Ajali zawasukuma madereva bodaboda kuchangia damu

Kahama. Waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda wa Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga,  wamejitolea kuchangia damu katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama mkoani humo ili kunusuru maisha ya wahitaji wa huduma hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Hospitali ya Manispaa ya Kahama mkoani humo, wastani wa  12 hutumika kila siku huku majeruhi wa ajali  za pikipiki na wajawazito wakitajwa kuwa miongoni wahitaji wakuu wa damu hospitalini hapo.

Bila kutaja idadi ya wagonjwa wa ajali wala wajawazito wanaojifungua, Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk Daniel Mzee amesema hospitali hiyo inakabiliwa na upungufu mara kwa mara.

“Wahitaji wakubwa damu ni wajawazito, kabla, wakati na baada ya kujifungua, watoto chini ya miaka mitano wanaougua malaria, wenye utapiamlo, wagonjwa wa selimundu na madereva bodaboda wanaopata ajali,” amesema Dk Mzee.

Kwa mujibu wa Dk Mzee,  madereva hao kupitia uchagiaji wao walioufanya kwa siku mbili mfululizo kuanzia Ijumaa, Januari 31,2025, wamefanikisha kupatikana uniti 56 zitakazofanyiwa uchunguzi kwenye maabara kabla ya kutumika kwa wagonjwa wenye uhitaji.

“Matumizi yetu ya damu kwa siku ni uniti 10 hadi 15  kwa siku katika hali ya kawaida ikitokea wahitaji wakaongezeka,  basi huenda ikavuka hapo kiasi kwamba inakuwa changamoto kuipata ama tunalazimika kuomba kutoka vituo vya mbali,” amesema Dk Mzee.

Madereva bodaboda hao wamejitokeza kuchangia damu kupitia hamasa ya kampeni maalum inayoratibiwa na Taasisi ya Okoa Jamii inayojishughulisha na kutoa misaada ya kibinadamu mkoani humo.

Mbali na kuchangia damu hiyo, Okoa Jamii na madereva hao wamefanya usafi kuzunguka hospitali hiyo na kukabidhi mashuka 50 yatakayotumika kwenye wodi ya wajawazito hospitalini hapo.

Dereva bodaboda wilayani humo, Metusi Elias ametoa wito kwa Watanzania wengine kujitoa kuchangia damu,  kwa kile alichodai damu hailimwi wala kutengenezwa badala yake inapatikana kwa kuchangia.

“Tunapaswa kujitoa na kuchangia damu kila mara na kwa kufanya hivyo tutaokoa maisha ya ndugu zetu ambao wana uhitaji wakiwemo wajawazito, watoto na wenzetu wanaopata ajali barabarani,” amesema Elias.

Kauli ya Elias, imeungwa mkono na Taison Davis ambaye amekiri kusukumwa kuchangia damu hiyo kutokana na mwenendo wa uwepo wa madereva wanaopata ajali na kuhitaji huduma ya damu wakati wa matibabu yao ikiwemo wanapofanyiwa upasuaji.

“Nimechangia damu kuokoa maisha ya kina mama wanaojifungua na madereva bodaboda wanaohitaji damu. Naomba na wenzangu wengine wajitokeze waweze kuchangia damu tuokoe maisha ya wenzetu,” amesema Taison.

Awali, Meneja Mradi wa Taasisi ya Okoa Jamii, Koga Siminzile alieleza kuwa mbali na kurejesha kwa jamii, hamasa hiyo ya kuchangia damu inasukumwa na uhalisia wa uwepo wa mwamko mdogo wa umma kujitokeza kuchangia damu katika vituo vya afya.

“Jamii inapaswa kuongeza mwamko wa kujitolea na kufanya matendo ya huruma ikiwemo kushiriki shughuli mbalimbali hususan  hospitalini, kuwafariji wagonjwa pamoja na kuunga mkono juhudi za Serikali katika utoaji wa huduma bora za afya kwa jamii,” amesema Siminzile.

Related Posts