Tanga. Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Batilda Buriani ameagiza wananchi wote waliovamia pori tengefu la Kitwai lililopo ndani ya Kata ya Mkindi wilayani Kilindi mkoani humo, kuondoka wenyewe ndani ya wiki moja kabla ya Serikali kuchukua hatua kali za kisheria.
Akizungumza na wananchi wa vijiji vya Lengusero na Kikwembe kwenye mkutano wa kusuluhisha mgogoro baina ya vijiji hivyo jana Januari 31,2025 wilayani Kilindi, amesema wote waliouziwa na kujimegea maeneo kwenye hifadhi hiyo waondoke mara moja.
Amesema wapo baadhi ya wakulima na wafugaji wamejimegea maeneo ndani ya msitu wa Kitwai hasa sehemu za malisho na kwenye ushoroba kwa ajili ya shughuli za ufugaji na kilimo, kinyume na taratibu za ardhi.
“Kwa wale wote waliouziwa maeneo ambayo hayana matumizi hayo na hawakufuata taratibu za kisheria waondoke, wajue hawapo kihalali na waondoke mara moja,’’ amesema.
Kamishina Msaidizi wa ardhi kanda ya Tanga Tumaini Bwagisa amesema pori tengefu la Kitwai lilianzishwa kwa GN namba 269 ya mwaka 1964 na lilikuwa na vijiji 22,ikiwemo Lengusero na Kinkwembe, lakini tatizo wananchi wamekuwa wakivuka mipaka katika shughuli zao.
Amesema hali hiyo ndio chanzo cha mgogoro wa vijiji hivyo ikichangiwa na uuzwaji wa maeneo yaliyopo ndani ya hifadhi unaofanywa na wananchi wa kijiji cha Kinkwembe.
Kutokana na maagizo hayo Mkuu wa wilaya ya Kilindi, Hashimu Mgandilwa ameagiza wananchi wote ambao wanaendelea na shughuli za ufugaji na kilimo katika eneo hilo kuacha mara moja, kwani hawapo kihalali na ndio wanaosababisha mgogoro kuendelea.
Aidha, Laigwenani wa kata ya Mkindi Yohana Samweli kwa niaba ya wafugaji amesema changamoto ni baadhi ya maeneo kutokuwa na mipango ya matumizi bora ya ardhi kwenye vijiji vyao, hivyo Serikali ya vijiji kwa kushirikiana halmashauri watafute ufumbuzi.
Mkulima Omari Rajabu mkazi wa Mabalanga amesema yeye ameuziwa kihalali mashamba kwenye eneo hilo na kuiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kumpa sehemu nyingine,kwani ana watoto 29 na wote wanategemea eneo hilo kwa shughuli za kilimo.
Pori tengefu la hifadhi ya Kitwai lipo katika wilaya ya Kilindi na Handeni ambapo awali kwenye eneo hilo kulikuwa na vijiji 62 na baada ya kufanyika mapitio ya sheria mwaka 2012 vilipunguzwa na kubaki vijiji 22.