Kilombero. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wilaya ya Kilombero, mkoani Morogoro imesema kuwa hali ya ulipaji kodi katika wilaya hiyo ni mzuri, kwani wafanyabiashara wanalipa kodi kwa hiari na kwa wakati shuruti.
Hayo yamesemwa leo na Meneja wa TRA wilayani humo Wilfred Makamba wakati wa kikao kilichohusisha wafanyabiashara na watendaji wa mamlaka hiyo na kuongeza kuwa ushirikiano uliopo kati yao na wafanyabiashara ni mkubwa.
Amesema hali hiyo imesababisha msimu uliopita kufikia malengo yao ya ukusanyaji wa mapato na kwamba lengo la kikao hicho, ni kuwapa elimu na kukumbushana sheria zilizopo na pia kuwapongeza walipa kodi bora.
Meneja huyo amesema wameona kuna haja katika kukumbushana kufuata sheria, kwani vitu vingi vimebadilika katika mifumo na hii itasaidia kuwaletea huduma jirani zaidi wananchi.
Amesema elimu wanayowapa ni ile inayosema sheria inataka nini kwa wakati huo ikiwemo sheria ya kodi na jinsi ya kutoa risiti, makadirio ya kodi zao na ulipaji wa kodi kwa wakati.
Naye Mkuu wa wilaya ya Kilombero, Dunstan Kyobya ameipongeza TRA katika juhudi za ukusanyaji wa mapato katika wilaya hiyo na kutaka uhusiano uliopo uendelee ikiwamo kuitishwa mara kwa mara vikao baina ya TRA na wafanyabiashara.
Kyobya amewataka wafanyabiashara hao kuongeza fursa za kujipanua zaidi kibiashara kwa kuwekeza majengo ya kisasa ikiwemo nyumba za kulala wageni za hadhi ya juu kutokana na kukua kwa mji wa Ifakara na maeneo ya jirani.
Kwa upande wao wafanyabiashara hao kupitia mwenyekiti wao, Beatus Soka wamepongeza ushirikiano uliopo baina yao, serikali na TRA na kusema kuwa vikao vya mara kwa mara vitasaidia wafanyabiashara wengi kulipa kodi zao kwa wakati bila usumbufu.
Katika kikao hicho pia TRA ilitoa tuzo mbili kwa walipa kodi waliofanya vizuri mwaka jana ambapo taasisi ya Saratani ya Good Samaritan ya Ifakara na mfanyabiashara Didas Kessy kupitia kampuni yake ya Kessy Hardware walipewa tuzo hizo.