Njombe. Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe wamependekeza kupunguzwa kwa bei ya ushuru ya mazao ili kuepusha wimbi la wafanyabiashara wadanganyifu kufanya utoroshaji wa mazao, jambo linalotajwa kuisababishia hasara kwa halmashauri hiyo.
Kauli hiyo wameitoa leo Februari Mosi, 2025 katika baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe robo ya pili lililofanyika huko Wilayani Wanging’ombe mkoani Njombe.
Wamesema ushuru wa mazao upo juu ukilinganisha na halmashauri zingine za mkoa huo, hivyo inasababisha wafanyabiashara kutorosha mazao na kwenda kukata vibali halmashauri zingine ili kupunguza gharama.
Diwani wa Itulahumba, Thobias Nkane amesema ushuru wa mazao ya mahindi kwa gunia la kilo 100 ni Sh1,500 wakati halmashauri zingine ujazo huo huo ni Sh1,000 hivyo kusababisha changamoto kwa halmashauri kushindwa kukusanya mapato kwa wingi.
“Wenzetu kwenye halmashauri zingine ushuru wa mahindi wanalipa Sh1,000 kwa gunia hii inafanya wafanyabiashara kuhamia halmashauri zingine,” amesema Nkane.
Kwa upande wa Diwani wa Mdandu, Annaupendo Gombela amesema ushuru wa 1500 kwa gunia unakwenda kuwa mzigo kwa wakulima wa halmashauri hiyo kutokana na kukosa masoko ya uhakika.
“Endapo bei hiyo itashuka itakuwa kivutio kwa wanunuzi wengi wa mazao kuja kununua ndani ya halmashauri na wakulima watapata kipato” amesema Gombela.
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe Onesmo Lyandala amesema katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka wa fedha 2024/2025, halmashauri hiyo imekusanya Sh3.1 bilioni kutoka vyanzo halisi vya ndani.
Amesema kuhusu ushuru wa mazao tayari halmashauri hiyo kwa kuona changamoto ipo kwenye mpango wa kupunguza bei ya ushuru kutoka Sh1,500 hadi 1,000 kwa gunia la mahindi la kilo 100 na la viazi mviringo kuvutia wanunuzi na kuongeza mapato ya halmashauri.