Dar es Salaam. Kaulimbiu ya Chadema ya “No Reform, No Election” imewaibua vigogo wa CCM ambao kwa nyakati tofauti wameizungumzia majukwaani wakiipinga huku wakieleza kwamba haina maana na kama wana hoja waende kuzungumza.
Kaulimbiu hiyo inayosimamiwa na Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu ina maana kwamba hakutakuwa na uchaguzi kama hakuna mabadiliko ya sheria zinazosimamia masuala ya uchaguzi pamoja na kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi.
Viongozi tofauti wa CCM wamesema amri hiyo ya Chadema haiwezi kutekelezwa kwa sababu ni shuruti, hivyo Chadema kama hakitaki kwenda kwenye uchaguzi, basi vyama vingine 18 vilivyosajiliwa vitashiriki uchaguzi huo.
Akizungumza Januari 23, 2025, jijini Dodoma, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Stephen Wasira alisema kaulimbiu ya Chadema ya “No Reform, No Election” haina maana yoyote kwa sasa, akisisitiza kuwa muda wa kufanya mabadiliko ya kisheria umekwisha kutokana na uchaguzi mkuu kukaribia.
Wasira alieleza kuwa CCM ni chama kikubwa, hakiwezi kushurutishwa na chama kidogo kama Chadema kupitia amri wanayoitoa ya “No Reform, No Election”.
“Bunge linavunjwa Juni 2025, sasa reforms anafanya nani? Bunge kazi yake ni kutunga sheria na sheria zina utaratibu wake wa kawaida wa kutunga sheria. Hili Bunge litavunjwa utaratibu huu haujaisha,” alisema Wasira.
Aliongeza kuwa: “Kauli ya ‘No Reform, No Election’ haina nafasi kwa sasa. Rais Samia Suluhu Hassan na CCM wameonyesha utayari wa mazungumzo, na Bunge linakaribia kuvunjwa, hivyo hakuna muda wa kufanya mabadiliko ya kisheria yanayohitaji muda mrefu.”
Jana, Januari 30, 2025, akiwa kwenye moja ya ziara zake huko Zanzibar, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla alieleza kwamba Lissu aliongea kwa ndimi mbili baada ya kupata shinikizo kutoka kwa viongozi wenzake wanaoutaka ubunge na udiwani.
Makalla amempongeza Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu kwa kuweka wazi kwamba chama chake hakijasusia uchaguzi kupitia kaulimbiu yake ya “No Reforms, No Election”.
Amesema katika mazungumzo ya Lissu, alimsikia akisema suala la “No Reforms, No Election” ni jambo moja, jambo lingine ni kwamba hawajasusia uchaguzi huo, kitu ambacho ni tofauti ni msimamo wake wa awali katika kaulimbiu yake.
“Hatujasusia uchaguzi, tafsiri yake ni nini? Kimsingi amekubali, hatasusia uchaguzi, tutakwenda nao kwenye uchaguzi.
“Tunampongeza Tundu Lissu kwa kauli ya ndimi mbili, lakini watu wazima tuliosoma Cuba tumemwelewa, atashiriki uchaguzi,” Amesema Makalla wakati akizungumza na wanaCCM huko Zanzibar anakoendelea na ziara yake ya siku sita.
Hata hivyo, Makalla alimkumbusha Lissu kwamba uchaguzi utafanyika kwani yeye ni chama kimoja na kuna vyama vingine 18 vilivyosajiliwa. Pia, amesisitiza kwamba mabadiliko yanafanywa na Bunge.
Januari 29, 2025 wakati akikabidhiwa ofisi za chama, Lissu alisema suala la “No Reforms, No Election” wanakwenda kulitengenezea mkakati wake wa utekelezaji kwani limepata baraka za kamati kuu na mkutano mkuu.
Amesema wanapozungumzia “No Reforms, No Election”, wanazungumzia njia zisizo za kawaida za kushurutisha mageuzi. Amesisitiza kwamba Bunge linaweza kukaa muda wowote kufanya hayo mageuzi.
“Tunakwenda kufanya harakati, na harakati za nguvu…Tutanyamaza tukiwa tumekufa au tuko gerezani. Tukiwa gerezani, hakuna kunyamaza.
“Tukifanya shuruti sawasawa, tutapata mageuzi na tutakwenda kwenye uchaguzi kwa mfumo mpya wa mageuzi. Tukifanya kwa kujaribu…hatutafika popote. Naomba tujiandae,” amesema mwenyekiti huyo wa Chadema.