Sillah awataja Kibu, Pacome | Mwanaspoti

MSHAMBULIAJI wa Azam FC, Gibril Sillah amesema Simba na Yanga zinacheza kwa viwango vya juu, lakini inapotokea wanataka kucheza nazo kuna majina yanayowatisha kiasi cha kukaa chini na kujipanga kukabiliana nayo ili kuiwezesha timu yao kuwa salama.

Nyota huyo raia wa Gambia amesema wakikutana na Simba ni ngumu kukwepa kuwafikiria Kibu Denis na Fabrice Ngoma kwa aina ya uchezaji wa kutumia nguvu, akili na kujitoa kwa ajili ya timu.

“Kibu ni mshambuliaji msumbufu ana nguvu, hakati tamaa katika mipira iliyokufa. Kama mchezaji lazima nitamfikiria endapo tukiwa na mchezo nao,” amesema Sillah.

“Kwa upande wa Yanga kuna Clement Mzize, Pacome Zouzoua na Stephane Aziz Ki haoo jamaa wanajua mpira. Hivyo tukikutana na Yanga huwezi kukwepa kuwawazia jinsi ya kukabiliana nao.”

Mbali na hilo, amezungumzia juu ya kuhusishwa kutakiwa na AS Vita ya DR Congo wakati wa dirisha dogo, kwamba ilitokana na watu kuhusisha ukaribu wake na aliyekuwa kocha wa Azam FC, Youssouph Dabo.

“(Mimi) ni mchezaji wa Azam kama kuna timu itanihitaji basi itawasiliana na viongozi maana kila kitu kipo wazi. Kuhusu kama nimeongeza mkataba mpya Azam bado sijafanya hivyo,” amesema Sillah.

Kuhusu malengo yake ya msimu huu amesema anatamani kufunga mabao 10 na sasa anamiliki matatu.

“Msimu uliopita nilimaliza na mabao manane, ila awamu hii yasiwe chini ya 10 nipo tayari kupambana kulitimiza hilo.”

Related Posts