Wakati dunia ikielekea kuadhimisha Siku ya Wakimbizi Duniani Juni 20, mwaka huu, nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), maelfu ya wakimbizi nchini humo walikuwa wamekimbia makazi yao kutokana na mapigano yanayoendelea.
Kwa mujibu wa ‘Voice of America’, kambi ya Minova ina wakimbizi zaidi ya 3,000 wanaohifadhiwa ambao wanaishi maisha magumu bila kupata misaada.
Wakuu wa mataifa ya Afrika Mashariki walikubaliana kupeleka jeshi la kikanda nchini DRC katika jitihada za kujaribu kumaliza vita mashariki mwa nchi hiyo.
Viongozi hao walikubaliana kutuma kikosi cha kikanda kujaribu kumaliza mapigano mashariki mwa DRC na kutoa wito wa kusitishwa mara moja kwa mapigano.
Hatua hiyo ilitangazwa na ofisi ya Rais wa Kenya baada ya nchi wanachama saba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kufanya mazungumzo mjini Nairobi kuhusu kushamiri kwa ghasia katika eneo hilo lenye hali tete.
Lakini kikosi hicho kinakabiliwa na vikwazo huku Serikali za DRC na Rwanda zikirushiana maneno makali huku DRC ikidai kuwa Rwanda inawafadhili waasi wa M23. Rwanda imekanusha madai hayo.
Ijumaa iliyopita msemaji wa serikali ya DRC, Patrick Muyaya, alisema katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kwamba DRC haitakubali wanajeshi wa Rwanda katika vikosi vya pamoja kutumwa katika majimbo yake yenye matatizo.
Rais Paul Kagame wa Rwanda na Rais Felix Tshisekedi wa DRC walihudhuria mazungumzo hayo. Wengine waliohudhuria ni wakuu wa mataifa ya Burundi, Sudan Kusini na Uganda, pamoja na Tanzania iliyowakilishwa na balozi wake nchini Kenya, Dk John Simbachawene.
Ukosefu wa usalama katika eneo hilo unazidisha mvutano kati ya DRC na Rwanda. DRC inamtuhumu jirani yake Rwanda kwa kuunga mkono kundi la waasi la M23, madai ambayo Rwanda imeyakanusha.
M23 imepigana kwa miaka mingi kudhibiti migodi yenye utajiri mkubwa wa dhahabu na platinamu inayopatikana mashariki mwa DRC, ambapo vikundi vingine vya waasi kutoka Rwanda na Uganda pia vimejihusisha na mzozo huo.
Mvutano uliongezeka hivi majuzi wakati askari wa Jeshi la DRC aliuawa ndani ya Rwanda, baada ya kufyatulia risasi vikosi vya usalama kwenye kituo cha mpakani.
Taarifa ya ofisi ya Rais Tshisekedi imesema jeshi hilo linatakiwa kuanza operesheni zake katika kipindi cha wiki zijazo, na lisijumuishe askari yeyote kutoka jeshi la Rwanda.
Mwishoni mwa Mei mwaka huu Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Dk Vincent Biruta, aliulaumu Mpango wa Umoja wa Mataifa nchini DRC (Monusco) kwa kufumbia macho kile walichosema ni uchokozi wa DRC
Akizungumza na waandishi habari mjini Kigali, Waziri Dk Biruta alisema Jeshi la DRC lilirusha mabomu nchini Rwanda Mei 19 na 23, lakini DRC haijaomba msamaha.
Sehemu kubwa ya mzozo nchini DRC unasababishwa na kundi la waasi la M23 linalopambana na wanajeshi wa serikali (FARDC). Kundi hilo linasema kwamba halitachoka kudai haki ya raia wa DRC na kutaka makubaliano ya mkataba yaliyofanyika Nairobi, Kenya kutekelezwa.
Desemba 12, 2013 DRC na M23 walitia saini jijini Nairobi uliokusudiwa kuleta maridhiano, uthabiti na maendeleo mashariki mwa nchi hiyo.
Msemaji wa kundi hilo Meja Willy Ngoma, amemweleza mwandishi wa idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika (VOA), Kennes Bwire, kwa njia ya simu kwamba Serikali ya Rais Tshisekedi imekataa kutekeleza mambo waliyokubaliana alipoingia madarakani na badala yake kutuma wanajeshi wake kuwashambulia.
