Bei mafuta ya kura yapasua vichwa wananchi Iringa

Iringa. Wananchi mkoani Iringa wamelalamikia kupanda kwa bei ya mafuta ya kula katika masoko mbalimbali, wakieleza kuwa hali hiyo inaathiri bajeti zao za kila siku.

Wakizungumza na Mwananchi leo, Februari 1, 2025 kwa nyakati tofauti, baadhi ya wananchi hao wamesema awali walikuwa wakinunua lita moja ya mafuta ya kula kwa kati ya Sh4,500 na Sh5,000, lakini sasa bei imepanda na kufikia kati ya Sh6,500 na Sh7,000.

Anna Agustino mkazi wa Kisesa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, amesema  leo amenunua dumu la lita tano kwa Sh35,000 kutoka Sh24,000 ya awali.

“Kwa sasa maisha yamekuwa magumu zaidi, hata bidhaa za msingi kama mafuta ya kula zimepanda bei. Hii ni changamoto kubwa hasa kwa familia zenye kipato kidogo,” amesema Agustino.

Wananchi wamesema ongezeko hili limekuwa mzigo mkubwa kwao kwani mafuta ya kula ni bidhaa muhimu inayotumika kila siku katika familia nyingi.

Nao wauzaji wa chakula maarufu mama lishe,  na wakaanga chipsi pia wamelalamikia hali hiyo, wakisema imewapunguzia wateja.

“Kupanda kwa bei ya mafuta kumetulazimu kupandisha bei ya vyakula tunavyouza zikiwamo chipsi, wateja wanakimbia,” amesema Amina Jafari, mama lishe anayefanya biashara zake  Manispaa ya Iringa.

Mwananchin pia limezungumza na wafanyabiashara wa masoko mbalimbali mkoani Iringa wamekiri kupanda kwa bei ya mafuta, wakieleza kuwa dumu la lita 20 ambalo awali lilikuwa likiuzwa kati ya Sh60,000 na Sh70,000, sasa linauzwa Sh120,000.

Mfanyabiashara wa duka la jumla aliyejitambulisha kwa jina la Joseph Semtawa amesema hawezi kusema moja kwa moja ni kipi kimechangia kupanda kwa bei hizo.

“Kuna kamchezo sasa hivi kanafanyika hasa kwenye mafuta ya kula, mtu anaweza kuamka tu asubuhi akaamua kupandisha bei hasa wale wauzaji wa maduka ambayo yako nje ya mji,” amesema mfanyabiashara huyo.

Lakini amesema kingine kinachochangia ni gharama za ununuzi kwa wafanyabiashara wa rejareja.

“Pamoja na kupanda kwa gharama za ununuzi, hata wateja wetu wa rejareja wanalalamika kuwa bei zimepanda mno. Biashara imekuwa ngumu kwa sababu idadi ya wanunuzi imepungua, na hatujui wanatumia mbadala gani,” amesema Joseph ambaye ni muuzaji katika soko la Semtema katika Manispaa ya Iringa.

Related Posts