Ving’ora, vimulimuli janga barabarani | Mwananchi

Dar es Salaam. Januari 26-28, 2025 baadhi ya maeneo ya Jiji la Dar es Salaam yalikuwa kwenye mwonekano tofauti na ule uliozoeleka kwa muda mrefu. Barabara takribani tisa za kuingia katikati ya jiji zilifungwa kwa muda ndani ya siku sita huku ulinzi ukiimarishwa kila kona.

Mabadiliko hayo yalilenga kuhakikisha  usalama na utulivu kwa wageni waliohudhuria mkutano wa kimataifa kuhusu nishati.

Mkutano huo ni mwendelezo wa heshima kwa Tanzania, kupewa fursa ya kuandaa mikutano mikubwa ya kimataifa inayojadili ajenda zenye maslahi mapana kwa bara la Afrika na wananchi wake.

Tofauti na siku nyingine, ndani ya siku hizo harakati za maisha ya kawaida zilibadilika. Wafanyakazi wa umma na taasisi binafsi walipewa fursa ya kufanya kazi majumbani kama hawakuwa na majukumu ya kuwalazimu kwenda ofisini. Wanafunzi  nao wakapitiwa na fursa hiyo,  kwani shule na vyuo nazo zilifungwa kwa muda.

Hata zile vurugu za bodaboda na bajaji zikakoma baada ya kupigwa marufuku kuingia katikati ya jiji.

Katika barabara na maeneo yote yaliyokusudiwa kuwa chini ya uangalizi maalumu usafi ulikuwa wa hali ya juu. Wafanyabiashara ndogondogo wanaopanga bidhaa pembeni mwa barabara walienda likizo kwa muda, kwa kifupi Dar ilibadilika.

Hoja kubwa kwa jamii imebaki kuwa, kumbe Serikali au Jeshi la Polisi zikiamua jambo  linawezekana.

Marufuku za bodaboda na bajaji kuingia katikati ya Jiji la Dar es Salaam na zingine zikiwemo za kuwaondoa machinga na ombaomba zimefanyika mara kadhaa, lakini huishia njiani bila mafanikio.

Hata hivyo, kwa sasa kero kubwa ni matumizi ya ving’ora na taa maarufu kama vimulimuli zilizofungwa kwenye magari ya Serikali na ya watu binafsi.

Matumizi hayo yamekuwa janga kubwa kwenye barabara za Tanzania kwa sasa kiasi cha watumiaji wengine kutofahamu cha kufanya wanapokutana na magari hayo.

Si kila gari linastahili king’ora na kimulimuli kwa mujibu wa Sheria ya usalama barabarani ya mwaka 1973 kifungu cha 54  iliyofanyiwa marekebisho 2002.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, magari yanayotakiwa kuwa na ving’ora na vimulimuli ni ya majeshi, dharura, kubebea wagonjwa, misafara ya viongozi na yale ya kusindikiza fedha.

Mbali na matumizi ya vifaa hivyo ambavyo vimekuwa vikiuzwa holela mitaani, janga lingine ni matumizi ya namba za magari zinazotumiwa na baadhi ya madereva.

Inafahamika kuwa zipo namba zinazowakilisha mashirika ya umma, taasisi za kijeshi, wanadiplomasia, namba maalumu za majina zinazotambulika kisheria.

Hata hivyo, yapo magari barabarani yenye namba za mataifa mengine au zinazotakiwa kutumika kwa kipindi fulani wakati taratibu zingine zikisubiriwa na huruhusiwa kutembea kwa muda maalumu.

Lakini, magari haya yamekuwa yakikiuka sheria ya usalama barabarani, inayokataza kuongeza kitu chochote kwenye gari zaidi ya vile lilivyotoka kwa mtengenezaji.

Sheria hiyo imekwenda mbali zaidi na kueleza, iwapo inahitajika kuongeza chochote ni lazima kuwasiliana na polisi kwa ukaguzi.

Pamoja na kuwepo kwa sheria inayokataza, magari hayo yanaendelea kuleta sintofahamu hasa yanapohusika kwenye matukio ya uhalifu na uvunjifu wa sheria za usalama barabarani. Swali ni je, Jeshi la Polisi limeshindwa kukabiliana na janga hili ama halijaamua?

