Dodoma. Serikali imesema utapeli kwa njia ya mtandao bado ni tatizo huku ikaelezwa chanzo ni kukua kwa teknolojia.
Hoja ya utapeli mtandaoni imebuka bungeni leo na Spika wa Bunge Dk Tulia Ackson amesema haoni juhudi za kukomesha utapeli huo.
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa amesema hayo bungeni leo Januari 31, 2025 wakati akitoa majibu ya nyongeza kufuatia swali la Spika aliyeuliza, ni kwa nini Watanzania wanaendelea kutapeliwa wakati vyombo husika vipo.
Silaa amesimama baada ya wabunge kadhaa kutaka kuuliza maswali ya nyongeza, kufuatia swali la Mbunge wa Makete (CCM) Festo Sanga, aliyeuliza iwapo Serikali haioni haja ya kuzuia usajili holela wa laini za simu mitaani kutokana na utapeli unaoendelea mitandaoni.
Wabunge waliohoji kuhusu utapeli huo ambapo Mbunge wa Nyamagana (CCM) Dk Anjelina Mabula na Spika wamesema bado ni mkubwa, lakini hawaoni wala kupata mrejesho wa taarifa wanazozitoa kwa mamlaka.
“Kwa nini Watanzania wanaendelea kutapeliwa na hivyo vyombo vipo? Jina langu linatumika kutapeli na hivi ninavyozungumza kuna watu wanatapeliwa huko, kila wakati tunatoa taarifa lakini hatupati mrejesho,” amesema Spika Tulia.
Spika amewaagiza wabunge kutoa elimu kwa wapiga kura wao ili watambue kuwa hakuna fedha za bure ambazo zinaweza kutolewa kwa mtu na kwamba yeye (Spika) hawezi kupiga simu na kumwambia mtu akachukue fedha.
Dk Mabula ameungana na Spika akisema majina ya viongozi wakubwa na viongozi wa dini yamekuwa yakitumiwa vibaya kwenye utapeli.
“Sisi ni wahanga (waathirika), watu wengi wanatapeliwa, majina ya viongozi wakubwa yanatumika na majina ya viongozi wa dini yanatumika vibaya, lakini hakuna kinachoendelea pamoja na kelele nyingi,” amesema Dk Mabula.
Katika swali la nyongeza Sanga amehoji iwapo Serikali imeshindwa kudhibiti mtandao wa wahalifu mtandaoni na usajili holela wa laini za simu ambao hufanywa na baadhi ya vijana wasiokuwa na uadilifu.
Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri wa Wizara hiyo Maryprisca Mahundi amesema Serikali imeweka miongozo ya kusajili laini za simu kupitia Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Epoca).
Mahundi amesema miongozo hiyo inahakikisha kuwa laini zote zinasajiliwa kwa alama za vidole, hivyo kutokuwepo kwa mianya ya kusajili laini kiholela. Hata hivyo, amesema wahalifu wa mtandaoni hutumia mbinu kwa kuwalaghai mawakala na watumiaji ili laini zilizokwishasajiliwa zitumike kwenye uhalifu.
Waziri Silaa amesema Novemba 22, 2025 aliitisha kikao kilichowahusisha wadau na sekta mtambuka ikiwemo Jeshi la Polisi ambapo walikubaliana kuongeza nguvu ya kupambana na suala hilo na wameunda kikosi kazi.
Hata hivyo, Waziri alisema utapeli umepungua kwa asilimia 19 ukilinganisha na kipindi cha nyuma huku akihidi kuwa wataongeza nguvu ya mapambano hayo kabla ya kutoa tahadhari na umakini kwa watumiaji wa mitandao kuacha kufungua ‘link’ zinazotumwa.