Dodoma. Mitambo minane kati ya tisa inayojengwa katika Bwawa la Umeme la Mwalimu Julius Nyerere, imekamilika na mmoja uliobakia utakamilika mwishoni mwa mwezi huu.
Kauli hiyo imetolewa bungeni leo Januari 31, 2025 na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko wakati akichangia kwenye azimio la Bunge la kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mwenyeji wa mkutano wa nishati Afrika (Mission 300) kwa mwaka 2025.
Azimio hilo limewasilisha na Mbunge wa Viti Maalum Asia Halamga na kuchangiwa na wabunge kabla ya kuhojiwa na kukubaliwa kwa kauli moja kulipitisha, huku Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson akitangaza kuwa ni wazo lililoibuliwa na wabunge wanawake.
Katika mchango wake, Dk Biteko ametaja sababu mbili zilizosababisha mkutano huo kufanyika nchini kuwa ni pamoja na kasi ya usambazaji wa umeme vijijini ukilinganisha na mataifa mengine barani Afrika.
Amesema kasi hiyo imewavuta wadau wengi kutaka kushiriki mkutano huo kiasi cha kufanya baadhi ya nchi zilazimike kupunguza idadi ya washiriki lengo ni kutaka kujua Tanzania imewezaje.
“Mfano hapa nyumbani, Watanzania waliotakiwa kushiriki ni 497, badala yake wameshiriki watu 90 tu,” amesema Dk Biteko.
Amesema Mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere (JNHPP) unaojengwa kwa gharama ya Sh6.6 trilioni, mpaka kukamilika kwake, utazalisha megawati 2115 za umeme ingawa kwa sasa Tanzania inazalisha megawati 3,404.
Lakini sababu ya pili, amesema ni kuimarika kwa diplomasia kati ya Tanzania na mataifa mengine.
“Kwa kifupi tu Mheshimiwa Spika mkutano ulipata mwitikio mkubwa, na kwa sababu hiyo nawashukuru kwa jambo hili kwa sababu Bunge hili ni bunge ambalo kazi zake mbili ni kuishauri na kuisimamia Serikali na kwa wakati wote limekuwa likiifanya hiyo kazi kwa bidii kubwa.”amesema Dk Biteko.
Katika hatua nyingine, amesema Wizara ya Nishati imejipanga kuhakikisha kila kilichojadiliwa kinafanyiwa kazi kwa vitendo na hakuna kitakachobaki kwenye makaratasi, kwa kuwa Taifa linatarajia baada ya miaka mitano, Watanzania waliounganishiwa umeme wafikie 13.5 milioni.
Kuhusu nishati safi, Dk Biteko amesema Serikali imelenga kuongeza kasi ya huduma hiyo kutoka asilimia 6.9 hadi kufikia asilimia 75 wakati nishati jadidifu itaongeza watumiaji kutoka asilimia 56 hadi 65.
Kwa upande wake, Dk Tulia ameiomba wizara hiyo kuwa sasa fedha walizokuwa wakizipeleka kwenye miradi ya umeme, zielekezwe kwenye maeneo mengine ili zikawasaidie Watanzania kwani wengi wana uhitaji hasa kwenye miradi ya maendeleo.