dhidi ya Mwanasiasa Mkongwe nchini Tanzania, Dk Wilbrod Slaa.

Uamuzi wa Mahakama Kuu jana, ulielekeza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kushughulikia suala la dhamana ya mwanasiasa huyo na kutoa uamuzi wa pingamizi la uhalali wa kesi ya jinai inayomkabili mahakamani hapo kwa haraka.

DPP amewasilisha notisi ya kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo, jana Januari 30, 2025 katika Mahakama ya Rufaa

Dk Slaa anakabiliwa na shtaka moja la kusambaza taarifa za uongo katika mitandao ya kijamii ya X, zamani ikijulikana kama Twitter.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Job Mrema ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo, Ijumaa Januari 31, 2025.

“Mheshimiwa hakimu, kwa mujibu wa kumbukumbu za mahakama, kesi hii ilipangwa kusikilizwa Februari 6, 2025 katika Mahakama hii lakini leo ni Januari 31, 2025 tumeitikia wito kwa sababu na sisi tumeitwa na mahakama yako kwa ajili ya kusikiliza maelekezo yako, hivyo tupo tayari kusikiliza” alidai Wakili Mrema.

Wakili Mrema ametoa taarifa hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki, baada ya Serikali kuitikia wito wa Mahakama uliowataka mawakili wa pande zote mbili yaani upande wa mashtaka na ule wa utetezi kufika katika katika Mahakama ya Kisutu kwa ajili ya kusikiliza maelekezo.

Alidai kutokana na kuwasilisha notisi hiyo, wanaomba mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu isitoe uamuzi wowote katika kesi ya msingi, mpaka hapo rufaa iliyowasilishwa Mahakama ya Rufani itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.

Mrema baada ya kuwasilisha maelezo hayo, yalipingwa vikali na mawakili nane wa utetezi wanaomtetea Dk Slaa wakiongozwa na Hekima Mwasipu akishirikiana na Peter Madeleka.

Jopo la mawakili wanane wanaomtetea Mwanasiasa mkongwe nchini, Dk Wilbrod Slaa, wakijadiliana jambo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Picha na Hadija Jumanne

Wakili Mwasipu alidai kuwa wameitwa Mahakama hapo kwa ajili ya kusikiliza uamuzi wa pingamizi la dhamana na wapo tayari kusikiliza.

Pia walihoji sababu za mshtakiwa kutokuletwa Mahakamani hapo, hoja ambayo ilijibiwa na upande wa mashtaka kuwa mahabusu wote hawakuletwa kutokana na changamoto ya usafiri wa gari la Magereza.

Kutokana na hali hiyo, hakimu Beda ameahirisha kwa muda wa masaa mawili kesi hiyo, ili aweze kupitia baadhi ya sheria kabla ya kuja kutoa uamuzi wa kuendelea na kesi au kutokuendelea.

Kesi hiyo itaendelea baada ya masaa 2.

Jana Januari 30, 2025 Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, iliielekeza Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Dar es Salaam kushughulikia suala la dhamana ya mwanasiasa maarufu nchini, Dk Wilbroad Slaa, na kutoa uamuzi wa pingamizi la uhalali wa kesi ya jinai inayomkabili mahakamani hapo kwa haraka.

Mbali na maelekezo hayo kwa mahakama ya Kisutu, pia kupitia sakata la dhamana ya mwanasiasa huyo, Mahakama Kuu ilitoa maelekezo maalumu kwa mahakama zote za chini namna ya kushughulikia suala dhamana za washtakiwa wa kesi za jinai.

Katika maelekezo hayo, Mahakama Kuu imezitaka mahakama hizo za chini yake kuweka kipaumbele cha kwanza kabisa kushughulikia dhamana kuliko masuala yoyote yanayohusiana na kesi hizo, huku ikisisitiza kuwa duala la dhamana linapaswa lishughulikiwe siku kwanza kabisa mshtakiwa anaposomewa mashtaka.

Dk Slaa alifungua mashauri hayo kutokana na mwenendo wa kesi ya jinai inayomkabili katika Mahakama ya Kisutu.

Katika mashauri hayo, mbunge huyo  mstaafu wa jimbo la Karatu alikuwa akiiomba mahakama hiyo iitishe na kupitia mwenendo wa shauri dogo lililofunguliwa na Jamhuri kupinga dhamana yake na wa kesi ya msingi, kujiridhisha na usahihi na uhalali wake.

Mashauri hayo yote yalisikilizwa na Jaji Kirekiano moja Alhamisi na lingine Ijumaa juma lililopita.

Endelea kufuatili mitando yetu

Related Posts