Kuuma kwa misuli ya mwili ni mojawapo ya matatizo yanayoweza kuwakumba watu wenye ugonjwa wa kisukari. Hali hii mara nyingi inahusiana na athari za kisukari kwenye mishipa ya damu, neva na misuli yenyewe.
Kwa watu wenye kisukari, maumivu haya yanaweza kuwa ya mara kwa mara na kuathiri ubora wa maisha. Neuropathy ni tatizo linalosababishwa na uharibifu wa neva kutokana na viwango vya juu vya sukari mwilini kwa muda mrefu.
Neuropathy husababisha maumivu ya misuli, hasa katika miguu na mikono. Hii ni kwa sababu neva zinazodhibiti misuli hupoteza uwezo wa kufanya kazi ipasavyo, na kusababisha misuli kupata maumivu au udhaifu.
Kisukari, hasa aina ya pili, kinaweza kusababisha mishipa ya damu kuwa myembamba au kuziba, hali inayojulikana kama ugonjwa wa mishipa ya pembeni (Peripheral Artery Disease – PAD).
Mzunguko duni wa damu husababisha misuli kukosa oksijeni na virutubisho vya kutosha, jambo linalochangia maumivu na uchovu wa misuli. Wenye kisukari wana uwezekano wa kuwa na viwango vya chini vya magnesiamu mwilini, madini muhimu kwa utendaji mzuri wa misuli.
Upungufu wa magnesiamu unaweza kusababisha misuli kukaza, kuuma au kukakamaa.
Kupata maumivu makali au yenye kuchomachoma yanayoweza kuongezeka, hasa kama sukari ikiwa juu sana au chini.
Katika kuhakikisha mwenye kisukari hapati shida hii, kudhibiti sukari ni hatua muhimu ya kwanza. Viwango vya juu vya sukari kwa kawaida vinaweza kuzidisha uharibifu wa neva na kusababisha maumivu makali.
Hakikisha unafuata mpango wa lishe ulioandaliwa na mtaalamu wa afya, pamoja na kutumia dawa au insulini kama ulivyoelekezwa. Mazoezi ya wastani, kama kutembea, kuogelea au yoga, yanaweza kusaidia kuboresha mzunguko wa damu, kuimarisha misuli na kupunguza maumivu.
Hata hivyo, ni muhimu kushauriana na daktari kabla ya kuanza programu yoyote ya mazoezi. Hakikisha unakula vyakula vyenye magnesiamu kwa wingi kama vile mboga za majani, karanga na mbegu.
Pia, vyakula vyenye omega-3 kama samaki wa maji baridi vinaweza kusaidia kupunguza uvimbe wa misuli na vyakula vyenye madini kama magnesiamu na vitamini D ni muhimu kwa afya ya misuli. Ikiwa kuna upungufu, daktari anaweza kupendekeza virutubisho.
Kwa wadada wenye kisukari, viatu vinavyobana au virefu vinaweza kusababisha matatizo ya mzunguko wa damu na kuongeza shinikizo kwenye misuli ya miguu. Watu wenye kisukari wanapaswa kuvaa viatu maalumu vinavyosaidia afya ya miguu.