Mtayarishaji na mzalishaji wa video na filamu mwenye uzoefu wa muda mrefu nchini Tanzania, Mussa Ally, maarufu kama Kaka Mussa, ni Mtanzania pekee aliyepata bahati ya kushiriki katika uaandaaji wa filamu ya Hollywood Marekani ya MUFASA: The Lion King, ambayo kwa sasa imeliteka soko la filamu duniani.
Akielezea ushiriki wake katika mahojiano na Global TV Online, Mussa alisema kuwa alikuwa miongoni mwa kikosi cha wapiga picha waliotumia drone kurekodi mandhari mbalimbali nchini Tanzania. Uamuzi wa kurekodi nchini ulitokana na kuvutiwa kwa timu ya waandaaji kutoka Walt Disney na uzuri wa vivutio vya Tanzania, hivyo wakaamua kuweka kambi nchini Tanzania na kurekodi baadhi ya sehemu za filamu hiyo.
“Sehemu zilizotumika kurekodi baadhi ya matukio katika filamu hii zinaonyesha uzuri wa kipekee wa Tanzania, ambazo ni Iringa – Isimila Pillars, Ziwa Natron, na Ngorongoro Crater.
“Mandhari haya ya kipekee yanatoa mchango mkubwa kwa hadithi hii ya kihistoria, huku yakidhihirisha uzuri wa asili wa nchi yetu kwa ulimwengu mzima,” alisema Mussa.
Aidha, aliongeza kuwa ni heshima kubwa kwake kuwakilisha Tanzania katika mradi huu unaoonyesha utajiri wa utamaduni na mazingira ya nchi yetu. Pia, alisema kuwa waandaaji wa filamu hiyo waliamua kurekodi Tanzania baada ya kutazama filamu ya The Royal Tour, iliyoongozwa na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
Mufasa: The Lion King ni filamu ya katuni inayohusu maisha ya wanyama wa Afrika, iliyotayarishwa na Walt Disney Feature Animation. Filamu hiyo imekuwa miongoni mwa filamu zilizovunja rekodi za mauzo tangu ilipozinduliwa rasmi Desemba 2024 nchini Marekani na kuonyeshwa kwenye majumba ya sinema na majukwaa ya kidijitali duniani kote.