BEKI wa Dodoma Jiji, Mkongomani Heritier Lulihoshi amesema licha ya ujio wa mabeki wapya kikosini, Mukrim Issa ‘Miranda’ aliyetokea Coastal Union, na Abdi Banda aliyesajiliwa kutokea Baroka FC ya Afrika Kusini, hana hofu ya kuwania namba.
Akizungumza na Mwanaspoti, Lulihoshi alisema ujio wa mabeki hao unampa changamoto zaidi ya kupambana kila atakapopewa nafasi ya kucheza, huku akiweka wazi ubora wao utaongeza motisha ya kukipambania kikosi hicho ili kifanye pia vizuri.
“Niko tayari kwa ajili ya changamoto zozote zile, nawakaribisha kwa moyo mkunjufu kwa ajili ya kuipambania timu iweze kufanya vizuri, ujio wao hapa haujanitisha isipokuwa nimefurahia kwa sababu watanifanya niongeze juhudi zaidi uwanjani,” alisema.
Beki huyo wa kati mwenye uwezo wa kucheza upande wa kulia au kushoto kwa ufasaha, alisema haogopi changamoto zozote kwa sasa katika maisha yake, huku akiweka wazi usajili mpya katika dirisha dogo utasaidia kikosi hicho kufanya vizuri zaidi.
Hata hivyo, licha ya nyota huyo kuzungumza hayo ila atakuwa na kazi ya kupigania nafasi ya kucheza mara kwa mara, kwani hadi sasa amecheza michezo saba tu ya Ligi Kuu Bara kati 16 iliyocheza Dodoma Jiji, huku akifunga mabao mawili kikosini.
Nyota huyo amejiunga na kikosi hicho msimu huu akitokea Tabora United ambapo mabao hayo mawili aliyafunga katika mchezo na JKT Tanzania ambao Dodoma Jiji ilishinda bao 1-0, Oktoba 26, 2024 na ushindi pia wa 3-1 dhidi ya Mashujaa Desemba 28, 2024.