CCM yajivunia 4R, kuwatambulisha Samia na Dk Nchimbi

Dodoma. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimesema kinaamini kuwa falsafa ya 4R itasaidia vyama vya siasa kuendelea kufanya siasa, huku vikitofautiana kiitikadi lakini nchi ikibaki kuwa salama.

Tangu ameingia madarakani Machi 19, 2021, Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Samia Suluhu Hassan, amekuwa akitekeleza falsafa ya 4R, ikimaanisha maridhiano (Reconciliation), mabadiliko (Reforms), ustamilivu (Resilience), na kujenga upya (Rebuilding).

Akizungumza leo, Jumatatu, Februari 3, 2025, jijini Dodoma, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla, amesema chama hicho kinadhimisha miaka 48 Februari 5, 2024, kikiwa ni chama imara chenye wanachama milioni 12 na chenye Serikali.

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla

“Lakini tunajivunia kuwa tunaposherekea miaka 48 ni chama imara, chama chenye wanachama wengi kuliko vyote hapa Tanzania, ni chama ambacho kimeunda Serikali na kinatekeleza ilani yake kwa kiasi kikubwa kupitia miradi mbalimbali ya Serikali zote mbili,” amesema.

Amesema chama hicho kinasherekea miaka 48, wakati kikiwa kimeshinda uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika mwaka 2024 kwa asilimia 98.

Ameongeza kuwa pia wanajivunia amani na utulivu chini ya Serikali mbili za Tanzania na ile ya Mapinduzi ya Zanzibar.

“Nchi yetu ina amani na utulivu pamoja na uwepo wa vyama, nchi yetu tunaendelea kuongozwa na falsafa ya 4R katika kufanya siasa. Ndio maana Chama cha Mapinduzi kinaamini kuwa 4R zitasaidia sana kwa vyama vya siasa kuendelea kufanya siasa tukitofautiana kiitikadi, lakini nchi yetu ikibaki kuwa salama,” amesema.

Amesema sherehe hizo zitaongozwa na Rais Samia, ambapo pamoja na mambo mengine watazitumia kuwatambulisha wagombea urais wa Serikali mbili za Tanzania na Zanzibar, ambao walichaguliwa katika mkutano mkuu uliofanyika Januari 19, 2025, jijini Dodoma kwa wanachama.

Wagombea hao ni Rais Samia, aliyechaguliwa na mkutano mkuu kwa asilimia 100 kugombea nafasi hiyo katika uchaguzi utakaofanyika mwaka 2025, huku Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Emmanuel Nchimbi, akichaguliwa kuwa mgombea mwenza.

Aidha, Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi, alipitishwa na Halmashauri Kuu ya Taifa kugombea nafasi hiyo katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka 2025.

“Ninajua muda utakapofika tutawatambulisha kwa wananchi, lakini kwa kuwa kuna sherehe za CCM tunawatambulisha kwa wanachama wa chama cha Mapinduzi,” amesema.

Mbali na hilo, bendera za kijani na mabango yenye picha za Rais Samia zimewekwa katika maeneo mbalimbali ya jijini, ikiwa ni maandalizi ya sherehe hizo zitakazofanyika katika uwanja wa Jamuhuri jijini Dodoma.

Related Posts