Meja Ngoma anadai kwamba mapigano ya hivi karibuni yanatokana na jeshi la DRC kuanza kile alichokitaja kama ‘uchokozi’ badala ya kutimiza ahadi.
“Sisi tunajibu mapigo peke yake. Ni hao wamekuja kushambulia ngome zetu. Sisi tunajibu mapigo yao na kuwafukuza mbali kabisa,” anasema Meja Ngoma.
Kundi hilo lilianza vita dhidi ya Serikali ya Congo Aprili 2012, likishutumu Serikali ya Joseph Kabila kwa kuwatenga watu kutoka jamii ya Watutsi na kukataa kuheshimu mikataba ya amani iliyokuwa imefikiwa awali.
Mkataba wa Nairobi ulifikiwa baada ya kundi hilo kupigwa na wanajeshi wa Serikali ya DRC wakisaidiwa na wanajeshi wa Umoja wa Mataifa.
M23 ni kundi lililoundwa Aprili 4, 2012 baada ya kuishutumu serikali kushindwa kuheshimu mkataba wa amani uliokuwa umesainiwa Machi 23, 2009, na hivyo kuliita kundi lake M23 kama kifupi cha Machi 23.
“Tulikubali kusaini mkataba wa Nairobi. Tulisaini tena mkataba wa Kinshasa na Rais Felix Tshisekedi alipoingia madarakani baada ya mazungumzo ya miezi 14 na tukakubaliana kuhusu mambo mengi sana. Tunasubiri watekeleze mambo ambayo tulizungumza. Badala yake, wamekuja kushambulia ngome yetu. Sisi tunajibu mapigo yao,” amesema Meja Ngoma.
Kulingana na Meja Ngoma, wanataka Serikali ya DRC ifanye mazungumzo ya kitaifa kuhusu amani, waasi hao waajiriwe na kuruhusiwa kuhudumu katika jeshi la serikali (FARDC), wanasiasa wa kundi hilo washirikishwe kwenye serikali, Jeshi la Serikali lipambane na kushinda nguvu kabisa makundi mengine ya waasi kama Allied Democratic Movement (ADF).
“Tulimwambia Tshisekedi kwamba tupo tayari kufanya kazi katika Jeshi la DRC na kama wamekataa, tupo tayari kurudi vijijini kwa mapigano na kundi la ADF kwa sababu tunaona wanaendelea kuua ndugu zetu,” anaeleza Ngoma na kuongeza kwamba “Hatupendi kupigana na Serikali ya Congo. Sisi tunataka amani, ndio maana tulisitisha mapigano ili tutafute na tujenge amani ndani ya Congo.”
Makundi mengine ya waasi kama Allied Democratic Forces, Mai-Mai na Codeco yamekuwa yakishambulia vijiji na kuuwa raia mashariki mwa DRC.
Mapigano kati ya M23 na jeshi la DRC yalisababisha kuangushwa kwa ndege ya kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa na kuuawa kwa wanajeshi wake wanane. Hakuna maelezo zaidi yametolewa hadi sasa.
Pande zote katika vita hivyo zilishutumiana kwa kuangusha ndege hiyo na hakuna habari kamili imetolewa kufikia sasa.
Kulingana na Meja Willy Ngoma, wao M23 wanataka amani ya raia wote wa DRC bila ubaguzi wa aina yoyote na kwamba kila raia wa Congo anastahili kuwa huru ndani ya nchi yake. “Hatutaki baadhi ya raia wa Congo wawe wa muhimu kuliko wengine. Tunataka makundi yote ya waasi kama ADF yaondoke Congo,” anasema Meja Ngoma.
Nini chimbuko la M23? Lilianzishwa lini na kwanini? Je, ni wapiganaji wa DRC? Ni waasi kutoka Uganda na Rwanda walioko DRC? Kwanini Jeshi la DRC linaishutumu Rwanda na Uganda kuwaunga mkono waasi wa kundi hilo katika mapigano yaliyozuka upya wilayani Rutshuru na kusabisha maelfu ya raia kukimbilia nchi jirani ya Uganda?