Hamas yawaachia mateka watatu wa Israel, Wapalestina 183 nao huru

Gaza. Wapiganaji wa kundi la Hamas wamewaachia mateka watatu wa Israel waliokuwa wanawashikilia tangu uvamizi uliofanyika Oktoba 7, 2023.

Katika makubaliano kati ya pande hizo, Serikali ya Israel imewaachia wafungwa wa kipalestina 183. Wafungwa hao ni waliokuwa wakitumikia vifungo mbalimbali kwenye magereza ya Israel ikiwemo adhabu ya kifo na kifungo cha maisha jela.

Mabadilishano hayo ni ya mara ya tatu tangu pande hizo zikubaliane kusitisha mapigano na kuridhia kuwaachia mateka na wafungwa wa kila pande ambapo hadi sasa mateka 15 wa Israel wamerejeshwa kuungana na familia zao huku Wapalestina zaidi ya 350 wakiachiwa huru.

Al Jazeera imeripoti kuwa miongoni mwa mateka wa Israel waliokuwa Gaza walioachiwa leo Jumamosi Februari Mosi, 2025, ni raia wa Israel mwenye asili ya Ufaransa, Ofer Kalderon na raia wa Israeli ambao wote wamekabidhiwa kwa maofisa wa Msalaba Mwekundu mjini Khan Younis.

Baada ya saa moja kupita, Hamas pia imemuachia raia wa Israel mwenye asili ya Marekani, Keith Siegel ambaye amekabidhiwa kwa maofisa wa Msalaba Mwekundu waliokuwa eneo la Kaskazini mwa Gaza nchini humo.

Wafungwa 73 kati ya 183 wa Palestina walikuwa wakitumikia adhabu ya kifungo cha maisha katika magereza mbalimbali nchini Israel.

Tayari basi la kwanza lililobeba wapalestina 32 kutoka gereza la Ofer nchini Israel limewasili mjini Ramallah, ukanda wa Magharibi mwa Gaza huku wakipokewa na mamia ya raia waliokuwa wanawasubiria eneo hilo.

Miongoni mwa walioachiwa ni wazee wa Kipalestina waliokuwa kifungoni kwa muda mrefu nchini Israel kutokana na mzozo wa pande hizo ambao umedumu kwa karibia nusu karne, wengine walikuwa kwenye viti vya kusukuma.

Mbali na hao, Wapalestina 111 kati ya 183 walioachiwa leo walichukuliwa na majeshi ya Israel baada ya shambulizi la Oktoba 7, 2023. Baada ya kuachiwa, saba kati yao watapelekwa uhamishoni nchini Misri.

Inakadiriwa kuwa kuna Wapalestina takriban 4,500 katika magereza ya Israel wakitumikia vifungo mbalimbali wakishikiliwa katika kile kinachoitwa ni vifungo vya kiutawala, ambavyo vinawazuia kushtakiwa badala yake kuamriwa kutumia kifungo jela bila kushtakiwa.

Wakati mabadilishano hayo yakifanyika, Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema Wapalestina takriban 50 wako kwenye uhitaji wa hali ya juu wa kupatiwa matibabu nje ya nchi hiyo na wanatarajiwa kuvushwa kupitia mpaka wa Rafah kuhudhuria matibabu hayo.

Pia, Jeshi la Israel (IDF) linashutumiwa kutekeleza shambulizi kwa kutumia boti iliyokuwa ikipita baharini na kurusha risasi karibia na Kambi ya Wakimbizi ya Nuseirat Gaza nchini humo na kusababisha kifo cha mvuvi katika eneo hilo.

Pia, IDF inadaiwa kuwaua watu wawili eneo la Ukanda wa Magharibi mwa Gaza katika kambi ya wakimbizi ya Jenin, siku moja tangu jeshi hilo litekeleze mauaji ya wengine 10 katika Mji wa Tammum nchini humo.

Uvamizi wa Jeshi la Israel eneo Gaza usababisha vifo vya raia wa Palestina zaidi ya 47,460 na kujeruhi 111,580 tangu Oktoba 7, 2023. Wakati huo Waisrael 1,139 waliuawa huku zaidi ya 200 wakichukuliwa mateka na Hamas.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika.

Related Posts