Moshi. Mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali, imesababisha maafa katika Kitongoji cha Zilipendwa Kata ya Makuyuni, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro baada ya nyumba kuezuliwa paa na kusababisha kaya kadhaa kukosa mahala pa kuishi.
Pia miundombinu ya umeme imeharibiwa baada ya miti kuangukia nguzo na nyaya za umeme huku baadhi ya barabara miti ikiwa imeanguka nyumba na nyingine zikiharibiwa na maji yaliyotokana na mvua hiyo iliyonyesha kwa dakika 45 jana Ijumaa Januari 31, 2025.
Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava akizungumza na Mwananchi leo Jumamosi Februari Mosi, 2025, amesema kutokana na hali ya hewa, ametoa rai kwa wananchi wanaoishi maeneo hatarishi kuchukua tahadhari kabla ya madhara makubwa hayajawafika.
“Jana ilinyesha mvua ambayo iliambatana na upepo mkali, ilileta madhara kwenye nyumba ambayo ilikuwa na wapangaji wanne na upepo uliezua paa na kusababisha familia nne kukosa mahala pa kuishi,” amesema Mnzava.
Ameongeza; “Madhara mengine yaliyojitokeza kutokana na upepo ule ambao ulikuwa ni mkali, uliangusha baadhi ya miti barabarani lakini pia nguzo za umeme zilianguka kutokana na miti kuziangukia.”
Aidha, amesema jitihada mbalimbali zimefanyika ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wananchi waliokumbwa na maafa hayo wanapata mahali pa kuishi pamoja na kuondoa miti iliyokuwa imeanguka barabarani.
“Jitihada ambazo zinaendelea ni kukata miti iliyoangukia barabarani ili kufungua barabara hizo lakini pia wataalamu wa Tanesco wapo maeneo hayo kuhakikisha wanarudisha huduma ya umeme,” amesema Mnzava.
Naye Mwenyekiti wa Kitongoji cha Zilipendwa, Kened Molel amesema mvua hiyo ilianza kunyesha saa 9 alasiri jana na ilichukua dakika 45 na kusababisha madhara hayo.
“Mvua hii imesababisha madhara mbalimbali ikiwemo nyumba kuezuliwa paa na kusababisha kaya nne kukosa makazi, uharibifu mkubwa wa miundombinu ya umeme na barabara kutokana na miti mingi kuanguka,” amesema Molel.
Mwenyekiti huyo ametoa wito kwa wananchi kuchukua taadhari katika kipindi hiki cha mvua zinazoendea kunyesha na kuhakikisha wanaepuka kukaa chini ya miti wakati wa mvua na kushika nyaya za umeme zilizoanguka.
Mmoja wa waathirika wa maafa hayo, Anjela Lyimo amesema wamepata hasara kubwa kutokana na mvua hiyo kuezua paa na maji kuharibu vitu vilivyokuwepo ndani.
“Nilikuwa msibani nikaitwa nikaja nikakuta nyumba imeezuliwa paa, maji yameingia ndani hakufai, bati zimetupwa mbali na kwa sasa hakuna chochote kinachoweza kufanyika,” amesema.