Mfumo wa Kidijitali wa Afya wa Digital Health Wallet Kuimarisha Huduma za Matibabu"

WIZARA ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kupitia Tume ya TEHAMA nchini kwa kushirikiana na Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi na kampuni ya watu wa Ulaya ya Gavstack wameunda mfumo wa afya wa kidijitali ‘Digital Health Wallet’, unaowezesha kutunza taarifa za matibabu za wananchi, ikiwa ni hatua ya utekelezaji wa mkakati wa uchumi wa kidijitali nchini.

Akizungumza leo Januari 31, 2025 Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Uendelezaji wa Mifumo Tehama Wizara ya Mawasialiano na Teknolojia ya Habari, Mohamed Mashaka amesema wameangalia namna gani wanaweza kutekeleza mkakati wa uchumi wa kidijtali kama ulivyozinduliwa rasmi na Rais Samia Suluhu Hassan mwaka jana na wameweza kuangalia katika sekta ya afya ili kuona namna watakavyoweza kusaidia.

Aidha amesema kuwa matumizi ya mfumo huo wa afya wa kidijitali utakwenda kusaidia mifumo ya hospitali za serikali na binafsi zinavyokwenda kusomana na kusaidia kutunza kumbukumbu za taarifa za wagonjwa.

“Mfumo huu utamuwezesha mwananchi kumiliki taarifa zake za kimatibabu kidijitali ambao utamsaidia kukumbuka historia ya matibabu yake hata pale atakapokwenda kutibiwa katika hospitali nyingine ambayo hakutibiwa mara ya kwanza”. Amesema

Pamoja na hayo Mashaka amesema kuwa wanashirikiana na watu wa ulinzi wa data binafsi kuandaa mfumo ili kuhakikisha data za watu zinasafiri salama.

Amesema mfumo huo utaweza kupatikana kwa mfumo wa simu ya kiganjani na kwa ambao hawana simu wameandaa mkakati wa kuanzisha vituo vya pamoja ili waweze kupata taarifa zao na kusisitiza kuwa mfumo huo tayari umeanza katika majengonya posta sehemu mbalimbali nchini.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt. Nkundwe Mwasaga amesema mfumo huo utakwenda kutengeneza miundombinu inayoweza kusaidia upatikanaji wa mazingira wezeshi kwa wabunifu kufanya ubunifu kwa kutumia miundombinu hiyo kupata huduma mbalimbali hususani kwa vijana.

“Kinachofanyika hapa ni kutengeneza mazingira wezeshi ambayo wabunifu wanaweza wakafanya ubunifu wao kupitia miundombinu hii ya kidijitali ambayo inawezesha jamii kupata huduma mbalimbali,” . Amesema Dkt Mwasaga.

Nae Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, Dk Emmanuel Mkilia amewatoa hofu wananchi kwamba kila mtu anatakiwa kuwa na imani kwamba taarifa zake zinalindwa kwani wamezingatia ulinzi katika uandaaji wa mifumo hiyo ili kuhakikisha taarifa binafsi za afya zinabakia kuwa falagha.














Related Posts