KIUNGO mshambuliaji wa KMC, Msomalia Ibrahim Elias ‘Mao’ ameanza mazoezi na kikosi hicho kinachojiandaa na mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam utakaopigwa Februari 6, baada ya kukaa nje ya uwanja kwa takriban miezi miwili.
Nyota huyo amerejea baada ya kusumbuliwa na majeraha ya misuli yaliyomfanya kukosekana ndani ya kikosi hicho tangu mara ya mwisho alipocheza mchezo wa Ligi Kuu waliopoteza mabao 2-0, dhidi ya Tabora United, mechi ikipigwa Novemba 29, 2024.
Akizungumza na Mwanaspoti kocha mkuu wa timu hiyo, Kally Ongala alisema ni habari njema kuona wachezaji wote wako katika hali nzuri kiafya, kwa sababu inaongeza morali ya upambanaji hususani kutokana na ugumu wa michezo iliyopo mbele yao.
“Kila mmoja wetu yupo tayari kwa ajili ya kuipambania timu raundi hii ya pili ambayo ni ngumu zaidi kutokana na ushindani uliopo, nafurahia kuona wachezaji wote wakizidi kuonyesha utayari wao kwa maana ya kimwili na kiakili mazoezini pia.”
Awali, nyota huyo aliripotiwa kuondoka kikosini baada ya aliyekuwa kocha wa kikosi hicho, Abdihamid Moallin kujiunga na Yanga, ingawa taarifa hizo zilikanushwa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa KMC, Daniel Mwakasungula.
Mchezaji huyo aliyejiunga na KMC msimu wa 2023-2024 akitokea Kibra United ya Kenya, msimu huu amefunga bao moja la Ligi Kuu Bara wakati timu hiyo ilipotoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Coastal Union, Agosti 29, 2024.
Msimu wake wa kwanza alimaliza na mabao matatu ya Ligi, ingawa safari hii ameanza kwa kuandamwa na majeraha, huku pia akionyeshwa kadi nyekundu walipochapwa mabao 3-1, dhidi ya Fountain Gate Oktoba 21.