Dar es Salaam. Wataalamu wa afya wamesema mabadiliko mbalimbali yanayotokea katika mwili wa binadamu huwa ishara ya changamoto za kiafya, hivyo hayapaswi kupuuzwa.
Meneja mradi wa afya ya mama na mtoto na mtaalamu wa lishe kutoka Shirika la World Vision, Dk Daud Gambo anasema baadhi ya watu wamekuwa na tabia ya kupuuzia baadhi ya dalili au mabadiliko yanayojitokeza katika miili yao pasipo kujua chanzo chake.
Gambo anasema tabia hiyo ni hatari, kwani matatizo makubwa yote yanayojitokeza huanza na dalili ndogo ndogo ambazo mtu anaweza kupuuzia.
Kauli ya Dk Gambo inaendana na kile ambacho kinasimuliwa na Nyasatu Emmanuel (si jina halisi) namna kupuuza dalili kulivyomfanya kuchelewa kugundua kuwa ana maambukizi ya virusi vya Ukimwi, hali iliyosababisha afya yake kudhoofu.
Nyasatu anaeleza kuwa miezi kadhaa kabla ya kugundulika kuwa na maambukizi alipata mabadiliko mbalimbali ya mwili, ikiwemo homa za mara kwa mara, kupungua uzito sana pamoja na kupungua kwa hamu ya kula.
“Nilidhani ni mabadiliko ya kawaida labda kwa sababu ya uchovu wa kazi, hivyo niliyatuliza kwa dawa za maumivu, baadaye nilizidi kuumwa na ndugu zangu kuhisi pengine nitakuwa nimerogwa.
“Nilipelekwa mara kadhaa kwa waganga kupata tiba bila mafanikio, hadi kukata shauri na kuamua kwenda hospitali kwa ajili ya uchunguzi zaidi ambao niligundulika kuwa na maambukizi na kwa wakati huo afya yangu ilikuwa dhaifu sana,” anaeleza Nyasatu.
Anaongeza kuwa baada ya kuanza kutumia dawa za ARV na kufuata ushauri wa daktari, sasa afya yake imeimarika na anaendelea na shughuli zake.
Miongoni mwa dalili zilizotajwa kwamba hazipaswi kupuuzwa ni pamoja na maumivu ya kichwa ya mara kwa mara, kikohozi au homa.
Gambo anasema hali hiyo inapojitokeza mara kwa mara, huweza kuwa ishara ya mabadiliko au changamoto fulani katika mwili, hivyo ni vyema kumuona daktari kwa ajili ya vipimo na uchunguzi zaidi.
Kuongezeka au kupungua kwa uzito ghafla
Gambo anasema mtu anapoongezeka au kupungua sana uzito ghafla, huweza kuashiria changamoto fulani kiafya.
Anasema hali hiyo huweza kusababishwa na kupoteza au kuongezeka zaidi kwa hamu ya kula ambayo kwa wakati mwingine huashiria maambukizi ya magonjwa, akitolea mfano ugonjwa wa kisukari unaoweza kumsababishia mtu kupungua uzito ghafla.
“Usijisikie furaha sana ikiwa umepoteza uzito bila kutarajia kwa sababu inaweza kuwa ishara ya tatizo la afya. Ikiwa umepungua au kunenepa ghafla ni vyema kumuona daktari na uende kuchunguzwa afya yako,” anaeleza.
Kupoteza hamu ya kula kwa muda mrefu, inaelezwa kuwa moja ya ishara kuwa afya ya mwili haipo sawa.
Dk Gambo anabainisha kuwa kuongezeka au kupungua kwa hamu ya kula bila sababu kunaweza kuwa sababu ya shida ya kiafya ambayo inahitaji kutambuliwa mara moja, kwani ina sababu mbalimbali, ikiwemo matatizo ya kisaikolojia kama kukabiliwa na msongo wa mawazo.
“Hivyo mtu anapopitia katika hali hiyo kwa muda fulani, ni vyema kufika kwa daktari na kufanyiwa uchunguzi ili kubaini ni nini kilichosababisha hali hiyo na kupatiwa matibabu,” anaeleza.
Mabadiliko katika haja kubwa
Dk Gambo anaeleza kuwa mtu anapopata haja kubwa vizuri bila changamoto yoyote ni moja ya kiashiria kuwa afya yake iko sawa, hasa katika upande wa mmeng’enyo wa chakula.
Hivyo mtu anapopitia mabadiliko mbalimbali kama vile maumivu makali wakati wa kutoa haja kubwa, kutoa haja kubwa inayoambatana na damu, kuharisha au kutopata haja kubwa kwa muda mrefu huashiria uwepo wa tatizo katika mmeng’enyo wa chakula.
Anaeleza kuwa mabadiliko hayo vilevile huweza kuashiria uwepo wa changamoto mbalimbali katika tumbo, ikiwemo vidonda vya tumbo pamoja na saratani ya utumbo.
Daktari wa ngozi kutoka hospitali ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Tumpale Luhanga anasisitiza kuwa ni muhimu kuwa makini na mabadiliko yanayojitokeza katika ngozi, kwani hueleza changamoto fulani katika afya ya binadamu.
“Ukipata dalili kama vile ngozi kuwasha, mabaka kwenye ngozi, wekundu kwenye ngozi au kuwasha ngozi, basi nenda ukachunguze afya yako badala ya kuhangaika na sabuni na vipodozi vinavyoweza kusababisha matatizo zaidi, kwani changamoto nyingi za ngozi huanzia ndani, na nje huwa kama matokeo tu,” anaeleza Dk Luhanga.
Kwa upande wake daktari wa upasuaji kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dk Mugisha Nkoronko anaongeza kuwa ni muhimu kumuona daktari pale mtu anapopata uvimbe usio wa kawaida katika sehemu mbalimbali za mwili.
Pia anashauri ni vyema mtu anapoona kipele, uvimbe au kitu chochote kisicho cha kawaida katika mwili wake, kufika hospitali ili kufanyiwa uchunguzi.
Anasema hiyo itasaidia kugundulika kwa tatizo mapema likiwa katika hatua za awali na kupatiwa matibabu ili kuepuka madhara makubwa yanayoweza kujitokeza.