“Halafu wewe utarudi saa ngapi?”
“Atakapokuja nenda jikoni unipigie simu. Umenielewa?’
Nikatoka. Nilipanda teksi nikaenda Ilala kwa Sele. Wakati nafika na yeye alikuwa anafika. Mimi nilishushwa na teksi, yeye alishushwa na bodaboda.
“Unatoka wapi?” Nikakimbilia kumuuliza.
“Ndio natoka benki. Nilikupigia simu nikiwa benki.”
“Ahaa, tumefika pamoja.”
“Umeniambia shangazi amezidiwa?” Akaniuliza.
“Kwa kweli hali yake inatatanisha sana.”
“Sasa kwanini hamumpeleki hospitalini?”
Sikushindwa kujibu swali hilo. Uongo ulikuwa kama chakula changu.
“Hospitalini tunampeleka mara kwa mara lakini ndio hivyo.”
Nilipompa jibu hilo Sele akanyamaza.
Tuliingia ndani, tukaketi sebuleni. Sele akatoa simu yake na kumpigia mtu fulani.
“Tumeshafika tupo hapa nyumbani, naomba uje,” alimwambia mtu huyo kisha akakata simu.
“Unamuita nani?” Nikamuuliza.
Kidogo nikapata hofu, isije kuwa anayeitwa ni Mustafa, akaja kunisuta.
Mbona umeshituka?” Sele akaniuliza.
“Nashangaa uliniita mimi kwa ajili ya mazungumzo yetu, sasa naona unaita mtu mwingine!”
“Yeye pia anahusika katika mazungumzo yetu.”
“Ni nani sasa na anahusikaje?’
“Ni mmoja wa wazee wa mtaani kwangu.”
“Anahusikaje katika mazungumzo yetu?”
“Mimi ndio nataka kumuhusisha, hatuwezi kufanya kila kitu peke yetu.”
Nikaamua kunyamaza ili nimuone huyo mzee.
Baada ya robo saa hivi mtu huyo akawasili. Alikuwa mzee hasa. Alikuwa amevaa kanzu na kofia ya darizi.
“Karibu ukae maalim.” Sele akamkaribisha.
Mtu huyo akakaa karibu na Sele.
“Huyu hapa ndiye yule mchumba wangu ninayetaka kumuoa. Uchumba wetu ulianza siku nyingi lakini ulivunjika nilipokwenda Afrika Kusini.” Sele alimueleza yule mtu kisha akaongeza.
“Kwa bahati mbaya nikiwa Afrika Kusini mwenzangu akaolewa na mtu mwingine lakini kwa vile riziki ilikuwa yangu aliachana na huyo mwanaume…”
“Sasa ndio nimekuelewa vizuri. Kwanza ulinishitua kidogo.” Yule mtu akasema.
“Nilikushitua kwanini?” Sele akamuuliza.
“Kama ulivyonieleza jana, nilipokuja hapa na kumuona huyu msichana nikajua ndiye huyo mchumba wako uliyenieleza. Sasa kilichonishitua ni kwamba huyu msichana namfahamu vizuri aliwahi kuolewa hapa hapa Ilala, halafu aliondoka akaenda kuishi kwa mume wake.”
Nikajiambia kimoyomoyo, leo naumbuka!
“Ni kweli kuwa aliolewa lakini aliachika.” Sele akamwambia.
“Ndio nikasema nimekuelewa. Kwa hiyo ndio mmekubaliana kurudisha uchumba wenu wa zamani?’
“Ndio. Na pia tuko katika mipango ya ndoa. Tatizo lililoko kwa mwenzangu, kama nilivyokueleza ni kuwa wazazi wake wote wawili walishafariki. Alikuwa akiishi na shangazi yake, shangazi mwenyewe hivi sasa ni mgonjwa na hajielewi tena.”
“Kwa hiyo mchumba wangu ameamua kubeba jukumu mwenyewe. Kupokea mahari mwenyewe na kujiozesha mwenyewe.”
“Kwa vile alishaolewa na wazazi hawapo, inajuzu (inakubalika}”
“Sasa ndio nimekuita uwe kama mshenga wangu ingawa mambo yote tumeyamaliza wenyewe, nikukabidhi mahari yake umpatie.”
Sele akafungua mkoba wake na kutoa pesa. Alihesabu shilingi milioni moja akampa yule mtu.
“Ni kiasi gani, mbona ni nyingi sana?’ Yule mtu akauliza.
“Ni shilingi milioni moja. Mwenyewe ametaka shilingi milioni mbili, natanguliza kumpa milioni moja kwanza.”
“Ni za mahari tu au kuna mambo mengine?”
“Mbona ni nyingi sana?”
Kauli yake ile ilinikera sana. Nikaona yule mzee alikuwa mnafiki sana. Inamuhusu nini kama ni nyingi. Wazee hao ndio wanaoozesha mabinti zao kwa shilingi elfu hamsini. Hawajui hata thamani ya mke.
“Si nyingi mzee, kawaida tu.” Sele alimwambia huku akitabasamu.
“Huyu unamuoa chuo cha pili, unampa mahari ya shilingi milioni mbili ingekuwa chuo cha kwanza ungempa kiasi gani?’
“He! Mzee wangu haikuhusu!” Nikajisemea kimoyomoyo. Nilikuwa nimeshapatwa na hasira.
Sijui Sele alimtoa wapi mzee mnafiki yule?
“Mpe tu.” Sele akasema.
Yule mtu kwa unafiki wake alizihesabu tena zile pesa ndipo akanikabidhi.
