Dodoma. Licha ya kutumika kutibu na kuchunguza maradhi kwenye mwili wa binadamu, mionzi ya X-Rays na Gama Rays ambayo haijadhibitiwa inaweza kusababisha maradhi kama saratani na kifo endapo itamfikia mtu kwa nje.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya nguvu za Atomu Tanzania (TAEC), Profesa Najat Mohammed, jijini Dodoma, wakati wa mahojiano na Mwananchi kuhusu masuala ya mionzi na udhibiti wake.
Amesema Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania ina majukumu mawili makubwa ambayo ni kudhibiti matumizi ya mionzi yote, inayotokana na nyuklia na ile isiyotokana na nyuklia.
Pia, amesema inafanya kazi ya kuhamasisha matumizi ya mionzi katika nyanja mbalimbali kwa sababu mionzi ina faida na pia ina madhara, kwa hiyo madhara yanadhibitiwa na faida inahamasishwa kwa ajili ya matumizi hapa nchini.
“Mionzi hapa nchini inatumika sana kwenye kutibu na kutambua maradhi ya saratani pamoja na maradhi mbalimbali kwa kutumia X-Ray na tunajua X-Ray zote zinatumika hospitalini kwa ajili ya kuangalia matatizo mwilini.
“Kuna mionzi inayotumika kutibu saratani katika hospitali za Ocean Road na Bugando kwa sasa, lakini pia, mionzi inatumika kwenye usalama hasa kwenye kukagua mizigo wakati wa safari au kama kuna mashaka msafiri ana vitu vya ncha kali, bunduki na vitu kama hivyo,” amesema.
Ameongeza kuwa mionzi katika nyanja za kilimo hutumika kutengenezea mbegu zenye ubora, kilimo na mifugo na kwenye uzalishaji wa mbegu za wanyama kama vile ng’ombe, kupunguza wadudu waharibifu kwa wanyama na kwenye mazao.
Vilevile, amesema mionzi inatumika kwenye ujenzi wa barabara ili kuangalia ujazo wa udongo, kwenye viwanda vya maji na soda kwa ajili ya kuangalia ujazo, kwa hiyo ina matumizi mengi.
Profesa Mohamed amebainisha madhara endapo mionzi hiyo itamwangukia binadamu kwa nje inaingia moja kwa moja ndani ya mwili ambako na ina tabia ya kuua chembechembe hai kwenye mwili wa binadamu, jambo ambalo ni hatari.
“Ikiwa viasili vya mionzi vikichanganyika na chakula au hewa, vikaingia ndani ya mwili wa binadamu, vile vyanzo ambavyo vinatoa ile mionzi pia vinaweza vikasababisha madhara makubwa hata kuua au kusababisha kansa kwa siku za usoni,” amesema.