Kiev. Jeshi la Russia limefanya mashambulizi mfululizo usiku wa kuamkia leo yaliyolenga miundombinu ya gesi iliyopo maeneo mbalimbali nchini Ukraine, Wizara ya Ulinzi ya Russia imesema.
Shirika la Associated Press limeripoti kuwa katika taarifa yake kwa umma leo Jumamosi, Februari Mosi, 2025, wizara hiyo imesema mashambulizi hayo yamefanyika usiku kucha maeneo mbalimbali ya mkoa wa Poltava na Zaporozhye nchini Ukraine.
Taarifa ya wizara hiyo pia imesema mashambulizi hayo yalilenga kuharibu miundombinu ya kijeshi na ile ya uzalishaji wa gesi nchini Ukraine.
“Malengo ya mashambulizi yetu yametimia. Maeneo yote tuliyotalenga tumefanikiwa kuyapiga, tatatoa majibu,” imesema taarifa ya wizara hiyo bila kuanika madhara yaliyosababishwa na mashambulizi hayo.
Tayari maofisa nchini Ukraine wamethibitisha kutekelezwa mashambulizi ya Russia maeneo mbalimbali nchini humo, huku ofisi ya mkoa wa Poltava ikitangaza kuwa kutakuwa na giza kuanzia leo.
Rais Volodymyr Zelenskyy, pia, amesema mashambulizi hayo yameleta uharibifu katika mkoa wa Odessa, Sumy, Kharkov, Khmelnytsky, na Kiev, huku akidokeza kuwa yalijumuisha matumizi ya makombora, ndege zisizo na rubani na mabomu ya kurusha kutokea angani.
Amesema watu watatu wamefariki kutokana na mashambulizi hayo mkoani Poltava, wawili mkoani Sumy, na mmoja mkoani Kharkov, huku mamia wakijerujiwa.
Russia imekuwa ikiendesha mashambulizi mfululizo yanayolenga kuharibu miundombinu ya nishati ikiwemo ya uzalishaji wa gesi nchini Ukraine, huku ikisisitiza kuwa malengo ya mashambulizi hayo siyo raia.
Moscow, pia, imesema mashambulizi hayo mbali na kulenga kulipiza mashambulizi ya Kiev kwenye miundombinu ya mafuta na majengo ya makazi nchini mwake, yanalenga kulipiza kisasi kufuatia tukio la wanajeshi wa Ukraine kuvamia, kubaka na kuwaua raia wa Russia katika kijiji kilichopo mkoani Kursk.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika.