Sababu Arusha DC kuvuka mwaka na bakaa ya Sh3.374 bilioni zatajwa

Arusha.  Halmashauri ya Arusha Vijijini imehitimisha mwaka wa fedha 2023/2024 ikiwa na bakaa ya bajeti ya Sh3.374 bilioni, fedha ambazo zilichelewa kuwasili kutokana na changamoto za kimfumo.

Kiasi hicho ni sehemu ya bajeti ya Sh60.2 bilioni iliyoidhinishwa na Serikali Kuu kwa mwaka huo wa fedha.

Katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya ya Arusha (DCC) kilichofanyika leo, Mkuu wa Idara ya Bajeti wa halmashauri hiyo, Anna Urio, ameeleza kuwa kuchelewa kwa fedha hizo kumeathiri utekelezaji wa baadhi ya miradi muhimu ya maendeleo.

Urio amefafanua kuwa fedha zilizobaki zitatumika kukamilisha miradi kadhaa, ikiwemo uboreshaji wa huduma za maji, ukarabati wa soko la Oldonyosambu, pamoja na ujenzi wa kituo cha stendi ya daladala Nduruma na miundombinu yake kama vyoo na maji.

Aidha, kwa mwaka wa fedha 2024/2025, halmashauri imepangiwa bajeti ya Sh67.965 bilioni, ambayo itaelekezwa katika miradi mbalimbali kama vile ukarabati na ujenzi wa madarasa mapya kwa shule zenye upungufu, ujenzi wa mabweni na usambazaji wa huduma za kijamii kama maji safi.

Mtaalamu wa uchumi, Saimon Mapolu ameeleza kuwa ucheleweshaji wa fedha za bajeti unaweza kuathiri utekelezaji wa miradi, hali inayosababisha madhara kwa wananchi.

“Ikiwa bajeti ya Sh2.5 bilioni ilitengwa kwa ujenzi wa zahanati lakini haikutekelezwa kwa wakati, basi mwaka unaofuata kiasi hicho hakiwezi kutosha kutokana na kupanda kwa gharama za vifaa vya ujenzi kama saruji na nondo,” amesema Mapolu.

Ameshauri Serikali kuboresha mifumo yake ya utekelezaji wa miradi ili kuhakikisha fedha zinatumika kwa wakati na kuepusha bakaa zisizo na tija.

Bajeti ya mwaka 2025/2026

Katika kikao hicho, wajumbe waliidhinisha rasimu ya bajeti ya Sh68 bilioni kwa mwaka wa fedha 2025/2026.

Urio amebainisha kuwa bajeti hiyo inalenga kuimarisha mifumo ya ukusanyaji wa mapato na kutekeleza miradi muhimu kama, ukarabati wa shule nne kongwe, upembuzi yakinifu wa ujenzi wa soko la Kisongo na dampo la Bwawani.

Mipango mingine ni uanzishwaji wa miradi ya biashara ya hewa ya ukaa (carbon credits) ili kuongeza mapato na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na uchambuzi wa uwezekano wa kujenga hoteli ya nyota tatu karibu na uwanja wa mashindano ya Afcon.

Mwenyekiti wa kikao hicho, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Amri Mkalipa amewasihi wajumbe waendelee kutoa ushauri wa kuboresha ukusanyaji wa mapato ili kuwezesha utekelezaji wa miradi kwa ufanisi.

Related Posts