Na Khadija Kalili, Michuzi TV
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Pwani imefanikisha kuongeza makusanyo Wilaya ya Kibiti Mkoani Pwani kwa kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2024.
“Tulifanya uzuiaji katika mfumo wa kukusanyaji wa mapato kwa kutumia POS mashine kwa kuongeza makusanyo kutoka 4,632,682.75 kwa wiki hadi Sh.Mil.12,089,760 ambapo kwa mwaka makusanyo yatakuwa MI.480,000,000.
Hayo yamesemwa leo tarehe 31 Januari 2025 na Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Pwani Alli Sadiki alipozungumza kwenye mkutano na Waandishi wa Habari uliofanyika ofisini kwake.
Amesema kuwa uzuiaji huo ulifanyika baada ya thathmini ya ukusanyaji wa mapato kwa kutumia mashine za POS kutoridhisha kwa kukusanya mapato kiasi kidogo kulingana na uwezo mkubwa wa kizuizi cha maliasili Kibiti.
Aidha amesema kuwa TAKUKURU ilisimamia ukusanyaji katika kituo hicho kuanzia Novemba 5 hadi 11 mwaka 2024 kwa masaa 24 nakukusanya Mil.12,089,760.
Kamanda Sadiki amesema baada ya kusimamia ukusanyaji wa fedha TAKUKURU imebaini kuwa baadhi ya wakusanya ushuru kuletewa fedha na wenye mizigo ili wasitozwe malipo ya ushuru wa Serikali, baadhi ya wenye magari yenye mizigo kuwasiliana na wakusanyaji ili wapite bila kukaguliwa na wasilipe mizigo waliyoibeba,baadhi ya magari wakati wa ukaguzi walikuwa wanafungua buti na kuweka fedha ya rushwa ili wakusanyaji wachukue na wasiendelee na ukaguzi na Kisha war Uhuru magari hayo kupita.
“Wakusanyaji wamepewa mwanya mkubwa wa kukadiria kiasi cha malipo cha kulipia katika mizigo inayopita,hivyo baadhi ya mizigo mikubwa imekuwa ikitozwa ushuru mdogo,baadhi ya bidhaa ambazo haziruhusiwi kusafirishwa zimekuwa zikipitishwa usiku na kutoa fedha ili wasichukuliwe hatua” amesema Kamanda Sadiki.
Wakati huohuo Kamanda Sadiki amesema kuwa katika kipindi tajwa TAKUKURU Pwani wamepokea jumla ya malalamiko 60 kati ya hayo malalamiko 37 yalihusu rushwa na taarifa hizo zimeshughulikiwa kwa mujibu wa sheria kwa kuanzisha uchunguzi ambao upo katika hatua mbalimbali za uchunguzi.
Taarifa 23 zilizobaki ambazo hazikuhusu rushwa zineshughulikiwa kwa njia ya uelimishaji,uzuiaji,ushauri na kuhamishiwa idaa nyingine.
Taarifa zilizopokelewa ni TAMISEMI 11,michezo1,utalii1,Polisi4,ardhi
10,maji1, Mahakama 2,binafsi3,Elimu8,Viwanda5 Ujenzi4,Afya4,Siasa2, maendeleo ya jamii 3 na ushirika1.
Aidha Kamanda Sadiki amesema kuwa TAKUKURU Pwani katika kipindi hiki imefanikiwa kufungua jumla ya kesi mpya 24 Mahakamani na kesi 13 washtakiwa wametiwa hatiani.
Akizungumza kuhusu mikakati ya TAKUKURU kuanzia Januari hadi Machi 2025 Kamanda Sadiki amesema kuwa wamejipanga kuendelea kutoa elimu kuhusu madhara ya rushwa katika uchaguzi mkuu kupitia semina, mikutano ya hadhara na vipindi vya redio ili kuwafikia wadau wote.
“Tutaendelea kufanyan udhibiti wa mapato ya serikali na usimamizi wa rasilimali kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo ,tutaendelea kupokea taarifa za vitendo vya rushwa kufanya uchunguzi na kufikisha watuhumiwa Mahakamani” amesema Kamanda Sadiki.