Gomez wa Fountain Gate atengewa mamilioni Wydad Casabalanca

WAKATI ikiwa inaendelea kufukuzia saini ya nyota wawili wa Yanga, Clement Mzize na Stephane Aziz KI, klabu ya Wydad Casablanca ya Morocco imekamilisha dili la kumnasa mshambuliaji wa Fountain Gate, Seleman Mwalim ‘Gomez’ kwa mkataba wa miaka minne wenye thamani ya Sh891 milioni.

Gomez anaichezea Fountain Gate kwa mkopo kutoka Singida Black Stars na inaelezwa mbali na kitita hicho cha kusaini mkataba huo, pia mchezaji huyo anayemiliki mabao sita Ligi Kuu Bara msimu huu, atapokea mshahara wa Sh6 milioni kwa mwezi mbali na bonasi za kupata fedha kila atakapofunga mabao akiwa na kikosi hicho kinachonolewa na kocha Rhulani Mokoena.

Wydad imetuma maombi Yanga ikiwahitaji mastaa wao wawili Mzize na Aziz Ki kabla ya dirisha la usajili Morocco linalofungwa leo, lakini baada ya kuona kuna ugumu kuwapata kwa haraka wakaamua kumnyakua Gomez aliyekuwa Mfungaji Bora wa Ligi Kuu ya Zanzibar (ZPL) akiwa na KVZ.

Jioni klabu ya Singida imetoa taarifa kwa umma juu ya kukubaliana na Wydad kumsajili moja kwa moja Gomez, lakini mapema Mwanaspoti limezinasa habari za ndani kuwa nyota huyo ameshaanza safari kutoka Manyara kuja Dar es Salaam ili kushughulikia VISA ya safari ya kwenda Morocco.

“Ni kweli Wydad imefanya mazungumzo na klabu yetu kwa ajili ya mchezaji huyo na mazungumzo yamekwenda vizuri muda wowote kuanzia sasa mambo yakikamilika atatangazwa kuwa mchezaji halali wa timu hiyo kwa mkataba wa miaka minne,” alisema mtoa taarifa huyo wa Mwanaspoti na kuongeza;

“Kwa asilimia 70 hadi 80 limekamilika kilichobaki ni mchakato mdogo wa mchezaji na klabu husika kumalizana kwa sababu kwa upande wa timu mazungumzo na makubaliano yamekwenda vizuri.”

Hata hivyo, muda mfupi uliopita, Singida ilitoa taarifa rasmi wameafikiana na Wydad kuwauzia Seleman Mwalimu kwa mkataba wa moja kwa moja kwa dau walilokubaliana.

“Sehemu ya makubaliano hayo ni klabu yetu kupata asilimia 10 ya mauzo ya baadae iwapo Wydad itamuuza klabu nyingine,” ilieleza taarifa hiyo na kuongeza;

“Kipekee tunapenda kuishukuru Fountain Gate kwa malezi na kukubaliana nasi kumpa fursa kijana kwenda kupata changamoto mpya. Uongozi wa Singida BS unamtakia Seleman Mwalimu kila la kheri na mafanikio katika safari yake ya soka.”

Mara ya mwisho kwa mchezaji huyo kufunga bao Ligi Kuu Bara ilikuwa kwenye ushindi wa kikosi hicho wa mabao 3-1 dhidi ya KMC, Oktoba 21, mwaka jana na sasa akifikisha siku 101 ambazo ni sawa na miezi mitatu na siku tisa bila ya kuona nyavu za wapinzani. Fountain Gate ipo katika nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi.

Related Posts