Yanga ilivyorudi kwa Fei Toto

DIRISHA la usajili likiwa limeshafungwa katika ligi za Tanzania, maisha ya soka yanaendelea, kwani kiungo nyota wa ushambuliaji pale Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’ ameendelea kutikisa anga za ndani na nje ya nchi.

Kinachoelezwa ni kwamba, mchezaji huyo aliyewahi kukipiga Singida United na Yanga, mambo yanaendelea kwenda kwa kasi sana kuhusiana na maisha yake.

Wakati kukiwa na taarifa mabosi wa Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini wamepeleka ofa nyingine iliyoongezwa dau ili kumtaka kiungo mshambuliaji wa Azam, Feisal Salum ‘Fei Toto’ waliokuwa waajiri wa zamani wa nyota huyo, Yanga inadaiwa wameamua kurudi kwa mchezaji huyo ili wamrudishe klabuni.

Hata hivyo, ili Yanga iweze kumrejesha tena Fei Toto Jangwani italazimika kutoa dau kubwa zaidi kuliko lile walilomuuza Azam, kutokana na vipengele vya mkataba uliopo baina ya klabu hiyo na mchezaji ambaye inaelezwa msimamo wake kwa sasa ni kutaka kucheza soka la kulipwa nje ya nchi na siyo ndani.

Inaelezwa moja ya kipengele kinachotajwa kuwepo ndani ya mkataba wa Fei Toto ni timu itakayohitaji kumnunua inapaswa kununua mkataba huo au kulipa klabu ya Azam Dola 500,000 (zaidi ya Sh1.2 Bilioni), nje na kile atakachokipata mchezaji huyo.

Fei alijiunga na Azam misimu miwili iliyopita akitokea Yanga katika sakata lililokuwa gumzo baada ya kuamua kususa mwishoni mwa mwaka 2022 kiasi cha Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kuingilia kati katika hafla ya kuipongeza Yanga kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika alipoitaka Yanga kumalizana na mchezaji huyo na siku chache kutangaza kumuuza Azam kwa zaidi ya Sh400 milioni.

Mwanaspoti limezinasa taarifa kutoka ndani za uongozi wa Yanga kutafuta kila njia za kumrejesha Fei Toto kikosini, ikiwemo kutumia njia ya kuzungumza na mama yake mzazi ili amshawishi kijana wake kurudi Jangwani. 

“Viongozi wa Yanga wamefanya mazungumzo na mama yake Fei Toto ili awasaidie kumshawishi aweze kurejea kikosini, sababu ya kufanya hivyo kuna uwezekano mkubwa wa Stephane Aziz Ki kuondoka mwisho wa msimu kutokana na ofa iliyokuja mezani, hivyo mbadala sahihi ni Fei Toto,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;

“Mbali na kuzungumza na mama yake Fei Toto, viongozi wanaangalia njia nyingine itakayowapa uwezekano wa kufanikisha hilo.”

Sio Yanga pekee inayohitaji huduma ya Fei Toto, ilianza kutajwa Simba na Kaizer Chiefs ambayo hadi sasa imeweka mezani ofa ya Dola 365,000 (Sh922 milioni) baada ya awali kuchomolewa na mabosi wa Azam ambao wamesisitiza hawana tatizo mchezaji kuondoka kama watalipwa Dola 500,000.

Kiwango hicho cha fedha ndicho kilichomtoa Prince Dube kutoka klabu hiyo ya Azam kwenda Yanga mwishoni mwa msimu uliopita na kusajiliwa rasmi msimu huu katika njia zinazofanana na zile za Fei Toto alivyotaka kuondoka Yanga kwenda Azam.

Taarifa zaidi zinasema, Fei Toto ni kati ya wachezaji ghali katika kikosi cha Azam na akifikisha mabao 10 ya mashindano yote kwa msimu anakuwa na bonasi ya Sh50 milioni, jambo linaloonyesha timu zinazomhitaji zijipange, japo mwenyewe alinukuliwa hivi karibuni akidai anataka kucheza soka nje, ingawa katika usajili lolote linaweza likatokea.

Related Posts