Dar es Salaam. Mafuta ni muhimu katika mwili kwa kuwa yanasaidia ufyonzwaji wa vitamini A, D, E na K. Kiafya binadamu anatakiwa kutumia kiasi cha kidole gumba chake kama kipimo cha mafuta alayo kwa siku.
Mafuta, hasa yatokanayo na samaki, yana virutubishi muhimu (asidi za omega 3 na 6) ambavyo ni bora kwa ukuaji wa ubongo na akili ya mtoto wakati akiwa tumboni kwa mama na miaka miwili baada ya kuzaliwa.
Hata hivyo, mafuta yakizidi huleta athari hasi mwilini. Licha ya wataalamu mbalimbali kuwataka watu kutokula vyakula vyenye mafuta, bado yana umuhimu katika mwili wa binadamu.
Kutokana na hilo, unachotakiwa ni kula kwa kipimo na siyo kupitiliza kwa kuwa itaweza kukuletea shida kwa kupata magonjwa ya moyo, shinikizo la damu na unene uliopitiliza.
Kazi za mafuta mwilini ni pamoja na kusaidia katika utengenezwaji wa nishati mwilini, kuupa mwili joto, husaidia katika kulinda sehemu za ndani za mwili na kusaidia katika utoaji wa taarifa mbalimbali ndani ya mwili.
Kazi nyingine ni kusaidia protini kufanya kazi zake vyema, kusaidia katika ukuaji wa kiumbe, kuboresha mfumo wa kinga mwilini na kusaidia katika mfumo wa uzalianaji.
Vyakula ambavyo mtu anaweza kupata mafuta ni pamoja na siagi, maziwa, mayai, karanga na jamii za karanga kama korosho, mbegu za chia, samaki, choklet, nazi, nyama, maharagwe ya soya na alizeti.
Aidha, upungufu wa mafuta mwilini, unaweza kukusababishia matatizo mbalimbali, ikiwemo kukauka kwa ngozi na ukurutu, kupata maambukizi ya mara kwa mara, kupona kwa vidonda kuliko hafifu na kuchelewa kukua kwa watoto.
Pamoja na umuhimu huo, bado kuna watu wananunua mafuta yasiyo katika mazingira mazuri au yasiyo na ubora, kisingizio ikiwa ni hali duni za maisha walizonazo.
“Binafsi siwezi kununua mafuta lita nzima, huwa nikienda kupima ya Sh200, Sh300 hadi Sh500, hivyo ukiniambia ninunue mafuta yaliyofungwa kwenye chupa huo ni uwongo,” anasema Husna Kirungu, mkazi wa Mbagala.
Mwananchi ilifanya mahojiano na wataalamu mbalimbali kuhusu umuhimu wa kiafya katika kutumia mafuta yaliyo bora na nini athari zake endapo mtu hatafanya hivyo na namna ya kuziepuka athari hizo.
Mhadhiri mwandamizi idara ya usindikaji kemikali na viwanda, Profesa Samwel Manyele, anasema mafuta hadi kumfikia mlaji yana michakato mbalimbali katika utengenezaji wake ambapo moja ya hatua ikikosewa inaweza kumletea madhara mtumiaji wa mwisho ambaye ni mlaji.
Profesa Manyele, ambaye pia amewahi kuwa Mkemia Mkuu wa Serikali, anabainisha kuwa kuna njia mbili za ukamuaji mafuta ambapo upo ule unaotumia mitambo, ambao unahusisha zaidi mafuta yatokanayo na mimea ikiwemo mawese, alizeti, pamba, karanga, mzaituni na mbegu nyingine.
Aina, nyingine ni ile ya kutumia kemikali. Katika njia hii kemikali ya solvent kama hexane hutumika kuchukua mafuta kutoka kwenye malighafi na baadaye mafuta hayo hutenganishwa na solvent kwa kutumia joto ili kuondoa masalia ya kemikali hiyo.
“Katika njia zote hizo mbili za kutengeneza mafuta, huwa kuna hatua kumi zinafuatwa ili kupata mafuta, ikiwemo kukusanya malighafi, kusafisha na kuandaa malighafi, kukausha, kusaga, kakamua mafuta na kuchuja.
“Hatua nyingine ni kuchuja na kusafisha kuboresha mafuta, uchujaji wa mwisho na ufungaji, ukaguzi wa ubora na mwisho ni usambazaji,” anasema.
Mtaalamu huyo anaeleza kuwa utengenezaji wa mafuta ya kula kiwandani ni mchakato mrefu na kote huku na unahitaji uangalizi mkubwa ili kuhakikisha ubora na usalama wa mafuta.
“Ukosefu wa hatua yoyote ya uchakataji au uzembe, unaweza kusababisha mafuta yasiyofaa matumizi yanayoweza kuhatarisha afya ya walaji,” anasema Profesa huyo.
Madhara mafuta yasiyo bora
Profesa Manyele anasema ulaji wa mafuta yasiyo bora unaweza kumsababishia mlaji matatizo mbalimbali ya kiafya, ikiwemo kuongezeka kwa hatari ya magonjwa ya moyo na mishipa.
Tatizo jingine ni shida za utumbo ambapo mafuta yasiyo safi au yaliyochakaa yanaweza kuwa na sumu na vitu vinavyodhuru vinavyoweza kusababisha kichefuchefu, maumivu ya tumbo na matatizo mengine ya mmeng’enyo wa chakula.
Aidha, tatizo la kuongezeka kwa sumu mwilini, mtaalamu huyo anasema nalo linaweza kujitokeza ambapo mafuta yaliyoharibika (rancid fats) hutoa kemikali zinazojulikana kama aldehydes ambazo ni sumu zinazoweza kusababisha athari mbaya mwilini, ikiwa ni pamoja na kuharibu figo.
Profesa Manyele anasema inatokea zaidi katika mafuta yanayopashwa moto mara kwa mara, haswa kwa njia ya kukaanga ambayo huzalisha misombo ya kansajeni inayoweza kuongeza hatari ya saratani, hasa ya matiti, tumbo na ini.
Matatizo mengine ni pamoja na kuongezeka uzito kupita kiasi, kupata matatizo ya ngozi kama vile chunusi au madoa kwa sababu ya mkusanyiko wa sumu mwilini, kukosekana kwa virutubisho muhimu kama vile vitamin E na aside ni muhimu kwa afya ya ngozi, macho na mfumo wa kinga.
Profesa Manyele anasema, mlaji anapaswa kutumia mafuta ya kula yaliyothibitishwa na mamlaka za afya na kuepuka kutumia mafuta yaliyopashwa moto mara nyingi.
Njia nyingine ni kuhifadhi sehemu kavu na zenye baridi ili yasiharibike, kununua mafuta yaliyofungashwa vizuri na kuangalia tarehe ya mwisho wa matumizi.
Kwa upande wa mzalishaji, anapaswa kufuata viwango vya kimataifa vya usalama wa chakula, kutumia teknolojia za kisasa na kuhakikisha uzingatiaji wa taratibu za uzalishaji bora.