Wanne kortini kwa madai ya kuwatapeli wastaafu

Dar es Salaam. Wakazi wanne wa mkoa wa Kagera na Mwanza, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashtaka 49 yakiwemo ya kutumia laini ya simu iliyosajiliwa kwa jina la mtu mwingine, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha fedha kiasi cha Sh5 milioni.

Washtakiwa hao ni mfanyabiashara Eradius Rwechungura (43) maarufu kama Rwamakala na mkazi wa Kiseke- Mwanza; Heri Kabaju (37) maarufu kama Babylon ambaye ni mchuuzi wa samaki na mkazi wa Rwamisheni mkoani Kagera; Abdurahim Karugila (42) maarufu kama Obra ambaye ni dereva na mkazi wa Kahororo- Kagera pamoja na Eradius Apornary (22)ambaye ni wakala na mkazi wa Kashai Rwamishenyi mkoani Kagera.

Rwechungura na wenzake, pia wanadaiwa kuwapigia simu watu mbalimbali na kujitambulisha kuwa wao ni wakurugenzi wa halmashauri ya wilaya za Kahama, Tunduma, Bukoba, Momba na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kwa madai kuwa watawasaidia kupata kazi ya ualimu, jambo ambalo walijua kuwa ni uongo.

Vilevile, mshtakiwa Kabaju anadaiwa kujitambulisha kama Mkuu wa Mkoa kwa Christopher Msemwa na anahitaji kumfanyia uhakiki wa taarifa zake za utumishi, wakati akijua ni uongo.

Pia, Kabaju anadaiwa kujitambulika kama ofisa utumishi kutoka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kwa mstaafu, Anuciata Mwageni, wakati akijua ni uongo.

Kabaju pia anadaiwa kujitambulisha kuwa yeye ni ofisa kutoka Hazina kitengo cha wastaafu, huku washtakiwa wenzake wakijitambulisha kama maofisa rasilimali watu kutoka wilaya za Njombe, Bukoba na Kahama, wakati wakijua kuwa ni uongo.

Washtakiwa hao wamefikishwa mahakamani jana jioni Januari 31, 2025 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi na wakili wa Serikali Mwandamizi, Nura Manja, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki.

Kabla ya kusomewa mashtaka yao, Hakimu Nyaki alisema washtakiwa hawatakiwi kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi.

Pia, shtaka la kutakatisha fedha linalowakabili washtakiwa hao halina dhamana kwa mujibu wa sheria.

Hakimu Nyaki baada ya kueleza hayo, alielekeza upande wa mashtaka kuwasomea mashtaka washtakiwa hao.

Kati ya mashtaka 49 yanayowakabili washtakiwa hao,  23 ni kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu; 13 kutumia laini ya simu iliyosajiliwa kwa jina la mtu mwingine; 11 kujiwasilisha kwa utambulisho wa mtu mwingine na shtaka moja ni kuongoza genge la uhalifu na jingine ni kutakatisha fedha walizozipata kwa njia ya udanganyifu kwa kuwalaghai watu kuwa watawatafutia kazi.

Akisoma mashtaka yao, Manja alidai shitaka la kwanza ni kuongoza genge la uhalifu na linawakabili washtakiwa wote.

Inadaiwa kuwa washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kati ya Oktoba Mosi na Desemba 31, 2024 katika eneo na mkoa usiojulikana ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, waliendesha genge lenye lengo la kutapeli watu tofauti na kujipatia Sh5milioni.

Shtaka la pili, tatu na kujiwasilisha kwa utambulisho wa mtu mwingine linalomkabili Rwechungura pekee yake ambapo anadaiwa kati ya Oktoba 4 na Desemba 12, 2024 ndani ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania, mshtakiwa kwa kutumia simu iliyosajiliwa kwa jina la Benetson Rwenyagira na Rukia Kombo, alijitambulisha kuwa yeye ni ofisa kutoka wilaya ya Bukoba na Kahama kwa Eliberth Kaliman na Filberth Mashim, wakati akijua kuwa ni uongo.

Shitaka la nne hadi la tisa, lilifanywa na Kaguja kwa kujitambulisha kuwa ofisa kutoka Mfuko wa Hifadhi wa jamii PSSSF kwa Anunciata Mwageni, alijitaja kuwa ni Ofisa kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ili kupata taarifa za muajiriwa Christopher Msemwa pia alidai kuwa ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Njombe kwa Jesca Kibena.

Manja aliendelea kudai kuwa Kabuja alijiwasilisha kuwa ni Ofisa Rasilimali watu kutoka ofisi ya Halmashauri ya Njombe mjini kwa Rustica Kayombo na Upendo Nsellu pia alijiwasilisha kama Muweka Hazina wa Idara ya Pensheni kwa Lucas Nzota huku akijua kuwa si kweli.

Katika shtaka la 10 hadi 12 lilifanywa na Rwechungura kwa kujiwasilisha kuwa yeye ni Ofisa Takwimu kutoka Halmashauri ya Tunduma mjini kwaTupilike Mbwile,  ofisa mradi kutoka Halmashauri ya Momba mjini kwa Elistulida Mwakyusa na ofisa rasilimali watu kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe kwa Emmanuela Mwambichi.

Mashtaka 13 yalikuwa ni ya kutumia laini ya simu iliyosajiliwa kwa jina la mtu mwingine na ilidaiwa walikuwa wakitumia laini zilizosajiliwa kwa majina ya Bazil Katono, Happyness Jems, Aziza Ramadhani, Royce Frenki, Sajda Abed, Valence Rwezaula, Ben Mhimbira, Benetson Rwenyagira na Sabitina Ally.

Vilevile mashitaka 23 ya kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu ilidaiwa kuwa washitakiwa walitenda makosa hayo katika tarehe tajwa wakiwa maeneo yasiyojulikana nchini na kupitiwa kujiwasilisha kwao kwa uongo walijipatia fedha jumla ya kiasi cha Sh5 milioni kutoka kwa watu waliojitambulisha kwao, wakiwaahidi kuwa wangewasaidia kupata kazi ya Ualimu, jambo ambalo ni uongo.

Mahakama iliendelea kueleza kuwa katika tarehe hizo, washtakiwa kwa pamoja na kwa vitendo vyao viovu, walitakatisha fedha kiasi cha Sh5milioni, wakati wakijua kuwa fedha hizo ni mazalia ya makosa yaliyotanfulia ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Baada ya kuwasomea mashtaka yao, upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kwamba wanaomba tarehe nyingine ya kutajwa.

Washtakiwa wamerudishwa rumande hadi Februari 14, 2025 kutokana na shtaka la kutakatisha fedha halina dhamana kwa mujibu wa sheria.

Related Posts