Viongozi SADC waahidi kurejesha amani DRC

Mwanza. Mkutano wa dharura wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) umesema lengo la wanachama wa jumuiya hiyo ni kuona amani inarejea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Kauli hiyo imetolewa na Rais wa Zimbabwe, Dk Emmerson Mnangagwa ambaye ni Mwenyekiti wa SADC wakati wa mkutano wa dharura wa jumuiya hiyo ulioitishwa jijini Harare kwa lengo la kujadili kutetereka kwa amani DRC.

Hali ya usalama ilianza kuyumba DRC baada ya kundi la waasi wa M23 kuanza uvamizi na kuyashikilia maeneo ya mashariki mwa DRC ikiwemo mji wa Goma.

Kwa mujibu wa Mnangagwa, suala la ulinzi wa raia nchini humo si la hiari, bali la kisheria kwa mujibu wa makubaliano yaliyosainiwa na nchi wanachama wa SADC.

“Ni kwa bahati mbaya nasema kwamba tangu mkutano wetu wa mwisho hali ya amani imetetereka nchini DRC. Mashambulizi ya M23 yamegharimu maisha ya wanajeshi wetu wanaolinda amani DRC chini ya SAMIDRC na kuwaacha wengine wakiwa wamejeruhiwa vibaya,” amesema Dk Mnangagwa.

Amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania kwa kuchukua hatua za haraka za kuitisha mkutano wa dharura na wakuu wa nchi na Serikali kupitia Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-Troika).

“SADC inaamini kwamba kusitishwa kwa mapigano ya DRC na M23 ndiyo namna pekee ya kukomesha umwagaji wa damu nchini humo. Vikosi vyetu vya SAMIDRC vimetuhakikishia kwamba viko imara na vinaendelea kulinda amani nchini humo,” amesema Dk Mnangagwa.

Rais wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-Organ), Samia Suluhu Hassan akishiriki mkutano wa dharura wa wakuu wa nchi na serikali wa SADC katika ukumbi wa New Parliament Building, Harare nchini Zimbabwe leo Januari 31, 2025.

Awali, Katibu Mtendaji wa SADC, Elias Magosi amewaeleza washiriki kwamba wanajeshi wa SADC kupitia SAMIDRC na Kikosi cha Ulinzi wa Amani cha Umoja wa Mataifa (Monusco) wamekuwepo nchini DRC tangu mwaka 2013.

“SADC imekuwa ni miongoni mwa jumuiya zinazohimiza na kuimarisha usalama wa DRC, vikosi vyetu vimekuwa vikitekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria na miongozo ya SADC kwa lengo la kupata maendeleo endelevu,” amesema Magosi.

Amesema uvamizi wa M23 mashariki wa DRC umesababisha vifo vya walinda amani wa SADC na Monusco zaidi ya 16 huku wengine (idadi haijatajwa) wakijeruhiwa vibaya.

“Tunatoa pole kwa familia ambazo zilipoteza wapendwa wao katika mapigano ya M23 nchini DRC dhidi ya vikosi vya Serikali,” amesema.

Mbali na Rais Samia na Mnangagwa (Zimbabwe), Mkutano huo wa siku moja umehudhuriwa na Andry Rajoelina (Madagascar), Cyril Ramaphosa (Afrika Kusini), Duma Boko (Botswana) na Daniel Chapo (Msumbiji).

Marais wengine walioshiriki kwa njia ya mtandao ni Felix Tshisekedi (DRC) na Hakainde Hichielema (Zambia).

Pia, Sam Matekane (Waziri Mkuu wa Lesotho), Thulisile Dladla (Naibu Waziri Mkuu Eswatini), Balozi Tete Antonio (Waziri Mambo ya Nje Angola) na wengine walioshiriki kwa mtandao.

Related Posts