Viungo vya mwili wa mtua asiyejulikana vyaopolewa kwenye shimo la choo

Dar es Salaam. Viungo vya mwili wa mtu asiyejulikana vimetolewa kutoka kwenye shimo la maji taka lililopo nyumba moja iliyopo kati ya mitaa ya St. Mary na Bluesky, Tabata, Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam.

Tukio hilo limezua taharuki miongoni mwa wakazi wa eneo hilo baada ya wafanyakazi wa gari la maji taka kugundua mwili huo wakati wakinyonya majitaka kwenye shimo hilo.

Viungo vya mwili huo wa binadamu vimebainika Januari 27, 2025, jioni na taarifa zilifikishwa kwa Jeshi la Polisi Januari 28, 2025, asubuhi na mwenye nyumba husika aliyejitambulisha kwa jina la Nivo Mremi.

Akizungumza na Mwananchi Digital, Mremi amesema alipata taarifa kutoka kwa dereva wa gari la maji taka, aliyemuajiri kwa kazi ya kusafisha mashimo kwenye nyumba hiyo.

Kwa mujibu wa Mremi, yeye si mkazi wa eneo hilo, anaishi Kibaha mkoani Pwani na mara chache hufika kutembelea nyumba yake.

Amesema Januari 27, 2025 alifika nyumbani hapo kwa ajili ya kuikagua na aifanyie marekebisho kadhaa, ikiwa ni pamoja na kuondoa majitaka kwenye mashimo hayo.

“Kwa kufanya hivyo niliamua kuita gari la majitaka ambalo nililisubiri kwa muda mrefu na baada ya kuona linachelewa, niliamua kuondoka na kuacha maagizo kwa mtoto wangu pamoja na fedha za malipo yao,” amesema Mremi.

Akiwa njiani kuelekea Kibaha, Mremi anasema alipigiwa simu na dereva wa gari la maji taka akimtaarifu kuhusu kitu kisicho cha kawaida walichokibaini ndani ya shimo.

Anasema alimwambia kuwa waliona kitu kama mfuko wenye kitu ndani. Hata hivyo, kwa kuwa hakujua ukubwa wa tatizo hilo, alimjibu dereva kwamba angerudi kesho yake.

Mremi anasema aliporudi kesho yake, naye aliona nguo ndani ya shimo na aliposukuma kwa mti, aliona kichwa na mguu wa binadamu.

Anasema walitoa taarifa kwa viongozi wa mtaa ambao walimshauri akatoe taarifa Kituo cha Polisi Tabata Shule, na askari walifika eneo la tukio na kuwaita Askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wa Mkoa wa Ilala kwa msaada wa uokoaji.

Mwananchi limezungumza na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Kamishna Msaidizi Mwandamizi Mabusi Peter kuhusiana na tukio hilo na amesema walipokea taarifa ya tukio hilo Januari 27 saa 9:30 alasiri na walifika eneo la tukio, lakini walikabiliwa na changamoto ya nafasi ndogo ya shimo hilo, lenye upana wa takriban mita moja na kina cha futi sita hadi nane.

Amesema wakati wa uokoaji walichokiona si mwili mzima, bali ni mabaki ya mwili ambao inaonekana ulitumbukia siku kadhaa zilizopita.

 “Harufu kali ilikuwapo kiasi cha kusababisha changamoto. Vijana walifika jioni na walihangaika na kazi hiyo hadi saa moja usiku kabla ya kusitisha shughuli hizo,” amesema kamanda huyo.

Hata hivyo, amesema waliporejea siku ya pili kuendelea na kazi hiyo walifanikiwa kuopoa vipande vipande vya mwili.

Kamanda Peter amesema mpaka anazungumza na Mwananchi, waokoaji tayari walikuwa wameopoa baadhi ya viungo, ingawa inaonekana baadhi vinakosekana.

“Kutokana na upungufu huo, niliagiza shimo hilo lisafishwe lote kwa kuondoa tope ili kuhakiki kama kuna viungo vingine vimenasa kwenye tope la shimo,” amesema.

Mkazi mmoja wa eneo hilo, ambaye hakutaka jina lake litajwe, amesema tukio hilo limewashangaza kwa kuwa hawajawahi kunusa harufu yoyote mbaya kutoka ndani ya nyumba hiyo.

“Hata watu waliokuwa wakiishi hapa nao tulikuwa tunawaona tu wakiingia na kutoka na  mpangaji mmoja aliondoka na vitu vyake  kuchukua mwanamke, tunashangaa leo tunasikia habari hizi na hatujui aliyekufa ni nani maana humu ndani pia waliishi Waarabu,” amesema jirani huyo.

Amesema siku iliyobainika tukio hilo, walishangaa kuona maaskari wakiingia na kutoka na walipojaribu kuuliza waliambiwa kuna mtu kafia ndani ya shimo la choo.

“Tulidhani katumbukia siku hiyo, kumbe ni muda mrefu,” amesema jirani huyo.

Related Posts