Dodoma. Bunge limepitisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria za Kazi namba 13 wa Mwaka 2024, ambapo sasa likizo ya uzazi kwa mwajiriwa ambaye atajifungua mtoto njiti, imejumuisha muda uliobaki wa kufikia wiki 40 za ujauzito, huku baba naye akipewa siku saba za kupumzika.
Shirikisho la Vyama Vya Wafanyakazi nchini (TUCTA) ni miongoni mwa wadau ambao wamekuwa wakipaza sauti zao kutaka kuongezwa muda wa likizo za waajiriwa hao, ili kuboresha ustawi wa watoto hao.
Marekebisho hayo yamewasilishwa leo Januari 31, 2024 na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde kwa niaba ya Waziri Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete.
Akiwasilisha muswada huo, Mavunde amesema awali ilipendekezwa muda wa wiki 36 kama ukomo wa muda wa mtoto kutimia baada ya kuzaliwa kabla ya muda.
Hata hivyo, amesema baada ya majadiliano na kamati, Serikali ilikubaliana na mapendekezo ya kuongezwa muda huo hadi kufikia wiki 40 na kuongeza muda wa likizo ya baba, ambaye atapata mtoto njiti kutoka siku tatu hadi siku saba.
Aidha, Mavunde amesema kifungu kipya cha 34A kinapendekeza kuongezwa ili kumwezesha mwajiri kumpatia mwajiriwa likizo bila malipo isiyozidi siku 30, ili kuweka mazingira mazuri yatakayomwezesha mwajiriwa kutokana na majanga au dharura zinazoweza kujitokeza.
Pamoja na hayo, kifungu cha 14 kinapendekezwa kubainisha aina ya mikataba ya muda maalumu ili kuongeza wigo wa mazingira ambayo mtu anaweza kuajiriwa kwa mkataba wa kipindi maalumu, ikiwamo mikataba ambayo mtu anaajiriwa kwa muda ili kuendana na ongezeko la wingi wa kazi, kutoa fursa kwa wahitimu wa vyuo kuwajengea uwezo na kufanya kazi nyingine za misimu.
Pia, amesema mwajiri na mwajiriwa wanaweza kuingia katika makubaliano ya namna watakavyofanya kazi katika hali ya dharura inayoweza kuathiri uzalishaji mahali pa kazi, wakati wa magonjwa ya milipuko na matukio ya dharura.
Amesema kifungu cha 94 kimeweka masharti ya kuzuia wahusika wa mgogoro kuwasilisha maombi ya mapitio kwa maamuzi madogo ya Tume, isipokuwa kama maamuzi hayo yana athari ya kumaliza mgogoro.
Mavunde amesema Kifungu cha tisa cha Sheria ya Usimamizi wa Ajira za Wageni, Sura ya 436 kimeweka masharti ya kumtaka raia wa kigeni mwenye kibali cha kazi daraja A anayekusudia kujihusisha na kampuni nyingine anayomiliki hisa kupata idhini ya Kamishna wa Kazi badala ya kibali kingine cha kazi.
Amesema marekebisho hayo yanalenga kuondoa usumbufu na kuweka mazingira bora ya uwekezaji kwa mwekezaji ambaye ni raia wa kigeni na mara baada ya kupata kibali cha kazi kwa kampuni moja, hatahitajika kupata kibali kingine kwa kampuni nyingine atakayomiliki hisa.
Amesema kifungu cha 10 kimeweka masharti ya kuzuia urejeshwaji wa ada ya maombi ya kibali cha kazi ili kutoa ufafanuzi kwa waombaji wa vibali vya kazi kuhusiana na ada zinazolipwa wakati wa maombi.
Aidha, kifungu cha 12 kitawawezesha wakimbizi wenye hadhi stahiki kuendelea kufanya kazi bila kubanwa na sharti la ukomo wa muda wa kibali cha kazi.
“Vilevile, kifungu hiki kinarekebishwa ili kuwezesha maombi ya kuhuisha kibali cha kazi kuwasilishwa kwa Kamishna wa Kazi angalau miezi miwili kabla ya kuisha kwa muda wa kibali,” amesema.
Akisoma maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Mwenyekiti wa kamati hiyo Fatma Toufiq, amesema amesema kamati imependekeza kuongeza muda wa likizo ya uzazi kwa mama aliyejifungua watoto njiti kutoka wiki 36 hadi 40.
“Kamati ilipata maoni kutoka kwa wataalamu wa afya na inaamini kuwa kiafya mtoto anakuwa yupo vizuri zaidi akifikia wiki 40, hivyo ikiwa mtoto atazaliwa njiti, mama mzazi atapaswa kupewa likizo ya uangalizi hadi pale atakapofikisha wiki 40. Hali hii itamsaidia kuweza kumhudumia vizuri mtoto njiti,” amesema.
Ameipongeza Serikali kwa kubali ushauri wa kamati na kuongeza likizo kutoka wiki ya 36 hadi 40 kwa mama aliyejifungua mtoto njiti kabla ya kuanza likizo ya uzazi.
Aidha, Toufiq alipongeza hatua ya Serikali kwa kubali ushauri wa kamati yake wa kuongeza kifungu kitakachoweka masharti ya kutoa likizo ya siku saba (7) kwa baba aliyepata mtoto njiti.
“Msingi wa hoja hii ni kutokana na ukweli kuwa kumekuwepo na matukio katika hospitali zetu ambapo baba mzazi hufanya jukumu la kuwapa joto watoto njiti ambao bado wapo katika uangalizi hospitalini,” amesema.
Mbunge wa Mchinga (CCM), Salma Kikwete amewataka wanaume watakaopata likizo ya wiki moja baada ya wake zao kujifungua watoto njiti, kutotumia fursa hiyo kwa shughuli nyingine nje ya kuwasaidia wake zao.
“Mmepewa wiki moja kumsaidia mama kulea mtoto kama mapumziko, basi subiri wakati mwingine kuanzia pale hata ukienda kazini jua kwamba mkeo anahitaji msaada,”amesema.
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Mariam Kisangi amesema kifungu cha 14 cha muswada huo kimerekebishwa ili kuwasaidia vijana waweze kupata ajira za muda.
“Kwa kweli tunatambua katika nchi yetu tumekuwa na wahitimu wengi wa chuo kikuu lakini wengi wako mitaani lakini kwa sheria hii, inakwenda kuwapa nguvu wale wahitimu, wakipata ajira za muda katika makampuni binafsi waweze kuchukuliwa kama watumishi au watu wanaochukua programu ya kuendeleza ujuzi,” amesema.
Mbunge wa Tabora Kaskazini (CCM), Almas Maige amesema muswada huo unapendekeza kufanya marekebisho kifungu cha 16 kwa lengo la kuweka sharti la makubaliano kati ya mwajiri na mwajiriwa katika hali ya dharura.
“Tulipata tatizo la Uviko – 19 na ofisi zikafungwa wafanyakazi wakaenda nyumbani, mwajiri aliendelea kuwalipa mishahara wafanyakazi kwa sababu hakukuwa na makubaliano tufanye nini juu ya hali hiyo.
“Sheria hii inatoa unafuu kwa mwajiri kukaa na mwajiriwa kujadiliana wafanye nini, kazi zimesimama, mwajiri alipe, asilipe au alipe kiasi gani. Kama watashindana, imewekwa CMA (Tume ya Usuluhishi na Uamuzi), kama msuluhishi, aingilie kati ili wafikie muafaka nini kifanyike,” amesema Maige.