Akizungumzia hayo, Januari 30, 2025 Mkaguzi wa Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani, Dumu Mwalugenge amekiri kushamiri kwa vitendo hivyo na kwamba tangu mwaka 2024 waliowaonya wamiliki wa magari wanaokiuka sheria na sasa wanaendelea na ukamataji.

“Tumeona kuna matumizi holela ya ving’ora kwa mtu kwenda dukani kununua na kubandika lakini hilo tunalikomesha kwa kuwachukulia hatua wahusika na tumeng’oa vingora na vimulimuli kwenye operesheni zinazoendelea,” amesema Dumu.

Amesema sheria imeweka wazi na imeelekeza magari yanayotakiwa kuwekewa ving’ora na vimulimuli, huku akitoa tahadhari kwa magari binafsi, mashirika ya umma na Serikali kufuata taratibu na sheria za usalama barabrani.

“Unapokuwa na gari ya Serikali sio kwamba linapewa sifa kuwa na king’ora yenyewe pia yanatakiwa yafuate utaratibu wa kuomba ridhaa na kisha kukaguliwa na kuwekewa hicho walichoomba, kama hakuna kibali tutavitoa na tutamchukulia hatua dereva,” amesema.

Amesema madereva wa magari ya Serikali wamekuwa wakiweka vifaa hivyo kinyume na sheria na kusababisha bughuza kwa watumiaji wengine wa barabara.

Dumu amesema wakati mwingine magari hayo yamekuwa yakisababisha foleni kwa kutofuata sheria kwa sababu ya kujichomeka ili kupewa kipaumbele wakati hawana hiyo fursa.

“Tumekuwa wakali kwenye operesheni zetu tulizozifanya,  hatua ya kwanza tumeondoa vimulimuli na ving’ora na wahusika tumewachukulia hatua za kisheria ikiwemo faini na wengine tumewapeleka mahakamani,” amesema.

Kamanda Dumu amesema kwa mwaka 2024 walifanikiwa kuyakamata magari 4,641 na pikipiki 4,074 yaliyokuwa yamefunga ving’ora kinyume na sheria kwa Tanzania nzima.

Katika Sheria ya usalama barabarani, Kifungu cha 53 kinasema kuwa kila gari lazima liwe na namba ya usajili inayotambulika na mamlaka husika (kama vile TRA – Mamlaka ya Mapato Tanzania).

Matumizi ya namba bandia au zisizoidhinishwa ni kinyume cha sheria na kwa kawaida hushughulikiwa chini ya kifungu cha 54, ambacho kinatoa adhabu kwa wale wanaokiuka sheria hii.

Dumu amesema hata hilo wamelichukulia hatua kwa kukamata na kuvitoa vibao kwenye magari.

“Operesheni yetu inafanyika nchi nzima ya juu ya namba zisizotambulika na watu wakae wakijua hilo na kwa wale ambao bado hawajabadilisha namba zao wafanye hivyo,” amesema.

Amesema inatambulika wazi kwa magari ambayo bado hayajapata usajili hutembea mwisho saa 12 jioni zaidi ya hapo tunakamata na utaratibu mwingine unaendelea.

Mkurugenzi wa Taasisi inayotoa elimu ya usalama barabarani (TARSI), Maliki Barongo amesema katika utekelezaji wa sheria,  Jeshi la Polisi linatakiwa kutoa elimu kwa kina kuhusu ving’ora na vimulimuli kama ilivyokuwa kwa katazo la namba za 3D.

Amesema msingi wa elimu hiyo utasaidia kwenye shughuli ya kukamata walioshindwa kutekeleza matakwa ya sheria kama ilivyowezekana kuzuia bodaboda na bajaji kuingia mjini kipindi cha mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika.

“Elimu ndiyo msingi bora wa kutii sheria zilizopo, Jeshi la Polisi wakifanya hivyo itasaidia hata kwa wale wakaidi wanapokamatwa kwa kutotii sheria, kwaani watakuwa mabalozi wa wengine,”amesema Mwarongo.

Related Posts