Dar es Salaam. Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu imesema mikoa ya Arusha na Manyara inaongoza kwa ukeketaji kwa kiwango cha asilimia 43, ikifuatiwa na Mkoa wa Mara kwa asilimia 28.
Hayo yamesemwa leo, Jumatatu, Februari 3, 2025 na Waziri wa wizara hiyo, Dk Doroth Gwajima, alipozungumza na waandishi wa habari kuelekea Siku ya Wanawake Duniani, ambapo kitaifa itafanyika mkoani Arusha.
Dk Gwajima amesema, pamoja na kushuka kwa ukatili huo kutoka asilimia 10 hadi 8, takwimu zinaonyesha kuwa mwaka 2015 na 2016 hadi kufikia mwaka 2023, mikoa ya Arusha na Manyara inaongoza kwa kiwango cha asilimia 43, huku Mara ikiwa na asilimia 28.
Amesema mikoa hiyo imekuwa ikikeketa wanawake na wasichana, jambo linalosababisha kutokwa na damu nyingi, kutojisikia hamu ya kufanya tendo la ndoa, na kusababisha migogoro ndani ya ndoa.
“Inashangaza sana mtu amezaliwa na viungo vyake, iweje umtoe kiungo muhimu kwenye mwili wake? Matokeo yake, akiolewa hajisikii kuwa na mwenza wake katika tendo la ndoa, wanajikuta wanazalisha migogoro ya ndoa,” amesema Dk Gwajima.
Amesema masuala ya ukatili yanasababishwa na masuala ya umaskini, mali, na mila potofu, hivyo, Serikali ikipeleka sauti yake katika mikoa hiyo, zitakomboa familia zinazokutana na ukatili huo.
Pia, amesema maadhimisho hayo yatakayofanyika kilele chake kitakuwa Machi 8, 2025 na yatajumuisha wananchi kupata elimu juu ya usawa wa kijinsia na maendeleo, ili kutokomeza mila potofu na kuwaondolea maumivu wanayokumbana nayo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Jinsia, Badru Abdunuru, amesema wamechagua Arusha kwa kuwa kuna vitendo vya ukatili wa kijinsia, ikiwemo mila na desturi potofu katika vitendo vya ukeketaji.
Amesema katika kipindi cha miaka 30, Serikali imeweka mikakati katika kukuza masuala ya usawa, kwa kuwa kuna mwitikio wa wananchi.
“Bahati nzuri, sera yetu tuliyofanya mapitio mwaka 2023, miongoni mwa vitu vilivyopewa kipaumbele ni suala la kuendeleza jitihada za ushirikishano wa wanaume, ambao ni wakala wa mabadiliko katika jamii,” amesema Abdunuru.
Tanzania ilianza maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani mwaka 1997, hadi sasa imetimiza miaka 30. Maadhimisho hayo ya kitaifa hufanyika kila baada ya miaka mitano, lakini kimkoa hufanyika kila mwaka.