Ajali ndege ya kusafirisha wagonjwa yaua sita Marekani

Philadelphia. Jinamizi la ajali za ndege limeendelea kuikumba Marekani baada ya ndege iliyokuwa imebeba mgonjwa, mama yake na wahudumu wanne kupata ajali na kuanguka eneo la Philadelphia nchini Marekani.

Ndege hiyo ilipata ajali saa 12:30 jioni muda mfupi baada ya kuondoka katika uwanja nchini Marekani kumpeleka mgonjwa huyo katika matibabu ya dharura jijini Tijuana nchini Mexico kisha kusababisha mlipuko mkubwa wa moto katika makazi ilipodondoka.

Taarifa kwa umma ya Shirika la Jet Rescue linalomiliki ndege hiyo inayotumika kusafirisha wagonjwa ilisema:

“Hadi sasa hakuna manusura katika ajali hiyo.” Taarifa hiyo ilieleza kwamba athari za ajali ya ndege hiyo eneo ilipodondokea bado hazijafahamika.

Msemaji wa shirika hilo ndege hiyo, Shai Gold amesema waliokuwemo ndani ya ndege hiyo ni raia wa Mexico akiwemo mtoto aliyekuwa akisumbuliwa na maradhi yaliyokuwa tishio kwa uhai wake jambo lililowalazimu wazazi wake kumpeleka Mexico kwa matibabu zaidi.

Kwa mujibu wa Gold, ndege hiyo ilipaswa kutua mjini Missouri kabla ya kuelekea kutua jijini Tujuana nchini Mexico ambako mtoto huyo alipaswa kupelekwa kwa matibabu.

Msemaji huyo amesema wahudumu waliokuwemo ndani ni watumishi wenye uzoefu kwenye sekta ya anga na afya,  huku akisisitiza kuwa wamekuwa wakijengewa uwezo kila mara wa namna ya kufanya shughuli hiyo.

“Janga la aina hii linapotokea inakuwa inashangaza kwa kweli,” Gold amelieleza Shirika la Habari la Associated Press huku akidokeza kuwa ndege zote za shirika hilo zimekuwa zikifanyiwa ukaguzi wa mara kwa mara kuimarisha usalama wa wagonjwa wanaosafirishwa.

Gavana wa Pennsylvania, Josh Shapiro akitoa taarifa kwa vyombo vya habari amesema madhara ya ajali ya ndege hiyo huenda yakaongezeka huku akisisitiza kuwa ufuatiliaji bado unaendelea.

“Tunatambua kuwa kutakuwa na vifo eneo ambalo imedondokea,” amesema Shapiro.

Ndege hiyo ilisajiliwa nchini Mexico ambako ndiko  yalipo makao makuu ya Shirika la Jet Rescue ambalo linatoa huduma za kusafirisha wagonjwa kati ya Mexico na Marekani.

Ajali hiyo imetokea zikiwa zimepita siku mbili pekee tangu itokee ajali ya Shirika la Ndege la American Airline iliyogongana na ndege ya kijeshi ya Black Hawk jijini Washington nchini humo.

Ndege hiyo ilikuwa imebeba abiria 60 na wahudumu wanne,  huku helikopta ya jeshi la nchi hiyo ikiwa na wanajeshi watatu waliokuwa mafunzoni.

Katika ajali hiyo hakuna aliyenusurika na tayari miili zaidi ya 45 imeshaopolewa kutoka ndani ya Mto Potomac uliopo jijini Washington nchini humo. Kwa mujibu wa mamlaka,  ndege hiyo ilikuwa ikitokea Wichita kwenda Washington nchini humo.

Historia inaonyesha ajali ya ndege iliyotokea eneo la Philadelphia ni ya pili kwa shirika la Jet Rescue katika kipindi cha miezi 15 iliyopita.

Ajali nyingine ilitokea 2023, ambapo wahudumu watano akiwemo rubani walifariki dunia baada ya ndege ya shirika hilo kuvuka njia ya kurukia mjini Morelos nchini Mexico na kugonga mlima.

Kipande cha video kilichorekodiwa na kamera ya mlangoni kinaonyesha ndege hiyo kwa umbali ikishuka kwa kasi na kugonga majengo ya maduka karibu na barabara kisha kulipuka na kusababisha moto uliotapakaa eneo hilo.

“Tulichosikia ni kelele na kishindo japo hatukujua zilitokea wapi. Baada ya kugeuka kuangalia tuliona moto mkubwa unawaka,” amesema Jim Quinn, ambaye kamera iliyoko kwenye mlango wa nyumba yake ilirekodi tukio hilo.

Ajali hiyo imetokea umbali wa takriban kilometa tano kutoka ulipo uwanja wa ndege Kaskazini Mashariki mwa Philadelphia, uwanja huo hutumiwa na ndege za kibiashara na za mashirika binafsi.

Kwa mujibu wa mamlaka ya usimamizi wa viwanja vya ndege, ndege hiyo (Learjet 55) ilitoweka kwenye rada baada ya kuruka kutoka uwanjani jana saa 12:06 jioni katika umbali wa futi 1,600 angani (mita 487).

Tovuti ya Flight Aware imeandika kuwa ndege hiyo ilisajiliwa kama ndege ya kutoa huduma ya matibabu nchini Mexico.

Kwa upande wake, Rais Donald Trump amechapisha katika akaunti ya mtandao wake wa Truth Social kuwa: “Nimesikitishwa na kitendo cha kuona ndege nyingine ikianguka huko Philadelphia.”

“Nafsi nyingine za watu wasio na hatia zimeondoka, watu wetu kwa hakika wameathiriwa na tukio hili,” ameandika.

Michael Schiavone (37) ambaye ni mkazi wa eneo ilipoanguka ndege hiyo, amesema akiwa ameketi nyumbani kwake Mtaa wa Mayfair, alisikia kishindo cha mkito wa ndege hiyo ardhini jambo ambalo anasema lilimshtua.

Amesema alihisi ni tetemeko la ardhi limetokea eneo hilo hadi pale alipobaini kuwa majengo yenye maduka yanateketea. Pia, alipoenda kutazama kamera za usalama zilizoko kwenye nyumba yake, ndipo aliposhuhudia tukio hilo.

“Kulikuwa na moto mkubwa ambao ulinifanya nihisi kuwa tumevamiwa tena na janga la moto kwa mara nyingine,” amesema.

Uchunguzi wa chanzo cha ajali hiyo umeanza na taarifa zaidi zitatolewa.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika.

Related Posts