Mastaa Pamba watuhumiwa kubeti Ligi Kuu

WAKATI kukiwa na mijadala kuhusu wachezaji wa ligi mbalimbali za soka nchini Tanzania kuhusika katika michezo ya kubashiri (betting) na kupanga matokeo, kuna jambo limeibuliwa Mkoani Mwanza na kuibua mijadala mingi miongoni mwa wadau.

Jambo hilo limehusishwa moja kwa moja na baadhi ya mastaa wa klabu kongwe na maarufu jijini Mwanza ya Pamba Jiji ambayo inashiriki Ligi Kuu Bara chini ya ufadhili wa Serikali ya Mkoa na mlezi wake akiwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda. 

Kauli hiyo ya kushtua ya Mtanda ambaye pia ni mshauri wa timu hiyo aliitoa jana jijini Mwanza wakati wa hafla ya chakula cha usiku na wachezaji, benchi la ufundi na menejimenti ya klabu hiyo kuelekea michezo ya mzunguko wa pili Ligi Kuu Bara.

Alisema tabia hiyo kwa sasa ni ugonjwa mkubwa katika soka la Tanzania, ambapo ili kuikomesha tayari wamewasilisha majina ya wachezaji wote wa kikosi chao kwenye Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kufuatilia nyendo zao.

“Hivi vitu vipo na vinatokea. Sasa wewe tunakulipa mshahara Sh3 milioni mpaka Sh4 milioni halafu unabashiri Pamba ipoteze, sasa nimepeleka namba zenu TCRA yeyote atakayebeti nitaona na ni rahisi kwangu,” alisema Mtanda.

“Kuna mchezaji mwenzenu nilimwambia mlipokwenda kucheza na Namungo alikuwa anashawishi wenzake muuze mechi na ukitaka ushahidi nitakupa nikamkanya aache. Nawaonya muache kwa sababu ushahidi ninao na sitaki mambo haya yaendelee.”

“Sitaki kutaja majina lakini nimeshaongea na baadhi yenu wengine wanatumia simu za wake zao kupokelea hiyo miamala, hivyo nawaonya hii ni timu ya taasisi ya serikali ambayo fedha nyingi zinatumika ambazo zingeenda kwenye miradi mingine,” alisema Mtanda.

P 01

Katika kukabiliana na tatizo hilo, alisema menejimenti imekubaliana kutafuta fedha za motisha na kuziweka kwenye akaunti ili ziwe tayari muda wote na wachezaji wapewe kianzio (advance) kabla ya mchezo.

“Tumekubaliana raundi hii ya lala salama kabla ya mechi CEO atachukua hicho kiasi cha bonasi na kumpa kiongozi wa msafara mechi ikiisha vijana wapewe huko huko na kama hawajashinda irudishwe kwenye akaunti ili tusilete maneno,” alisema Mtanda.

Alipotafutwa na Mwanaspoti kuzungumzia kauli ya mkuu wa mkoa huo, Kocha Mkuu wa Pamba, Fred Felix ‘Minziro’ alisema kuwa suala la kubeti upande wa wachezaji na makocha ni hatari kwa soka, kwani kufanya hivyo ni kupanga matokeo na kudidimiza baadhi ya timu.

“Wachezaji na makocha kucheza kamari ya kubashiri matokeo ni hatari na haina afya kwenye mchezo huo. Kwa wenzetu, nchi ya Tanzania wakifanya hivyo wanachukuliwa hatua ya kufungiwa,” alisema.

“Kuhusiana na kauli ya Mtanda kuwa wachezaji wa Pamba Jiji wanabashiri siwezi kuzungumzia kwa upana kwa sababu mimi sijafuatilia kama alivyofanya yeye kuchunguza na kubaini hayo mambo.”

lakini, Minziro alisema amefurahishwa na kauli hiyo ambayo ameipokea akiamini kuwa itaisaidia timu yake kufanya vizuri mzunguko unaotarajiwa kuanza mwanzoni mwa mwezi huu akiamini wachezaji wataipambania timu hiyo.

Ofisa Habari wa Bodi ya Ligi Tanzania, Karim Boimanda alisema kuna kanuni ambazo zimewekwa kuzuia wadau wa mpira wa miguu kujihusisha na masuala ya ubashiri wa matokeo na rushwa.

“Tunapokea taarifa kutoka kwa mdau yeyote halafu masuala ambayo hayahitaji uchunguzi yanapelekwa kwenye Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi, lakini kwa yale yanayohitaji uchunguzi yanapelekwa kwa Kamati ya Maadili au Nidhamu za TFF (Shirikisho la Soka) ambazo zenyewe ndio zitamuita mhusika au wahusika na kuwahoji kisha kuchukua hatua,” alisema  Boimanda.

P 02

Kanuni ya 40 (6); Ni marufuku kwa kocha, mchezaji, kiongozi au ofisa wa mchezo kushiriki michezo ya kubashiri (betting). Kocha, mchezaji, kiongozi au ofisa wa mchezo atakayekiuka, atafikishwa kwenye Kamati ya Nidhamu au Kamati ya Maadili ya TFF.

Kanuni 41(11);Mchezaji atakayebainika kupanga matokeo ya mchezo kwa namna yoyote ile atafungiwa maisha kucheza mpira ndani na nje ya nchi.

KANUNI ZA MAADILI ZA FIFA

Ibara ya 27; Kujihusisha na kamari au shughuli kama hizo inasema;

1. Watu waliofungwa na kanuni hii watakatazwa kushiriki ama moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja kamari, bahati nasibu au matukio kama hayo ama miamala inayohusiana na mechi za kandanda au mashindano na/au yoyote inayohusiana shughuli za mpira wa miguu.

2. Watu waliofungwa na kanuni hii hawatakuwa na fedha za moja kwa moja au zisizo za moja kwa moja au maslahi (kupitia au kwa kushirikiana na wahusika wengine) katika shughuli, kama vile kuweka dau, kamari, bahati nasibu au matukio kama hayo au miamala inayohusiana na mechi za soka na mashindano. Maslahi ni pamoja na kupata chochote kinachowezesha faida kwa watu waliofungwa na kanuni hii wenyewe na/au wanaohusiana vyama.

3. Isipokuwa kwamba mwenendo husika haujumuishi ukiukwaji mwingine wa kanuni hii, ukiukaji wa kifungu hiki utaidhinishwa na faini ya angalau Faranga ya Uswisi 100,000 (Sh280 milioni) na kupigwa marufuku kushiriki katika masuala yoyote ya soka kwa muda usiozidi miaka mitatu. Kiasi chochote kinachopokewa kitakuwa kimejumuishwa katika hesabu ya faini.

MECHI ZA PAMBA LIGI KUU BARA

Related Posts