Uzembe wasababisha ndoo 18 za rangi kuharibika kwa kukosa malipo ya fundi

Geita. “Hakuna zaidi ya uzembe, kilichofanyika ni uzembe.” Hii ni kauli ya Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Geita, Azza Mtaita aliyoitoa akielezea mkwamo wa ujenzi wa Kituo cha Afya cha Isabageni kinachojengwa kwa zaidi ya Sh726 milioni, kukwama kwa zaidi ya miaka mitano huku vifaa vilivyonunuliwa vikiisha muda wake kabla ya kutumika.

Kituo hicho kinachojengwa katika Wilaya ya Geita baadhi ya majengo yamekamilika lakini hayajafungwa vifaa vya maji na umeme kama mkataba wa ujenzi unavyoeleza, huku ndoo 18 za rangi zenye thamani ya Sh2.4 milioni zikiharibika kabla ya kutumika.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Januari 31, 2025 Mtaita, amesema vifaa vilivyoharibika vilikaa muda mrefu na uchunguzi umebaini sababu za kukaa kwake ni kukosekana kwa fedha za kumlipa fundi.

“Ni uzembe tu, huwezi kusema wamekosa fedha za kumlipa fundi na kuacha vifaa viharibike, mengine ni utetezi tu, lakini kubwa tumebaini uzembe na ndio maana tumemwagiza mkurugenzi achukue hatua kwa wahusika, ambao ni kamati ya ujenzi na ofisa mtendaji wa kata ya Isabageni kwa kusababisha hasara, na tumeelekeza hasara iliyopatikana ilipwe,” amesema Mtaita.

Akizungumzia kusuasua kwa ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilomita 17 zinazojengwa kwa kiwango cha lami katika Manispaa ya Geita, Mkuu huyo wa Takukuru amesema tayari wameishauri mamlaka ya juu (Tamisemi), kuvunja mkataba na mkandarasi anayejenga barabara hizo.

Amesema barabara hizo zinazojengwa kwa gharama ya Sh22.5 bilioni kwa fedha za mkopo wa Benki ya Dunia (WB) ujenzi wake ulianza Novemba 2023 na unapaswa kukamilika Februari 19, 2025 lakini hadi sasa ujenzi uko chini ya asilimia 30.

Mtaita amesema wamebaini mkandarasi alipewa kazi na Tamisemi na Halmashauri ya Geita ni msimamizi, hivyo haina mamlaka juu ya mradi huo.

“Huu mradi uko nyuma ya muda na tumefuatilia tumebaini uwezo wa mkandarasi ni mdogo na hakutafutwa na halmashauri, walikubaliana wizarani na alikuja huku kuutekeleza lakini halmashauri yeyewe ni msimamizi tu, haiwezi kumchukulia hatua yoyote mkandarasi, hivyo tumeishauri mamlaka ya juu kuvunja mkataba huo,” amesema Mtaita.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Rajabu Karia alipotafutwa na Mwananchi kujua hatua alizochukua kwa waliohusika na uzembe huo, amesema kwa sasa yuko safarini hivyo hangeweza kulizungumzia.

Ikorongo Otto, mkazi wa Geita ameipongeza Takukuru kwa hatua ilizochukua lakini akasema uzembe huo umesababisha hasara kwa wananchi.

Amesema ni vema wahusika wakachukuliwa hatua kwa mujibu wa taratibu za kiutumishi.

Kuhusu ujenzi wa barabara za lami zinazojengwa mjini Geita, amemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuingilia kati akidai hakuna wa kuinyooshea kidole wizara zaidi ya Rais.

Related Posts