Gavana wa Benki Kuu, Emmanuel Tutuba akizungumza na wadau wa fedha na Wakala wa Uwezeshaji wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA) kuhusiana na masuala ya Mikopo ya ZEEA kidijitali.
Makamu wa Rais na Meneja Mikakati Kampuni ya Airpay Tanzania, Mihayo Wilmore akizungumza jijini Dar es Salaam leo Januari 31, 2025 walipo kutana na Gavana wa Benki Kuu juu ya masuala ya fedha kidijitali.
Mkurugenzi Mtendaji Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA), Juma Burhan Mohamed akiwa kwenye mkutano na Gavana wa Benki Kuu jijini Dar es Salaam leo Januari 31,2025
Picha ya pamoja
KATIKA kurahisisha urejeshaji wa mikopo Gavana wa Benki kuu, Emmanuel Tutuba ametoa wito kwa wafanyabiashara wote na wanachi waliopata fursa ya kupata mikopo ya serikali watumie fedha vizuri na wasidhani kuwa ni zawadi kutoka serikalini.
Ameyasema hayo leo Januari 31,2025 jijini Dar es Salaam leo, wakati akizungumza na wadau kutoka benki, huduma za kifedha kwa njia ya simu na wadau wa huduma za kifedha Kidijitali.
Amesema fedha hizo ni za uwezeshaji wananchi kiuchumi ambapo lengo lake ni kuwajengea fursa ya kuwa na shughuli za kiuchumi zinazotengeneza faida.
“Na sisi kama wasimamizi wa sekta tunaendelea kuweka mifumo vizuri ya kuhakikisha serikali inawawezesha wananchi na wananchi wanafanya biashara zao wanapata faida na wanarejesha na kuendelea na biashara zao.” Amesema Tutuba
Ameeleza kuwa viongozi wa serikali wamekuwa wakisisitiza kila mwenye vigezo vyote akope mkopo na arejeshe lakini kila anayepata fursa ajue kwamba amebahatika kwa sababu serikali imeweka mifumo ya kuweza kurejesha fedha hizo kwani angeweza kupata kwa gharama kubwa.
“Utaratibu wa kurejesha ni mzuri kwa mtu ambaye atakuwa anarejesha ili iweze kujenga matumaini kwa wananchi wengine kwa kurejesha kwa wakati.” Amesema
Akielezea namna mikopo ambavyo imekuwa hairejeshwi, Tutuba amesema kiwango cha mikopo chechefu kimekua kwa wastani wa asilimia 28 ya mikopo ambayo hairejeshwi bila kuwa na sababu za msingi.
Kwa upande wa Makamu wa Rais na Meneja Mikakati Kampuni ya Airpay Tanzania, Mihayo Wilmore amesema kuwa kwa upande wa Zanzibar tayari kuna mifumo mbalimbali kwa kila benki na mitandao ya simu wanachotaka ni kuunganisha mifumo hiyo pamoja ili iweze kumrahisishia wananchi na wananchi kulipa kwa mikopo ya ZEEA.
“Sisi kama Airpay tumejenga mifumo wa ‘Loan Management system’ ambayo ni kama chungu cha mifumo yote ya ZEEA itakayokuwa inawasaidia wananchi kulipa marejesho yake kwa kwenda kwa wakala yeyote kulipa .” Amesema Wilmore
Akielezea Changamoto wanayoipitia amesema kuwa kunabaadhi ya wananchi wanakuwa hawataki tuu kutoa marejesho na kufanya mkopo kuwa Chechefu.
Kwa Upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Uwezeshaji wananchi kiuchumi Zanzibar (ZEEA), Juma Barhan Mohamed amesema kuwa kikao hicho kimewasaidi kuwa na mpango wa pamoja na wadau wote wa fedha kidijitali.
“Tunaamini baada ya kikao hiki cha leo wale ambao hawafanyi marejesho watarejesha kiurahisi zaidi bila ya kuwa na kikwazo cha kusafiri kutoka sehemu moja ama nyingine kwaajili ya kurudisha marejesho kwa wakati.” Amesema
Ameeleza kuwa Wananchi waendane na kauli mbiu ya kopa kwa maendeleo ya yako binafsi na maendeleo ya taifa.
Amesema kuwa upande wa Zanzibar wanaendeleza huduma za kifedha kidijitali ili kufikia 2030 uchumi wa Zanzibar uwe wa kidijitali.
“Sisi kama wawezeshaji wa wananchi kiuchumi tunajukumu la kuhakikisha wanaubadilisha uchumi wa kawaida na kwenda uchumi wa kidijitali.” Amesema Mohamed
Amesema kuwa kumekuwa na nadhria mbaya kuhusiana na pesa ya serikali kwamba watu wasirudishe licha ya kufanya kazi vizuri na mabenki sasa pesa zinarudishwa baada ya kufanikiwa kufanya kazi na benki na tafiti mbalimbali, kwamba wasiofanya marejesho kwa wakati sio wafanyabiashara, biashara wanazo ila wamekuwa na mtazamo wa fedha ya serikali, hairudishwi rejesho.
Amesema kuwa wanaokopa watakuwa na fursa ya kurejesha kidijitali akiwa mahali popote huku nauli na usumbufu mwingine ukawa ni sehemu ya marejesho ya mkopo.
Hata hivyo Mohamed ameishukuru kampuni ya Airtel na Benki ya TCB kuwa kampuni za kwanza za kifedha kuweza kukamilisha muunganisho wa mifumo ya malipo kidijitali na ZEEA pamoja na Airpay.
“Hichi kilichofanywa na kampuni hizi mbili kimesaidia na kimeonesha jinsi gani wanaunga mkono serikali katika kuhakikisha tunakuwa na uchumi jumuishi visiwani Zanzibar,”