NI sahihi kusema Simba imepishana na gari la mshahara baada ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf) kupitisha uamuzi wa kuruhusu klabu kuwatumia wachezaji ambao wameshatumikia klabu nyingine kwenye mashindano ya klabu Afrika, uamuzi ambao unaanza msimu huu.
Hiyo ni kutokana na Simba kutokuwa na uwezo wa kumsajili mchezaji katika kipindi hiki kutokana na kufungwa kwa dirisha la ndani la usajili, linalomfanya mchezaji husika apate leseni ya kushiriki mashindano ya ndani ambayo ndio inamwezesha kupata leseni ya kushiriki mashindano ya klabu Afrika kwa mujibu wa kanuni za mashindano ya klabu Afrika.
Kwa mujibu wa kanuni ya 5(2), ya Ligi ya Mabingwa Afrika, mchezaji ili acheza mashindano ya klabu Afrika anapaswa kuwa na leseni ya kushiriki mashindano ya ndani.
“Awe na leseni ya klabu yake iliyotolewa na chama cha soka cha nchi husika na awe anakidhi vigezo vya kucheza mashindano ya ndani ya nchi ambayo klabu inayoshiriki ligi ya mabingwa ipo,” inafafanua kanuni hiyo.
Taarifa iliyotolewa na Caf juzi imefafanua kamati yake ya utendaji imeamua klabu zinaweza kuwasajili na kuwatumia wachezaji waliotumika na klabu nyingine kwenye mashindano yake ndani ya msimu mmoja.
Awali kanuni zilikuwa zinazuia mchezaji ambaye ameshatumika na timu moja kwenye mashindano ya klabu Afrika kutumikia timu nyingine katika msimu huo huo mfano ni kanuni ya nne ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu.
“Ndani ya mwaka mmoja, mchezaji kimsingi atakuwa halali kuchezea klabu moja hiyo hiyo katika mashindano ya klabu ya Caf. Hata hivyo, kwa mchezaji ambaye amesajiliwa katika orodha ya klabu ambaye hajapangwa katika mchezo wowote wa mashindano ya klabu ataruhusiwa kuchezea klabu nyingine inayoshiriki mashindano ya klabu Afrika ndani ya mwaka mmoja ilimradi iwe imetimiza matakwa ya kikanuni.”
“Mchezaji aliyepangwa ni miongoni mwa 11 wanaoanza katika mechi au ambaye amepishana na mmoja kati ya wachezaji walioanza katika kikosi cha kwanza. Mchezaji wa akiba aliye katika orodha ambaye hajashiriki kama ilivyofafanuliwa hapo juu, hatohesabika kama alipangwa,” inafafanua kanuni hiyo.
Kwa sasa zuio halitokuwepi kutokana na mabadiliko hayo ambayo Caf imeyafanya na kuyatangaza juzi.
“Shirikisho la Soka Afrika (Caf), leo (juzi) limebadilisha kanuni za usajili wa wachezaji za Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika, ili kuruhusu klabu za soka kusajili mchezaji, kwa ajili michuano hiyo ya CAF, ambaye ilishiriki katika mojawapo ya mashindano hayo, kwa klabu nyingine ya soka, ndani ya msimu huo wa soka.
“Kwa kubadilisha kanuni hizi za usajili wa wachezaji, Ligi ya Mabingwa ya Caf na kanuni za Kombe la Shirikisho la Caf sasa zinafanana na UEFA Champions League na kanuni za usajili wa Wachezaji wa UEFA Europa League.
“Marekebisho ya Kanuni hizi yatachangia ligi ya mabingwa wa Caf na kombe la shirikisho la Caf kuwa ya kuvutia na yenye mvuto kwa mashabiki wa soka, watazamaji wa TV na wadhamini na washirika barani Afrika na duniani kote.
“Mabadiliko haya yanaweza pia kuboresha ubora wa klabu za soka Afrika vinazoshiriki kombe la dunia la klabu la FIFA 2025 litakalofanyika Marekani mwezi Juni-Julai 2025. CAF pia ilichukua azimio la kuongeza muda wa mwisho wa usajili wa wachezaji wa ligi ya mabingwa ya Caf na kombe la shirikisho la Caf hadi 28 Februari 2025,” ilifafanua taarifa hiyo ya Caf juzi.
Wakati uamuzi huo ukitangaza huku Simba ikishindwa kunufaika kwa vile dirisha la ndani limefungwa, timu kutoka mataifa ya Kaskazini ambayo yanazungumza lugha ya Kiarabu hapana shaka zitapokea kwa mikono miwili uamuzi huo kwa vile madirisha yao ya usajili yapo wazi katika nchi zao.
Mfano wa timu zinazokenua ni Al Ahly ambayo sasa ina nafasi ya kuwatumia wachezaji wawili iliowanasa katika dirisha linaloendelea la usajili ambao ni Achraf Bencharki na Mahmoud Hassan ‘Trezeguet’.
Wakizungumzia uamuzi huo, wadau wa soka nchini wameipongeza Caf wakisema una tija.
“Ni Uamuzi mzuri sana ambao unafungua njia mpya katika usajili kwa klabu kuwa na wigo mpana muda wowote. Unakipa hadhi kipindi cha usajili wa dirisha dogo kuwa na umuhimu sawa na dirisha kubwa. Manufaa zaidi yataenda kwa wachezaji ambao timu zao zimekosa nafasi ya kuendelea ila wao wameonyesha vipaji vyao ili kuhamia timu nyingine zinazoendelea na mashindano.
“Pia kuwianisha na kwenda na wakati kwa kanuni zetu na za mashirikisho mengine nje ya Africa. Katika klabu manufaa yatakuwa zaidi kwa wenye nguvu na meno mengi ya kula chochote muda wowote sokoni,” alisema mkurugenzi wa zamani wa wanachama na mashabiki wa Simba, Hashim Mbaga.
Meneja Rasilimali Watu wa Singida Black Stars, Muhibu Kanu amesema uamuzi huo una faida kwa timu na wachezaji.
“Ni uamuzi mzuri hata kwa wachezaji unawasaidia. Naunga mkono hiyo hoja mchezaji anaposajiliwa kwenda klabu nyingine, malengo na mipango anayoikuta pale aendelee nayo pasipo kubanwa.
“Klabu pia inapomsajili haiwezi kukaa tena ikasubiri. Anapokuja anaongeza nguvu kwenye malengo ambayo klabu imejiwekea,” alisema Kanu.