Dodoma. Baada ya mchakato wa muda mrefu hatimaye Rais Samia Suluhu Hassan amezindua Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 toleo la mwaka 2023, huku akitaja mambo matatu yalimsukuma kutaka kufanyika mapitio ya sera baada ya kuingia madarakani.
Akizungumza jana jijini Dodoma alisema licha ya kwamba ndiye aliagiza kufanyika kwa mapitio hayo, kazi kubwa ilishafanywa na watangulizi wake na ndiyo iliyomfanya kuona kuna haja ya kufanyika kwa mapitio haya ili elimu inayotolewa kuendana na kasi ya maendeleo ya teknolojia.
Alisema, “Nimesimama kwa fahari juu ya mabega ya walionitangulia kwa sababu wao ndiyo walijengea jukwaa linalonifanya mimi nione mbele. Huko mbele ninaona dunia inayobadilika kwa kasi sana, mabadiliko ambayo ni sawa na upepo unaovuma kwa kasi unaweza kutupepea au kutupeperusha.
Upepo huo ni kasi ya mabadiliko ya teknolojia ya habari na mawasiliano katika kujifunza au kuiharibu jamii, hivyo kutokana na upepo huo aliona ni lazima tuwe na maandalizi ya kufanya upepo utupee na usitupeperushe. Mbele yetu pia ninaona mahitaji makubwa ya ajira kwa vijana ambayo yataendelea kuongezeka mbele ya safari kwa sababu kubwa tatu,” alisema.
Alizitaja sababu hizo ni ni kasi ya mabadiliko ya kiteknolojia itakayosababisha baadhi ya kada nyingine kukua na nyingine kutoweka.
Sababu ya pili ni utandawazi ambao unatoa fursa ya bidhaa na huduma kutoka sehemu moja ya dunia kwenda nyingine kwa njia rahisi na bila kulazimika kuwa na msimamizi.
Pia, ongezeko la idadi ya watu lisiloendana na kasi ya ukuaji wa uchumi ni sababu nyingine iliyomsukuma Rais Samia kutaka mapitio hayo ya sera na mitaa.
“Ukuaji wa asilimia 3.2 kwa mwaka inakadiriwa kwamba ifikapo mwaka 2044 idadi ya watu hapa nchini itakuwa milioni 123 na hivyo kuongeza uhitaji wa kazi na ajira kwa vijana, hivyo ninachokiona huko mbele kinatufanya tuwe na maandalizi ya kutosha kwa kuinua ubora wa elimu yetu.
Kwa kutoa elimu bora zaidi ya kisasa na kuandaa vizuri zaidi vijana wetu ili waweze kumudu stadi muhimu zitakazowawezesha kuajiriwa au kujiajiri. Elimu itakayowafanya vijana wetu waweze kushindana kikanda na kimataifa, kuwajengea ujasiri kuweza kujiamini. Kwa kufanya hivyo tutakuwa tunaandaa mazingira mazuri ya upepo kuwapepea vijana wetu badala ya kuwapeperusha.
Rais Samia amesema miongoni mwa mambo muhimu yatakayoangaliwa ili kufanikisha utekelezaji wa sera na mitaala hiyo ni mapitio ya maslahi ya kada ya ualimu nchini.
Hatua hiyo inalenga kuipa hadhi inayostahili kada hiyo ambayo ndio mama wa taaluma zote akieleza kuwa mwalimu ndiyo kiungo wa utekelezaji wa sera na mitaala.
“Kwa maoni yangu ndio kiongozi wa elimu, hivyo katika maboresho haya lazima mwalimu awe katikati ya mduara wa maboresho yaliyofanyika na kusisitiza kuwa Serikali itaendelea kuajiri walimu wenye sifa na kuwapa mafunzo stahiki ili waendane na muelekeo wa sera hii,” amesema.
“Aidha, tutapitia upya maslahi ya kada ya walimu nchini ili kuipa hadhi inayostahili kama mama wa taaluma zote duniani,”amesema.
Katika kuhakikisha rasilimali fedha zinapatikana za kutosha Rais Samia aliziagiza Wizara ya Fedha, Wizara ya Mipango na Uwekezaji, Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Mitaa (Tamisemi) kuwezesha na kusimamia kikamilifu utekelezaji wa sera na mitalaa mpya ili kuleta matokeo yaliyokusudiwa.
“Sera ni nzuri, yaliyolengwa ndani ni makubwa Serikali peke yake hatutaweza na kutegema wahisani peke yao hatutaweza dunia inabadilika kila nchi ina changamoto zake lakini tukienda na sekta binafsi tunaweza kufanya vizuri. Kwahyo tufanye maandalizi ya kwenda pamoja na sekta binafsi,” alisema Rais Samia.
