Waliofariki ajali  ya basi, Rav4 Moshi watambuliwa

Moshi. Miili ya watu watatu waliofariki kwa ajali ya gari iliyohusisha basi la kampuni ya Esther Luxury na gari dogo aina ya Toyota RAV4 mkoani Kilimanjaro, imetambuliwa.

Ajali hiyo imetokea leo asubuhi, Februari Mosi, 2025 katika eneo la Mdawi, Wilaya ya Moshi, mkoani humo, baada ya dereva wa gari dogo kugongana uso kwa uso na basi la abiria la Esther lililokuwa likitokea Moshi kwenda Dar es salaam.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kuwataja waliofariki kuwa ni  Paul Sita (25) mkazi wa Dar es salaam ambaye alikuwa ni dereva wa gari dogo, Exaud Mbise (65) na Apaikunda Ayo (61), wote  wakazi wa Mkoa wa Arusha.

Kamanda Maigwa amesema  chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva  wa gari dogo kujaribu kuyapita magari mengine,  bila kuchukua tahadhari na kugongana uso kwa uso na basi la abiria la kampuni ya Esther luxury.

“Ajali hii imesababisha vifo vya watu wote watatu waliokuwa kwenye gari ndogo aina ya Toyota Rav4 na kusababisha uharibifu wa magari yote mawili,” amesema.

Kamanda Maigwa amesema miili ya marehemu imehifadhiwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini KCMC kwa taratibu taratibu nyingine.

Akizungumza katika eneo la tukio, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava ametoa pole kwa wafiwa wote na kuwataka madereva kuwa makini barabarani ili kuepusha ajali zinazoweza kuzuilika.

Amesema baada ya kutokea ajali hiyo, abiria waliokuwa kwenye basi la Esther luxury walifanyiwa utaratibu wa kupatiwa gari mbadala kwa ajili ya kuendelea na safari kuelekea mkoani Dar es Salaam.

“Tunashukuru vyombo vya ulinzi na usalama na uokoaji ambavyo baada ya kupata taarifa hizi walifika mara moja eneo la tukio kwa ajili ya kutoa miili na kuhifadhi,” amesema DC Mnzava.

Pia, ameongeza: “Tunaendelea kutoa wito kwa watumiaji wote wa barabara na watumiaji wa vyombo vya moto, kuendelea kufuata taratibu ambazo zote zinaelekeza sheria za usalama barabarani ikiwa ni pamoja na kuangalia usalama wao pamoja na watumiaji wengine wa barabara pamoja na mwendo kasi ambao umekuwa ni chanzo cha ajali,” amesema DC Mnzava.

Ramadhan Issihaka, mmoja wa mashuhuda wa ajali hiyo, amesema ajali hiyo imesababishwa na dereva aliyekuwa akiendesha gari dogo kuwa na spidi kali na kushindwa kulimudu gari hilo na kwenda kugongana uso kwa uso na basi la abiria.

“Ile asubuhi nilikuwa nimesimama pembezoni mwa barabara, gari dogo lililokuwa likielekea Moshi mjini lilikuwa na spidi kali ambapo dereva alikuwa akiyapita magari mengine na kwenda kugongana uso kwa uso na basi ambapo aliburuzwa mpaka akatolewa nje ya barabara,” amesema shuhuda huyo.

Shuhuda mwingine, Josephine Minja amesema dereva wa gari dogo alikuwa kwenye mwendokasi.

“Dereva wa gari dogo ndiye mwenye makosa kwa sababu alikuwa na spidi kali, ajali kama hizi zinaumiza sana. Cha msingi madereva tuwe makini na tusipite magari mengine sehemu ambazo sio sahihi, inatusababishia vifo kama hivi,” amesema shuhuda huyo.

Related Posts