“Haya mama mahari yako hii hapa shilingi milioni moja,” akaniambia huku akinitazama kwa jicho la kinafiki.
Nilihisi hata yeye alikuwa akizimezea mate zile pesa. Laiti kama angekuwa na binti nyumbani kwake, naona angemshawishi Sele amuoe mwanawe ili apate zile pesa.
Nikazipokea zile pesa na kubaki nazo mkononi. Uso wangu haukuficha hasira niliyokuwa nayo.
“Mama mbona umekasirika?” Yule mtu akaniuliza akionyesha kunistukia nilivyobadilika.
“Naona kama umekunja uso.”
“Mzee nakushukuru sana.” Sele akamkatiza. Alifanya vizuri kwani ningeweza kumpa maneno machafu pale pale.
“Nilitaka kujua ndoa yenu itakuwa lini?” Mtu huyo akauliza.
“Ndio tuko katika mipango, nitakuarifu.”
Mtu huyo akacheka lakini pia niliona kilikuwa kama kicheko cha kinafiki.
“Sawa bwana, nawatakia heri na fanaka katika ndoa yenu. Kuna kingine au tumemaliza?”
“Suala la leo tumelimaliza, nakushukuru sana.”
“Basi mimi naondoka niwaache muendelee kupanga.”
“Ngoja nikutoe.” Sele akamwambia huku naye akinyanyuka.
Mkono wa Sele ulikuwa umeingia kwenye mfuko wa suruali yake, nikajua alikuwa anakwenda kumpa chochote huko nje. Wakatoka.
Waliponiacha nilizitia zile pesa kwenye mkoba wangu. Baada ya muda kidogo Sele akarudi na kuketi.
“Mzee huyu umempata wapi Sele?” Nikamuuliza.
“Ni mzee wa mtaani kwetu.”
“Anauliza maswali kama mpelelezi, wazee wa aina hii mimi siwapendi.”
“Umemfikiria vibaya tu lakini ni mtu mzuri.”
“Uzuri wake ni kudadisi mambo ya watu?’ Nikamuuliza Sele huku nikiwa nimekunja uso.
“Amekudadisi kitu gani?”
“Kwani hukumsikia akikuhoji kuhusu hizi pesa, anasema ni nyingi. Zinamhusu nini?’
“Hayo yameisha Mishi, aliuliza tu si unajua wazee wa Kiswahili wakiona pesa.”
“Anajidai anazihesabu, kwani amepewa yeye? Unafiki mtupu!”
“Alizihesabu ili kuzihakikisha kama ziko sawa.” Sele akaniambia.
“Lakini haikumuhusu, ule ni unafiki tu.”
“Basi achana naye, kumbe amekuudhi sana!”
“Sasa tupange ndoa yetu, ungependa tuoane lini?’
“Kwani unataka ndoa ya sherehe?”
“Lazima sherehe iwepo.”
“Kumbe ulitaka iwe wapi?”
“Tuoane hotuba tu, sherehe iwe baadaye.”
“Shangazi yangu anaumwa, sherehe ya nini?”
“Kwa hiyo tusubiri atakapopata nafuu ndio tufanye sherehe?”
“Nadhani hivyo ndio itakuwa vizuri zaidi. Tukifanya ndoa ya sherehe watu hawatanielewa kabisa.”
“Ili kurahisisha mambo, tutaoana hapa hapa kwako. Mimi nitakuwa chumbani, wewe utakuwa ukumbini. Utaozeshwa na shehe wako kisha utakuja chumbani kunipa mkono. Ndoa itakuwa imeshapita. Au waonaje?”
“Itakuwa ndoa ya kimya kimya sana.”
“Inabidi iwe hivyo, mimi sitaki sherehe yoyote kwa sasa kwa sababu ninamuuguza shangazi yangu, angekuwa mzima tungefanya sherehe lakini ni mgonjwa, sherehe ya nini?”
Sele alifikiri kisha akasema.
“Sawa. Tutakuja kufanya sherehe yetu wakati mwingine.”
“Hayo yanafanyika sana.”
“Rafiki yangu mmoja pia alioa kwa mtindo huo. Alikuja kufanya sherehe baadaye.”
“Sasa kwa vile tumerahisisha mambo tuharakishe ndoa yetu.”
“Sawa, basi nitakwambia siku.”
Wakati ule nazungumza na Sele nikasikia simu yangu ikiita ndani ya mkoba wangu. Ilikuwa na mlio hafifu ambao niliweza kuusikia mimi mwenyewe.
Nikapatwa na wasiwasi. Sikujua ni nani aliyekuwa akinipigia. Ni Mustafa au ni mtumishi wangu.
Nikanyanyuka ghafla na kumwambia Sele ninakwenda kujisaidia. Niliondoka na mkoba wangu, nikaenda maliwatoni. Nilipoingia nilitoa simu yangu na kutazama namba ya aliyekuwa akinipigia. Nikashituka nilipoona namba ya mtumishi wangu wa Mbezi.
“Unasemaje?’ Nikamuuliza kwa sauti ya kunong’ona ili isisikike.
“Baba amekuja.” Mtumishi huyo akaniambia kwenye simu.
“Hivi sasa yuko nyumbani?’ Nikamuuliza.
“Ndio ameingia sasa hivi, nimemwambia uko kwa jirani.”
“Ameguna tu kisha akaingia ndani.”
“Kuna kitu chochote alicholeta?”
“Ameleta nyama ya mbuzi.”
“Basi subiri nakuja sasa hivi.”
Hapo hapo nikapata wazo jingine.
“Unanisikia?” Nikamuwahi kabla hajakata simu.