Rais Samia alisema elimu itakuwa ya lazima kutoka miaka saba na kuwa 10 na kwamba ilitokana na wanafunzi kumaliza elimu ya msingi wakiwa na umri wa miaka 13 na hivyo kukosa sifa ya kuajiriwa na kujiajiri huku hawana elimu ya ufundi na kwa sasa kupitia sera hiyo itamuwezesha kijana kuingia kwenye uzalishaji.
Aidha, alisema sera hiyo inajibu hoja ya muda mrefu ya kuweka mfumo wa kutoa na kurasimisha ujuzi unaopatikana nje ya mfumo rasmi wa elimu na mafunzo uliopo.
Alisema somo la ujasirimali litakuwa la lazima kwa kila mwanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha nne ili kumpa misingi ya biashara na watajifunza lugha ya kiingireza, kichina, kifaransa na kiarabu kwa kuwa ndizo zinazoendesha uchumi duniani.
Akimkaribisha Rais Samia, Makamu wa Rais Dk Philip Mpango amesema sera hiyo itawezesha kubadilisha mfumo wa elimu ili kuzalisha nguvu kazi yenye ujuzi wa teknolojia.
Alisema ziko tafiti kama zinaonyesha kama sera ya elimu haiakisi mabadiliko ya teknolojia kunakuwa na ukosefu mkubwa wa ajira kwa sababu nguvu kazi isiyokuwa na ujuzi inazalishwa kwa wingi kuzidi mahitaji.
“Na hilo nalo linapelekea tofauti kubwa ya vipato ambapo nguvu kazi yenye ujuzi hunufaika zaidi ama maradufu kwa hiyo mheshimiwa Rais Sera hii itatuwezesha kubadili mfumo wetu wa elimu ili tuweze kuzalisha nguvu kazi yenye uwezo wa kumudu mabadiliko ya teknolojia,”amesema.
Akitoa ufafanuzi kuhusu sera hiyo Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda alisema asilimia kubwa ya mambo yaliyokuwa katika sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 ambayo ilizinduliwa mwaka 2015, hayakutekelezwa.
Alisema asilimia kubwa ya mambo yaliyokuwa ndani ya sera hiyo yalikuwa ni mazuri, lakini wakati inazinduliwa Rais Jakaya Kikwete alikuwa anamaliza muda wa uongozi wake na kulikuwa na utekelezaji wa miradi mingi ambayo ilihitaji fedha nyingi.
“Wakati tunapitia (sera), tulijiuliza sana, mheshimiwa Ndalichako (aliyekuwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako), nadhani unakumbuka. Tulikuta mitaala inafanyiwa kazi lakini kwa elimu ya msingi ya miaka 7 na sababu sio Ndalichako,”amesema.
“SGR (Reli ya Mwendo Kasi) hiyo, bwawa la Mwalimu Nyerere hilo, vyote ni gharama kubwa na vinahitaji fedha nyingi, tuna vipaumbele vingi na vyote ni muhimu,”amesema.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Ushirikiano wa Elimu Duniani (GPE), Rais Mstaafu Jakaya Kikwete amesema bodi ya shirika hilo kuanzia mwaka 2013 hadi sasa imechangia miradi ya maendeleo ya elimu yenye thamani ya Sh518 bilioni.
Kikwete alisema tayari mazungumzo ya awali katika awamu ya tatu yameanza kati ya Serikali na GPE ambapo Dola za Milioni 88.56 zimeshatengwa na ziko nyingine Dola Milioni 50 ziko tayari kujumuishwa kwenye mpango huo.
Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson, alisema katika kuendana na mabadiliko ya teknolojia dunia na kuwapo na ubora wa elimu inayotolewa Bunge lipo tayari kufanya marekebisho ya sheria zitakazoonekana haziendani na sera hiyo mpya.
Aidha, ameshauri baada ya kuzinduliwa kwa sera ni muhimu kuangalia masomo ambayo hayahitajiki tena kwa kuwa watoto wanauwezo wa kufahamu bila kufundishwa.
Naye Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Leila Mohamed Musa alisema kwa upande wa Zanzibar mapitio ya mtaala wa mafunzo ya amali yameanza ili kwenda sambamba na mabadiliko ya sera na kwamba matayarisho ya mafunzo kwa ajili ya walimu yamekamilika na kuanza kutolewa.
“Sera inazungumza kuanzishwa kwa mkondo wa elimu ya amali ambao unaenda kutoa fura zaidi kwa Serikali kuandaa wataalam watakaokwenda kufanya kazi katika sekta ya utalii kwa umahiri mkubwa, masuala ya bahari na uvuvi,” amesema.