Dar es Salam. Baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania (DPP) kuwasilisha nia ya kukata rufaa Mahakama ya Rufaa kupinga uamuzi wa Mahakama kuhusu dhamana ya Dk Wilbrod Slaa, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imefungwa mikono kuendelea na suala hilo.
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imesema kwa sasa imefungwa mikono kuendelea na kesi hiyo ya msingi hadi itakaposikilizwa rufaa hiyo na kutolewa uamuzi.
Dk Slaa anakabiliwa na shtaka moja la kusambaza taarifa za uongo katika mtandao wa kijamii wa X.
Uamuzi huo umetolewa leo, Januari 31, 2025 na Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki baada ya kupitia na kujiridhisha kwenye mtandao wa Mahakama kuwa upande wa mashtaka umefungua maombi mawili ya kukata rufaa Mahakama ya Rufaa kupinga uamuzi ulitolewa na Mahakama Kuu.
“Niliahirisha kesi hii kwa muda ili kwenda kujiridhisha iwapo nyaraka za kukata rufaa zilizowasilishwa na upande wa mashtaka ni halali na kama zimesajiliwa katika mfumo wa mahakama na nimeangalia nyaraka hizo zimesajiliwa kwa namba 202501317506828 na 202501319648936” alisema hakimu Beda na kuongeza:
“Kwa sababu hiyo, nachelea kusema kuwa mikono yangu imefungwa kutoa uamuzi wowote kuhusu kesi hii hadi hapo rufaa hii inakavyosikilizwa na kutolewa uamuzi na Mahakama ya Rufani,” amesema.
Baada ya kueleza hayo, hakimu Beda amesema huo ndio uamuzi wake na upande wa utetezi una haki ya kukata rufaa, iwapo hawajaridhika na uamuzi alioutoa.
Jana Januari 30, 2025 Mahakama Kuu iliielekeza Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Dar es Salaam kushughulikia suala la dhamana ya mwanasiasa huyo na kutoa uamuzi wa pingamizi la uhalali wa kesi ya jinai inayomkabili mahakamani hapo kwa haraka.
Mbali na maelekezo hayo kwa mahakama ya Kisutu, pia kupitia sakata la dhamana ya mwanasiasa huyo, Mahakama Kuu ilitoa maelekezo maalumu kwa mahakama zote za chini namna ya kushughulikia suala dhamana za washtakiwa wa kesi za jinai.
Katika maelekezo hayo, imezitaka mahakama hizo za chini yake kuweka kipaumbele cha kwanza kabisa kushughulikia dhamana kuliko masuala yoyote yanayohusiana na kesi hizo, huku ikisisitiza kuwa duala la dhamana linapaswa lishughulikiwe siku ya kwanza kabisa mshtakiwa anaposomewa mashtaka, uamuzi ambao upanda wa jamhuri umeukatia rufaa.
Dk Slaa alikata rufaa mahakama kuu kupinga hatua ya mahakama ya Kisutu kumnyima dhamana, pia akitaka ipitie upya mwenendo wa kesi ya msingi kuona uhalali wa mashtaka dhidi yake.