Jamii yakosa imani usikilizwaji kesi kwa njia ya mtandao, elimu yahitajika

Geita. Wadau wa Mahakama Mkoa wa Geita wamesema licha ya uendeshaji wa Mahakama kwa njia ya mfumo wa teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) kuwa na tija, bado jamii ina uelewa mdogo kuhusu matumizi ya mfumo huo.

Kutokana na uelewa huo mdogo wa jamii, wadau hao wameiomba Mahakama kutoa elimu zaidi ili kujenga imani hususan kwa watuhumiwa ambao kesi zao zinasikilizwa kwa njia ya mtandao.

Hayo yamebainishwa na wadau wa Mahakama wakiwemo mawakili wa Serikali, wale wa kujitegemea pamoja na Magereza wakati wa mdahalo wa kuangazia utendaji kazi wa mwaka mmoja tangu kuanzishwa kwa Mahakama Kuu mkoani Geita.

Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwendesha Mashtaka mkoani hapa, Godfrey Odupoy amesema pamoja na Mahakama kufanikiwa kuhama kwenye matumzi ya karatasi kwa asilimia 100 bado wadau wakiwemo watuhumiwa, hawana imani kama kesi inayosikilizwa kwa njia ya mtandao itatendewa haki.

“Tunasema wadau wa Mahakama ni wale wote wenye uhitaji wa Mahakama tukianza na jamii inayotuzunguka, polisi, mawakili hawa wote hawana uelewa wa kutosha kuhusu Tehema tunajua kuanzishwa kwa Mahakama imeleta matumizi ya Tehama bado tunahitaji elimu ili tuendane na kasi yenu,” amesema Odupoy.

Kuhusu matumizi ya Mahakama, mtandao amesema wapo watuhumiwa ambao hawaamini kamaa kesi ikisikilizwa kwa njia ya mtandao (video) watatendewa haki sawa na yule aliyeingia kwenye chumba cha Mahakama na kuonana na jaji ana kwa ana.

“Wengine ukiwaambia kutokana na sababu hizi utasikilizwa kwa njia ya mtandao wanaona kama wamenyimwa haki yao ya kusikilizwa na pengine haamini kama mahakama mtandao ni mahakama kama ile ya kufika kwenye chumba cha mahakama na kumuona jaji tunaomba mtoe elimu kuhusu Mahakama mtandao ili jamii ipate uelewa na kujua hadhi ya Mahakama mtandao ni sawa na kufika mahakamani,” amesema.

Amesema changamoto nyingine ni kutopatikana nyaraka kwenye mfumo, amesema pamoja na hukumu kuwekwa kwenye mfumo, lakini zipo baadhi ya nyaraka ambazo haziruhusu mdau kuzipata kwenye mtandao.

Kauli hiyo imeungwa mkono na wakili wa kujitegemea, Erick Lutehanga na kuiomba Mahakama kutoa elimu zaiid ili kujenga uelewa kwa wananchi juu ya matumizi ya Tehama.

Wakizungumzia mwaka mmoja tangu kuanzishwa kwa Mahakama kuu Geita wamesema imesaidia kupunguza gharama za uendeshaji wa kesi kwa kuwa awali kesi hizo zilikuwa zikisikilizwa mkoani Mwanza.

“Imepunguza gharama nyingi ulikua ukiandaa kesi unamwekea na gharama za usajili lakini sasa hiyo haipo, tulikua tukiandaa mashauri lazima uende mahakamani ukaandikishe lakini sasa hivi kila kitu unafanya kwa njia ya mtandao,” amesema.

Akizungumza katika mdahalo wa mwaka mmoja tangu kuanzishwa kwa Mahakama Kuu Geita, Jaji mfawidhi wa Mahakama hiyo, Kelvin Mhina amezitaka taasisi nyingine ikiwemo Mahakama ya ardhi kuhamia kwenye mfumo wa Tehama ili kuokoa muda na fedha.

Jaji Mhina amesema mfumo wa Tehama umesaidia kuimarisha usimamizi katika utoaji haki, kurahisisha ukaguzi na kufuatilia mrundikano wa kesi, hivyo kuwa rahisi kushughulikia kesi zinazosubiriwa.

Amesema uwepo wa Mahakama mtandao umepunguza gharama kwa mashahidi, mawakili na washtakiwa kusafiri hadi mahakamani, pia, imesaidia kupatikana kwa taarifa za mashauri kwa urahisi na kusaidia utunzaji bora wa majalada.

“Kwa sasa hakuna kupotea kwa jalada na vielelezo au kuambiwa mwenendo hausomeki mambo haya hayapo tena. Takwimu inarahisha sana na imeleta ufanisi kufanya kazi kwa haraka zaiidi,” amesema Jaji Mhina.

Related Posts